Balozi Seif akiwa pembezoni mwa dirisha ndani ya chumba cha chini ya Bahari akiangalia samaki n...
Balozi
Seif akiwa pembezoni mwa dirisha ndani ya chumba cha chini ya Bahari
akiangalia samaki na mazingira yake mara baada ya kuuzindua mradi huo
hapo Manta Resort Hoteli Makangale.
Balozi
Seif akiangalia ngazi ya kutokea juu ya chumba cha chini ya Bahari
katika Hoteli ya Manta Resort Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba kwenye
sherehe za uzinduzi wa chumba hicho ikiwa ni muendelezo wa sherehe za
kutimia miaka 50 ya mapinduzi ya Zanzibar
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimpongeza Meneja Mkuu wa
Hoteli ya Manta Resort Bwana Methew Saus kwa kukamilisha ujenzi wa
chumba cha chini ya Bahari kwenye hoteli yake iliyopo Makangale Mkoa wa
Kaskazini Pemba huku Waziri wa Habari Mh. Marouk akifurahia kitendo
hicho.
Kitanda
na mandhari halisi na nzuri iliyomo ndani ya chumba cha chini ya Bahari
katika hoteli ya Manta Resort Makangale Kaskazini Pemba mradi
uliozinduliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif.
Sehemu ya choo katika chumba cha chini ya Bahari kilichopo kwenye Hoteli ya Manta Resort huko Makangale Pemba.
Meneja
Mkuu wa Hoteli ya Manta Resort Bwana Methew Saus Maarufu “ Babu kwa
Nini “akitoa maelezo ya hatua zilizochukuliwa kukamilisha ujenzi wa
chumba cha chini ya Bahari katika Hoteli ya Manta Resort iliyoko
Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba.Kushoto
ya Balozi Seif ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi, Waziri wa Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk na Naibu wake Mh.
Bihindi Hamad.
Meneja
Mkuu wa Hoteli ya Manta Resort Bwana Methew Saus akionyesha eneo la juu
la chumba cha chini ya bahari ambapo mgeni atapata fursa ya kupunga
upepo pamoja na kuota jua.
Mandhari nzuri ya Hoteli ya Manta Resort ya Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba eneo ambalo kipo chumba cha chini ya Bahari.
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mradi mpya wa
ujenzi wa Chumba cha chini ya Bahari uliofanywa na Hoteli ya Manta
Resort iliyopo katika Kijiji cha Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba
umeiweka Zanzibar katika ramani mpya ya Dunia katika harakati za
kuimarisha sekta ya Utalii unaobeba nafasi kubwa ya Uchumi katika
Mataifa mengi Ulimwenguni.
Chumba hicho cha
chini ya Bahari kilichopo Makangale ambacho ni cha pekee Barani Afrika
kimeiwezesha Zanzibar kuwa ya tatu kwa kuwa na mradi kama huo Duniani
ikitanguliwa na Nchi za Puerto Riko,Sweden, Kisiwa cha Fiji na
ikifuatiwa na Dubai.
Mradi huo ulioko
katika Matengenezo unatarajiwa kuwa na vyumba takriban 220. Jengo hilo
lenye huduma kamili anazostahiki kuzipata mwanadamu ni pamoja na chumba
cha kulala,huduma za maji safi,Choo, umeme, sehemu ya Mapumziko, na eneo
maalum la juu kwa ajili ya kuotea jua. Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambae ndiye aliyeweka Nanga ya Msingi ya
mradi huo wa Makangale Miezi 12 iliyopita Tarehe 25/12/2012 akakizindua
tena rasmi chumba cha mradi huo kilichoko umbali wa mita Nne chini ya
Bahari.
Uzinduzi huo
uliojumuisha mamia ya Wananchi wa Kijiji cha Makangale pamoja na
majirani zake ulishuhudiwa pia na Viongozi kadhaa wa Serikali, vyama vya
Siasa pamoja na watendaji wa Sekta ya Utalii wakiongozwa na Waziri wa
Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk na Naibu wake
Mh. Bihidndi Hamad.
Akizungumza mara
baada ya kuuzindua Mradi huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif alisema kwamba uwepo wa mradi huo wa chumba cha chini ya Bahari ni
kielelezo muhimu kitakachokuwa kivutio kwa wageni katika harakati za
kukuza utalii hapa Zanzibar.
Balozi Seif
aliupongeza Uongozi wa Hoteli ya Manta Resort ya Makangale kwa kuamua
kuwekeza mradi huo wa kipekee Barani Afrika ambao utaleta maendeleo
makubwa katika Sekta ya Utalii. “ Nimeshuhudia uzuri wa chumba hichi
ambapo yapo mazingira mazuri ya mapumziko na kulala, samaki wa kuvutia.
