STRAIKA wa Mbeya City, Mwagane Yeya, alitofautiana na baba yake mzazi aitwaye, Yeya Mwanavyembe, kwa muda wa mwezi mmoja alipoifunga Yanga kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mwagane alifunga bao hilo kwenye Uwanja Sokoine
jijini Mbeya katika mechi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1. Alipofunga
alifurahi pamoja na wachezaji wenzake, lakini hali haikuwa shwari kwa
mzazi wake huyo ambaye anaipenda Yanga na ni shabiki mkubwa wa klabu
hiyo ya Jangwani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwagane ambaye alikiri
kuwa alipokuwa mdogo naye alikuwa anaishabikia Yanga akifuata nyayo za
baba yake, lakini anasema alipopata akili za utu uzima akazamisha mawazo
yake kwa Mbeya City anayoipenda kwa nguvu zote.
“Familia yetu inaipenda Yanga, baba yangu ndiyo
haumwambii lolote kuhusu Yanga. Siku ile tulipocheza nao pale Sokine
mzee alikasirika kwanini niliwafunga, yaani ulipita kama mwezi mmoja
hivi hatukuwa na maelewano mazuri na mzee,” alisema.
“Lakini baadaye nilikaa naye nikamwelewesha, nashukuru Mungu alinielewa na tukayamaliza.”
Mwagane ndiye mchezaji mwanzilishi wa Mbeya City, aliichezea tangu ilipoanzishwa hadi ilipopanda Ligi Kuu.
Mbali ya kucheza, Mwagane pia ni mwalimu wa Shule
ya Sekondari Iduda, Uyole na ndiye nahodha wa timu hiyo inayoshiriki
ligi hiyo kwa mara ya kwanza lakini imeleta changamoto kubwa.
No comments:
Post a Comment