MGOMBEA nafasi ya urais wa Shirikisho la Mpira Miguu Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani amejinadi kusimamia na kutekeleza programu ya muda mfupi na mrefu ya shirikisho hilo na kuwa hawanii nafasi hiyo akiwa na ilani yake ya uchaguzi binafsi.
"Chama chochote hata cha siasa, hupitisha mgombea wao na wenye chama hutengeneza sera ya chama hicho itakayotekelezwa na serikali yake kwa maendeleo ya eneo husika na si mtu," alisema Nyamlani alipozungumza wanahabari kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam, jana.
"Katika soka huwezi ukawa na ilani ya uchaguzi hata kidogo, umekaa na shemeji yako ama rafiki tu, mseme soka la Tanzania liwe hivi, haiwezekani, yapo makundi ya ufundi ya kiutaalamu yenye kupewa jukumu hilo na taasisi kutengeneza programu za maendeleo na si itoke mfukoni mwangu," alisema
"Kama kiongozi unatoa mapendekezo yako kwa kamati ya utendaji, kinachangiwa na wenzako nao wanasema na hata kilichopo sasa katika makrabasha ya TFF si msaafu, kinaweza kuongezwa kitu ama kutolewa, lakini si mawazo yangu peke yangu yaendeshe soka la Tanzania, hilo haliwezekani."
Alisema yeye ni miongoni mwa watu waliomsaidia kwa ukaribu, Leodegar Tenga kuweka misingi ya utawala bora, kiasi kwa sasa hakuna kiongozi wa chama chochote kilicho chini ya TFF ikiwemo klabu, kuwa na migogoro inayozaa kufukuzana.
"Kwanza unaimarisha utawala bora, hapo panakuwa na amani, baadaye unakwenda kwenye udhamini na kujenga misingi ya mpira wa miguu, kwa kufanya hivyo ni rahisi mpira kuchezeka, lakini penye migogoro na chama kutokuwa na amani, hakuwezi kuwepo mtu wa kuwekeza, hilo sisi tumefanikiwa," alisema.
Alijinadi kuwa, kamwe hatafumbia macho rushwa na hilo ni jambo jema iwapo atafanikiwa kwa kuwa siku za nyuma ilikuwa ni vigumu kutoa maamuzi ya aina yoyote katika hilo, kwa kuwa, hakukuwa na vyombo vinavyoshtaki na kutoa hukumu za aina hiyo ndani ya katiba ya TFF, wala kujitetea kwa kukata rufaa.
"Ilikuwa kama kuna mshukiwa inapaswa kupelekwa Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), baadaye mahakama za kiraia, hivyo sisi kukosa meno ya eneo hilo kwa hukumu za aina yoyote zitolewazo huko, katiba ya sasa ya TFF iliyofanyiwa marekebisho katika mkutano mkuu wa mwisho, vilipitishwa vyombo hivyo, ikimaanisha sasa kinachotakiwa ni utekelezaji kivitendo bila kumuonea mtu," alisema.
Kuhusu kamati za TFF kutofautiana maamuzi, alisema hilo lipo popote pale penye utawala bora.
"Hata sisi kwenye kamati ya rufaa ya CAF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika), mara nyingine tunatofautiana na kamati ya utendaji, ama hata mahakama haiwezekani lazima maamuzi yatolewayo na kamati moja, nyingine zote lazima ziunge mkono, hiyo si sahihi mahala popote penye utawala bora," alisema.
"Nashukuru nimekuwa katika mpira wa miguu kuanzia uongozi wa klabu, mjumbe kamati utendaji Tefa, katibu msaidizi Tefa, katibu mkuu Tefa, katibu msaidizi DRFA, katibu mkuu DRFA, mjumbe kamati ya muda FAT na makamu wa kwanza wa rais TFF, wadhifa nilionao hadi sasa, nina uzoefu wa kutosha na ninajua majukumu makubwa ninayotarajia kukumbana nayo katika changamoto za soka la Tanzania."
Alipoulizwa kuhusu madeni yaliyosababisha kufungiwa akaunti za TFF, alijibu " kudaiwa na kudai ni sehemu ya maendeleo," kicheko kikatawala ukumbini hapo kwa wanahabari na kufafanua, lilikuwa ni suala la kukaa pamoja kati yao na TRA sanjari na serikali waliokuwa wakimlipa Kocha Marcio Maximo, akifafanua wajibu wa mlipamshahara na hilo lilimalizwa baada ya kukaa pamoja.
