Imeandikwa na Bongo5,com
Nikiwa na begi langu lenye camera ya kazi, niliwasili Leaders Club
mapema mida ya saa 2 kasoro hivi usiku. Nakubali, ndio nilienda mapema
mno. Si kwasababu nilikuwa nimeipania show ya P-Square, lahashaa.
Nilihitaji tu kuwasili mapema ilimradi nisipitwe na kila jambo muhimu
litakalotokea.
Nje ya Leaders, ulinzi ulikuwa mkali mno. Walionekana askari wengi
kuanzia kwenye kona ya kwanza ya kuingia Leaders baada ya kuiacha
barabara ya lami. Muonekano huo tu, ukanipa faraja kubwa kuwa mali na
watu muda wote wa show watakuwa salama.
Kulikuwa na njia moja tu ya kuingilia iliyogawanishwa katika vimilango
vingine zaidi ya sita vilivyosimamiwa na askari wa ulinzi waliokuwa na
sare zao. Hapo nikakaguliwa kwa vifaa maalum kuanzia chini na ndani ya
begi langu ili kuangalia kama nilikuwa na bomu ndani… Lol… usishtuke,
nilikuwa nimebeba camera yangu tu, hakuna kingine. Itifaki ilizingatiwa.
Ndani palikuwa pameshaanza kuchangamka. Kwa mbali nilimuona DJ Sama
kwenye 1 na 2 akifanya yake kama wasemavyo wenyewe wazee wa East Africa
Radio. Eneo la mbele jirani na jukwaa tayari palikuwa pamejaa. Watu
wengi hasa wazungu waliokuwa wamechangamka kiaina, walionekana kukunwa
na burudani hiyo na kucheza kwa raha zao.
Kwa pembeni kidogo kulikuwa na sehemu ya VIP iliyokuwa imetengwa na
Hennesy. Palikuwa pametengenezwa vizuri na wale walioweza kumudu
walijimwaya kule.
Mwanzoni palianza kama kuboa kiaina, hivyo nikaenda pembeni kidogo
kutafuta kinywaji changu kupoza koo. Kama kawaida pembezoni mwa uwanja
kulikuwa na vibanda kadhaa vilivyokuwa vikitoa huduma ya bites na misosi
mbalimbali.
Haukupita muda mrefu, washereheshaji wa siku hiyo, Dulla Mjukuu wa Ambua
na T-Bway walivamia stage kutokea chini kwa ngazi maalumu
zilizotengenezwa kupanda zenyewe kutoka chini hadi juu huku wao wakiwa
wameinama kama kiumbe cha ajabu kilichoanguka kutoka mawinguni.
Shangwe zilitawala baada ya wawili hao kuanza kutangaza na kuwapandisha
watumbuizaji wa kwanza, dancers walioshinda shindano la Dance 100.
Sikupenda performance yao japo walipata shangwe za hapa na pale. Sababu
kubwa ya kutopenda kile walichokifanya ni aina yao ya uchezaji kwa
kutumia zaidi sauti za effects na si kwa kucheza kwenye wimbo
unaoeleweka. Kingine ni utengezaji wao mbovu wa megamix yao iliyokuwa na
nyimbo fupi na ambazo hazishiki.
Performance ya kwanza ya kueleweka ilianza baada ya Ben Pol
aliyesindikizwa na msanii wake Alice kupanda. Akiwa amevaa koti la rangi
ya blue bahari lilitengenezwa na mbunifu wa mavazi, Pedaih wa PSJ
Couture, Ben Pol alionesha ukomavu katika uimbaji wake kwa kutumbuiza
hits zake zote kwa ustadi mkubwa.
Alifuatia Lady Jaydee na dancers wake. Mkongwe huyo alikuwa amevalia
mavazi kama askari jeshi wa kike anayeshiriki kwenye gwaride na
kupendeza sana. kama kawaida yake, Lady Jaydee alizikonga vyema nyoyo za
waliohudhuria kwa kutumbuiza nyimbo zake za zamani na za sasa zikiwemo
Yahaya na Joto Hasira.
