“Inashangaza
sana kuwa wale wanaotajwa hawachukuliwi hatua, lakini wananchi wanazidi
kuteseka… Mathalani, zipo taarifa kuwa wakuu wa polisi katika mikoa
inayopakana na Mbuga ya Serengeti ndio waratibu wa shughuli za ujangili,
lakini hatujasikia hao wakichukuliwa hatua,”
Dodoma. Wabunge
jana walichachamaa na kushinikiza kutolewa kwa orodha ya vigogo
wanaojihusisha na ujangili wakati wa kikao cha kwanza cha mkutano wa 13
wa Bunge unaofanyika mjini Dodoma.
Wabunge hao walitaka kutajwa kwa majina ya mawaziri, viongozi wa Serikali na wabunge wanaojihusisha na biashara hiyo.
Baada ya kumalizika kwa kipindi cha
maswali na majibu, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, aliomba
mwongozo, akiitaka Serikali kuwataja hadharani na kuwachukulia hatua
viongozi wake na wanasiasa, wakiwamo mawaziri na wabunge, ambao
wanatajwa kuhusika na vitendo vya ujangili nchini.
Lugola aliomba mwongozo wa Naibu Spika
baada ya kutoridhishwa na jibu lililotolewa na Naibu Waziri wa Maliasili
na Utalii, Lazaro Nyalandu, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge
wa Kahama (CCM), James Lembeli.
Katika jibu hilo, Nyalandu alilieleza
Bunge kuwa Operesheni Tokomeza inayolenga kukomesha vitendo vya ujangili
nchini bado inaendelea, lakini alishindwa kulieleza Bunge ni nani hasa
wamebainika kuhusika na vitendo hivyo.
Lugola, hata hivyo, aliitaka Serikali kuwasilisha ripoti bungeni kuhusiana na utekelezaji wa operesheni hiyo.
“Tangu Aprili tumekuwa tukipewa majibu mepesi kuhusiana na operesheni hii, wakati suala hili si la masihara,” alionya Lugola.
Lugola alisema kuwa taarifa zimewataja
watu wanaohusika na vitendo hivyo wakiwamo viongozi serikalini, mawaziri
pamoja na wabunge, lakini tangu operesheni hiyo ilipoanza hakuna yeyote
miongoni mwa hao wanaotajwa ambaye amekamatwa isipokuwa wananchi wa
kawaida.
Alisema operesheni hiyo imekuwa
ikiendeshwa kwa unyama kwani wanaokamatwa hupigwa na kuteswa bila ya
ushahidi unaoonyesha kuhusika kwao na vitendo vya ujangili.
“Inashangaza sana kuwa wale wanaotajwa
hawachukuliwi hatua, lakini wananchi wanazidi kuteseka… Mathalani, zipo
taarifa kuwa wakuu wa polisi katika mikoa inayopakana na Mbuga ya
Serengeti ndio waratibu wa shughuli za ujangili, lakini hatujasikia hao
wakichukuliwa hatua,” alisema.
Kabla ya Naibu Spika kutoa majibu ya
mwongozo ulioombwa na Lugola, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri
Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama na kukiri
kuwapo kwa vitendo vya utesaji wa watu wanaokamatwa katika operesheni
hiyo.
Alitolea mfano tukio la kukamatwa kwa
msaidizi wake jimboni ambaye alipigwa na kuteswa na askari hao kabla ya
kuachiwa baada ya kushikiliwa kwa siku moja, huku akionyesha kuwa
ushahidi wa tukio hilo anao kwenye simu yake.
“Lakini
sisemi haya kwa kutaka kuitetea Serikali kuwa isilete ripoti hapa
bungeni. Nadhani kuwa kuleta ripoti hivi sasa haitakuwa vizuri. Ni
vizuri tusubiri mpaka kazi hii ikamilike na nina uhakika kuwa Wizara
itaandaa ripoti na kuiwasilisha kwenye kamati husika,” alisema na
kuongeza:
“Nadhani kuwa `entry point’ (mahali pa kuanzia) yetu iwe ni kwenye ripoti hii itakayowasilishwa kwenye Kamati,”
Suala
la ujangili limeingizwa bungeni wakati kukiwa na usiri mkubwa wa nani
anahusika na vitendo hivyo, huku majina ya vigogo wanaotajwa kuhusika
nayo wakiwa hawafahamiki.
Polisi watajwa vinara
Awali
akijibu swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk
Faustine Ndugulile, Nyalandu alisema Jeshi la Polisi ni vinara miongoni
mwa makundi manne ya majeshi ambayo watumishi wake wamekamatwa
wakijihusisha na ujangili.
Katika
matukio saba ya ujangili yaliyowahusisha watumishi tisa wa vyombo vya
ulinzi na usalama, Nyalandu alisema kati ya hao sita ni polisi wakati
kwa kupande wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa
(JKT) na Magereza alikamatwa mtu mmoja mmoja.
“Katika
matukio hayo, jumla ya meno ya tembo 686 na vipande 447 vikiwa na uzito
wa kilogramu 4,253.9 vilikamatwa, jambo ambalo linaonyesha ukubwa wa
tatizo hilo kwa vyombo vya ulinzi,” alisema Nyalandu.
Katika
swali la msingi, Dk Ndugulile alitaka kufahamu idadi ya matukio ya
upatikanaji wa pembe za ndovu yaliyohusisha vyombo vya ulinzi na
usalama.
Katika
swali la nyongeza, Lembeli ambaye ndiye aliyeuliza swali hilo kwa niaba
ya Dk Ndugulile, aliitaka Serikali kuacha kigugumizi na kueleza ukweli
kuwa wapo baadhi ya viongozi, wakiwamo wabunge ambao wamekuwa
wakijihusisha na biashara hiyo.
“Katika
biashara ile kuna hali ya kulindana sana, hebu Serikali itueleze
taarifa za kuwa wahusika wengine ni wanasiasa na baadhi ya wabunge,
ukweli uko wapi, na kuna taarifa kuwa viongozi wa Polisi wanaoishi
kuzunguka hifadhi zetu ndio ambao wanatumiwa kusafirisha nyara hizo,
Serikali inasemaje?” alihoji Lembeli.
Nyalandu
alisema Tanzania iko katika hali mbaya katika kiwango cha mauaji ya
tembo ambapo wastani unaonyesha kuwa kila siku tembo 30 huuawa na
majangili.
“Hata
hivyo, suala la ulinzi bado tuko nyuma sana kwani wastani wa ulinzi wa
kimataifa ni askari mmoja kwa kilomita za mraba 25, lakini sisi askari
wetu mmoja analinda kilomita za mraba 150 ndani ya hifadhi,” alisema
Nyalandu.
0 comments :
Post a Comment