Natarajia
wakaazi wanaonguuka eneo hilo watashirikiana vyema na uongozi wa Hoteli
hiyo katika kukilinda chumba hicho kinachotarajiwa kuongeza ushawishi
kwa watalii kutembelea Zanzibar “. Alisisitiza Balozi Seif.
Alielezea
matumaini yake kwamba Uongozi wa Hoteli ya Manta Resort Makangale
utaendelea kutoa huduma bora na za uhakika ili kuongeza idadi ya wageni
na watalii kutembelea Pemba. Katika kuunga mkono jitihada hizo za
wawekezaji alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwapa
mashirikiano ya karibu wawekezaji wa sekta hiyo ili waendeshe shughuli
zao kwa ufanisi mkubwa.
“ Sisi Viongozi
wa Serikali akiwemo Mheshimiwa Rais, Makamu wa Kwanza wa Rais na mimi
mwenyewe tunapofanya ziara nje ya nchi hutumia fursa ya kuwabembeleza
wawekezaji kuwa kuwekeza Nchini mwetu hasa katika sekta ya utalii na
Viwanda.
Bahati nzuri
wanatuitikia na wanakuja na ndio maana leo Zanzibar ina vitega uchumi
vingi vya sekta ya utalii na mfano hai ni huu mradi wa chumba cha chini
ya Bahari hapa Makangale “. Alifafanua Balozi Seif.
Alifahamisha
kwamba pamoja na maendeleo ya ujenzi wa miradi ya uwekezaji katika sekta
ya utalii lakini bado Serikali pamoja na Wananchi wanahitaji kuendelea
kuwa na matumaini ya kuongezeka kwa idadi ya watalii hali ambayo
itasaidia kuongeza mapato ya Taifa.
Hata hivyo
Balozi Seif alitahadharisha kwamba watalii na wageni hao hawataingia
nchini iwapo jamii haitojikita katika kuendeleza amani na utulivu ndani
ya maeneo yao hasa sehemu zenye vitega uchumi hivyo.
Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar alisema wananchi hawanabudi kupania kuiweka nchi
katika hali hiyo ya amani na usalama ili wageni hao washawishike kupenda
kuendelea kutembelea Nchini na kuishi bila ya wasi wasi.
“ Tuwe
wanyenyekevu kwa wageni wetu, tuwaonyeshe bashasha za Kizanzibari kama
ilivyo tabia na desturi yetu, tusiwabughudhi wakiwa ufukweni au katika
matembezi yao. Tunataka wafurahie ukaazi wao katika visiwa vyetu vya
karafuu na Viungo “. Alieleza Balozi Seif.
Mapema Meneja
Mkuu wa Hoteli ya Manta Resort Bwana Methew Saus Maarufu “ Babu kwa Nini
“ alisema utafiti wa mradi huo ulifanyika kwa karibu miaka sita ambapo
wataalamu wa kimazingira na mambo ya bahari walilazimika kupima mwenendo
wa maji ya bahari ya eneo hilo ili kuwa na uhaika wa kuanzisha mradi
huo.
Bwana Methew
Saus alisema mazingira ya Kisiwa cha Pemba yamepelekea kuanzishwa kwa
mradi huo wa majaribio wa chumna cha chini ya Bahari uliogharimu zaidi
ya Dola za Kimarekani Laki Tano { U$ 500,000 } sawa na fedha za
Kitanzania Milioni Mia 758,000,000/-.
Meneja huyo wa
Hoteli ya Manta Resort ya Makangale ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar pamoja na Wizara inayosimamia Sekta ya Utalii kwa ushirikiano
iliyompa kuweza kufanikisha mradi huo muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa
Zanzibar.
Akimkaribisha
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Waziri wa Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk alisema mradi huo kwa
kiasi kikubwa umeanza kuitangaza vyema Zanzibar katika sekta ya utalii
wa Daraja la juu duniani.
Waziri Mbarouk
aliwaasa wananchi na hasa wavuvi wanayoizunguuka hoteli hiyo kujiepusha
na uvuvi pembezoni mwa mradi huo jambo ambalo litaondoa sifa na
mazingira halisi ya kuwepo kwa samaki wanaokizunguuka chumba hicho.
Alikemea tabia
iliyoanza kujichomoza ya baadhi ya wavuvi wa maeneo hayo ya kuvua kwa
kutumia nyavu ndogo nje ya chumba hicho kwani inaweza kumvunja moyo
muwekezaji huyo ambae ameshajitolea kusaidia maendeleo ya Vijiji jirani
na Hoteli hiyo.
Mradi wa mwanzo
wa ujenzi wa vyumba vya chini ya Maji Jules Undersea Lodge umeanza
Nchini Puerto Rica mwaka 1970, Utter In Vasteras Sweden Mwaka 2000,
Poseidon Undersea Resort Fiji na Mwengine Crescent Hydropolis unaendelea
kujengwa Nchini Dubai.
0 comments :
Post a Comment