Wakati akiimba Joto Hasira ndipo alipomkaribisha rasmi Profesa J
kuchukua usukani wa show. Profesa alikuwa amesindikizwa na rapper ambaye
sijawahi kumuona lakini aliyemudu vyema kumpa tafu Mchawi huyo wa
rhymes kufanya show nzuri pia.
Niseme wazi, Joh Makini ndiye aliyekuja kuipa uhai hip hop. Japokuwa
yeye hakuwa akipigiwa vyombo na bendi, show yake iliwasha moto Leaders
Club. Mwamba huyo wa Kaskazini alitumbuiza nyimbo zake zote zilizohit na
nusu ya uwanja ulisikika ukimalizia mashairi yake. Kuanzia Higher,
Stimu Zimelipiwa, Hao, Niaje ni Vipi, Manuva na zingine.
Joh Makini
Joh Makini
Baadaye, Joh alikuja kupewa kampani na Weusi, Nikki wa Pili na G-Nako na kuongezea nyimbo zingine, Nje ya Box na Bei ya Mkaa.
Mpaka Weusi wanaondoka kwenye stage, wapenzi wa burudani walikuwa tayari kuumudu moto uliokuwa unakuja wa P-Square.
Alikaribishwa DJ Mafuvu kuwaweka sawa kwanza na ndipo bendi yenye watu wanne tu ilipanda kuweka sawa vifaa vyao.
P-Square walipopanda, uwanja mzima wa Leaders Club ulizalisha shangwe
nene kuwakaribisha. Peter na Paul wakaanza kuangusha fire. Kitu kimoja
ambacho mimi kiliniacha mdomo wazi, ni muziki mzito uliokuwa ukipigwa na
watu wanne tu, na kufanya uonekane kama unachezwa na watu zaidi ya 10.
Bendi ya P-Square inajua haswaaa. Ilikuwa ikipiga nyimbo zao kwa ustadi
kiasi ambacho ilikuwa rahisi mno kuyadanganya masikio yako kuwa
unachokisia pale huenda sio live bali ni CD. Tofauti yake ni kuwa,
P-Square wanajua mno kutengeneza ladha tofauti ya nyimbo zao na
kuzifanya ziwe tamu zaidi zinapoimbwa live. Kwa mfano, walikuwa wakianza
kwa kuimba kama slow na baadaye kuja kuuimba wimbo kwa namna
ulivyozoeleka.
Kwa namna ambavyo walikuwa wakilitawala jukwaa, ni halali P-Square wawe
wasanii wanaolipwa zaidi barani Afrika. Si kwa maneno tu, nimeamini
kuwa, ni wasanii wachache sana wa Afrika (ukiwatoa DRC) wenye uwezo wa
kutumbuiza vizuri zaidi live. Nadiriki kusema kuwa, unaweza kuwaweka
Davido, Iyanya na Wizkid pamoja lakini hawawezi kufikia uwezo wa mapacha
hawa.
Kuna mambo kadhaa niliyojifunza kwenye show hiyo ambayo ni pamoja na:
Kutengeneza versions tofauti za nyimbo
Hiki si kitu kipya sana, na wasanii wengi hufanya hivi pale wanapokuwa
wakiimba live. Lakini P-Square walinigusa zaidi kwa jinsi wanavyofanya
wao. Baadhi ya nyimbo zao za kuchangamka ambazo nilitegemea
wangezikimbiza kama kawaida, walizitengenezea ladha nyingi tamu ya
kusikilizika zaidi. Hakuna wasiwasi kuwa, jamaa hawa hufanya mazoezi
makali na bendi hiyo na kila wimbo ulibadilishwa na kupigwa katika aina
ambayo usingeweza kuona hata chembe ya kosa.
Nyimbo zilizokuwa zinagusa mapenzi na uhusiano waliziimba kwa hisia kali
na kwa uwezo wao wote. Huu ulikuwa ni uimbaji kama wa msanii mchanga
aliyependa kwenye stage kubwa kama ile kwa mara ya kwanza na anayetaka
kuwadhihirishia watu kuwa ana uwezo mkubwa.
P-Square walitumbuiza kama si wasanii wale matajiri tunaowafahamu. Kwao
kila show ni muhimu na ni lazima wazikonge nyoyo za mashabiki.
Peter
Peter
Bendi ni zaidi ya wafanyakazi, ni familia..