Alisema amekuwa katika nafasi ambayo imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa uwazi, ikiwa ni chama ama taasisi pekee Afrika Mashariki inayotangaza mapato yake, hasa ya mechi kubwa siku mbili tu, baada ya kupatikana, hiyo ikiwa na pamoja na mahesabu yao kukaguliwa na mkaguzi anayetambulika.
Kabla hawajaingia madarakani, ilikuwa ni taasisi ambayo mwenyekiti anaweza kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari, siku inayofuatia ikipingwa na katibu wake, jambo ambalo kwa sasa alidai ni historia, hiyo ni kutokana na mfumo kufanya kazi na si mtu.
Kuhusu kazi yake na nafasi anayoomba ni kwa jinsi gani anaweza kujigawa, Nyamlani alijibu kuwa, wakati wanaingia madarakani hata mhudumu ilikuwa ni jambo gumu sana kumlipa, madeni yao ya malimbikizo ya mishahara yalikuwa lukuki.
Lakini kadri siku zinavyokwenda, kuna waajiriwa wengi ndani ya TFF, hivyo ikifika rais awe wa kuajiriwa, hilo litafanyika, lakini katiba ya sasa haisemi rais wa kuajiriwa, basi si vyema tukawa na rais asiyekuwa na kazi kwani mshahara wake haumo kwenye makabrasha yoyote ya kujilipa.
"Hata Fifa enzi za Joao Havellange, rais hakuwa wa kuajiriwa, Sepp Blatter akiwa katibu, lakini kwa sasa katibu wa Fifa ni kama msaidizi tu wa rais, kwani rais ni mtendaji na aliye katika ajira, hiyo ilifanywa na wanachama wa Fifa kubadilisha katiba yao, hivyo nasi tukifikia huko basi haitakuwa budi, lakini kwa sasa ni vyema nafasi zetu za juu ziwe na watu wenye kazi zao," alisema.
Alisema kutokana na ushirikiano mzuri na FIFA, uongozi wake akiwa chini ya Tenga umepata kiwanja katika Manispaa ya Tanga na wamepeleka mapendekezo yao ya kupata msaada wa ujenzi FIFA, wamekubaliwa ambapo utajengwa uwanja ambao utakaomilikiwa na Shirikisho hilo, itakuwa ni hatua kubwa, na mikoa mingine itafuatia kutokana na kufanikisha mipango ya awali.
"Wakati naomba ridhaa ya kuongoza nafasi ya makamu wa rais, nilijinadi kuwa, nitapendekeza kwa kamati ya utendaji mikoa ipate ruzuku, kitu ambacho hakikuwepo awali, imefanikiwa ingawa kwa kiasi kidogo sana, lakini japo kiwasaidie kulipia pango la nyumba, yaani sh. milioni 2 kwa mwaka, lakini naahidi kuboreshwa kwa ruzuku hiyo isiwe chini ya sh. milioni 5," alisema.
Akijibu hoja ya kutelekezwa vijana wa Copa Coca Cola, Nyamlani alijibu kuwa si kweli, kwani sasa asilimia 90 ya wachezaji wa ligi kuu Tanzania Bara wanatokana na zao la Copa Coca Cola, akiwemo Mbwana Samatta aliyekuwa akiichezea Temeke.
"Simba na Azam, vijana wanaojivunia zao nl Copa Coca Cola na Uhai Cup, sasa ni vipi watu wanashindwa kufanya utafiti mdogo tu kwa hilo, jamani hata Ulimwengu (Thomas), yule katokea huko," alitolea mfano wachezaji hayo.
"Wanahabari mmeshuhudia mechi za ligi, timu za vijana zikicheza kabla na kandanda la hali ya juu mnashuhudia, huko nyuma haikuwa hivyo, hilo ni sharti letu, lazima klabu ziwe na timu za vijana," alisema.
Kuhusu soka la vijana na wanawake, alisema mwaka huu ligi ya Copa Coca Cola ilikuwa ni sharti la kila mkoa kupeleka wachezaji wenye umri chini ya miaka 15, kwa jinsia zote hizo, sasa ni rahisi miaka michache ijayo kuwa na chaguo pana la wacheaji wa timu ya taifa, hilo linatokana na nyakati za nyuma kuchaguliwa katika wigo mfinyu sana kwa kukosa program za kusaka na kutengeneza vipaji.
0 comments :
Post a Comment