Peter alisema wapigaji wa vyombo wa bendi yao ni watu waliokuwa nao
tangu enzi za utoto miaka iliyopota. Ni washkaji zao wanaotembea nao
kila mahali. Uhusiano uliopo kati ya P-Square na bendi hiyo ni mkubwa
kiasi cha kuchukuliana kama familia. Uhusiano huo ndio unaoleta kile
nilichokishuhudia siku ile.
Kuengage na mashabiki
P-Square si wasanii tu, ni entertainers. Nilifurahishwa na uwezo wao
mzuri wa kuwashirikisha watazamaji kwenye show yao. Kwa mfano
walianzisha mashindano ya kizushi pale pale jukwaani ili kuonesha nani
kati yao ndiye mwenye kipaji zaidi. Mwanzoni Peter alivuta juu shati
lake na kuonesha six pack yake kifuani, huku Paul akidai kuwa yeye hana
six pack bali anayo one pack kubwa zaidi na kutoa suruali yake kubaki na
boxer, hali iliyoamsha shangwe za hatari.
Baaadaye Paul alikamata gitaa la besi akitaka aoneshe uwezo wake. Peter
akasikika akisema, amekua pamoja kwenye nyumba moja na hajawahi kumuona
kaka yake akipiga gitaa. ‘His name is Paul Okoye, Paul Okoye disgrace
yourself,’ alisema Peter. You got one pack, show them one pack or 2
pack, go go let me see,’ aliongeza. Akiwa ameshika gitaa lake, Paul
alisema ‘I am about to do 2 Pac, let’s go’ na ndipo alipoanza kupiga
bass ya wimbo wa 2 Pac ‘Do For Love’, bendi ikampokea na Peter kuanza
kuimba chorus ya wimbo huo.
Baada ya hapo Peter alishikaa gitaa la solo na kucharaza wimbo wa Ja
Rule aliomshirikisha Ashanti, Always on Time kabla ya kupiga wimbo wa
The Product G&B na Wyclef – Cluck Cluck.
Surprises
Peter Okoye ametoka kufunga ndoa hivi karibuni lakini ili kuwafurahisha
zaidi watu aliamua kumkosea kidogo mkewe Lola Omotayo kwa kumfanyia
surprise msichana mrembo aliyekuwa pale. Alimpandisha juu mrembo huyo na
kumvalisha saa yake kabla ya kumbusu na kuibua shangwe zito Leaders
Club.
Mrembo akivishwa saa na Peter
Mrembo akivishwa saa na Peter
Hakuna anayeweza kuiongelea vibaya show hiyo iliyohudhuriwa na watu wa kila aina wakiwemo wazungu kibao wa mataifa mbalimbali.
Ilikuwa ni show ya watu wengi lakini iliyokuwa na heshima kubwa. Kwa
aina ya watu wale waliohudhuria siku hiyo, nilipata picha kuwa burudani
ni kiwanda kikubwa kinachoweza kuwapa kipato kikubwa si tu wanamuziki
wanaotumbuiza, bali waandaji wenyewe pia kama tu kila kitu kikifanywa
vizuri.
Hakikuwa kitu cha kawaida Leaders kujaa vile ilhali kiingilio kilikuwa
ni shilingi 35,000 hadi 50,000 uwanjani. Inawezekana kabisa kufanya
maandalizi kama hayo kwa kutumia wasanii wa hapa hapa nyumbani na kwa
kiingilio kama hicho, kwa kuweka bendi ya uhakika na wasanii wakalipwa
mathalan shilingi milioni 50 kila moja.
Kwa mfano huo, waandaaji wa matamasha wanaweza kutengeneza tamasha la
muziki (music festival) la hata siku tatu mfululizo na kama line up ya
wasanii ikiwa ya kueleweka na muziki upigwe live, Dar inaweza kuwa na
tamasha lake sawa na Sauti za Busara lilivyo.
Niwapongeze sana East Africa Radio kwa maandalizi mazuri ya show hiyo.
Watu wengine wanaoandaa matamasha kama hayo, wajifunze kitu kutoka
kwenye show hiyo ili tukuze zaidi kiwanda cha burudani nchini.
Bongo5,com
0 comments :
Post a Comment