Wakati
Watanzania wakisubiri matokeo ya kidato cha pili mwaka 2013, imebaini
kuwa Serikali imetoa agizo kwamba wanafunzi wote waliofeli mtihani huo
kuendelea na masomo ya kidato cha tatu, huku wakisoma mafunzo ya kurudia
mtihani wa kidato cha pili.Licha ya matokeo hayo kutotangazwa hadi
sasa, imebainika kuwa waliofaulu mtihani huo uliofanywa Oktoba 7 hadi 21
mwaka jana ni asilimia 62 tu, asilimia 31 wakitakiwa kukariri (kurudia)
kidato cha pili mwaka huu, huku asilimia saba wakishindwa mtihani huo
kwa mara ya pili.
Jumla ya wanafunzi 531,457 walitajwa na Wizara ya Elimu mwaka jana kuwa watafanya mtihani huo.
Uamuzi
huo wa Serikali ni tofauti na ule uliotolewa na Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa Novemba 4, mwaka 2012, kwamba
kuanzia wakati huo mtihani wa kidato cha pili utakuwa ni wa mchujo na
kwamba atakayefeli atatimuliwa.
Dk
Kawambwa alisema matokeo ya mtihani wa kidato cha pili yatatumika kama
kigezo cha kuchuja na kukariri kidato cha pili kwa watahiniwa
watakaoshindwa kufikia wastani wa ufaulu wa alama 30.
Alisema
mtahiniwa ataruhusiwa kukariri kidato cha pili mara moja tu na endapo
mtahiniwa atashindwa mtihani kwa mara ya pili kwa mwaka utakaofuatia,
itabidi aendelee na elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi.
Gazeti
hili limeiona barua iliyoandikwa Januari 16 mwaka huu na Wizara ya Elimu
na Mafunzo ya Ufundi na kusainiwa na Katibu Mkuu wake, Profesa Sifuni
Mchome, kwenda kwa wadau wa elimu nchini, wakiwamo maofisa elimu wa
mikoa na Chama cha Wamiliki wa Vyuo na Shule Binafsi (Tamongsco).
Katika
barua hiyo, wizara hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha kuwa wanafunzi
watakaofeli mtihani huo, wanaendelea na masomo ya kidato cha tatu.
"Matokeo
ya kidato cha pili yamepokewa na kufanyiwa uchambuzi ili kupata taswira
ya taifa. Taarifa ya matokeo hayo imebaini kuwa watahiniwa waliofanya
mtihani na kufaulu ni sawa na asilimia 62 tu," inaeleza sehemu ya barua
hiyo na kuongeza;
"Hali hii
inaonyesha kuwa asilimia 31 ya wanafunzi watatakiwa kukariri kidato cha
pili, 2014. Wale walioshindwa kwa mara ya pili ambao ni asilimia saba
wanatakiwa kuendelea na masomo nje ya mfumo rasmi."
Barua
hiyo inaeleza kuwa wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 na
kuendelea waendelee na masomo ya kidato cha tatu mwaka 2014, wakati
awali Serikali ilitoa tamko kuwa watakaoshindwa kufikisha alama 30
watatimuliwa.
"Wanafunzi
waliofaulu kwa wastani wa alama 20 hadi 39 wapewe mafunzo rekebishi
'Remedial class' wakiwa kidato cha tatu," inaeleza sehemu ya barua hiyo.
Inaeleza
kuwa uamuzi huo unawahusu wote wakiwamo wale walioshindwa kwa mara ya
pili, "Kwa maana hiyo hakuna mwanafunzi atakayerudishwa nyumbani."
Mwisho
barua hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha kuwa inawapa taarifa mameneja
na wamiliki wa shule na seminari ili kusimamia utekelezaji wa uamuzi
kuhusu matokeo hayo.
Kauli ya wizara
Akitolea
ufafanuzi suala hilo, Profesa Mchome alisema, "Suala la wizara kuagiza
wanafunzi wote waliofeli kuendelea na masomo ya kidato cha tatu mimi
sijalisikia, ninachojua ni kwamba wapo watakaorudia."
Alisema
kuwa tayari wizara imeshapeleka taarifa za matokeo hayo na uamuzi wa
Serikali katika kila kanda nchini. "Kila shule ina taarifa hizo. Wapo
wanafunzi watakaorudia."
Akizungumza
kuhusu matokeo ya kidato cha pili mwaka 2013 kutotoka mpaka sasa
alisema, "Ninachofahamu ni kwamba matokeo ya kidato cha pili
yameshawasilishwa katika kanda zote nchini."
"Unajua
matokeo ya kidato cha pili siyo kama matokeo ya darasa la saba, kidato
cha nne na sita. Matokeo ya kidato cha pili ni kama mwendelezo wa
tathmini 'Continuous assessment' kwa mwanafunzi, hutumika pia katika
mtihani wa kidato cha nne."
Alisema
ndiyo maana matokeo hayo hupelekwa katika shule husika. "Baada ya
kupelekwa katika shule husika, hapo ndipo inaweza kutolewa taarifa za
matokeo hayo pamoja na ufafanuzi."
Kwa
nyakati tofauti gazeti hili lilimtafuta Dk Kawambwa na Naibu wake,
Phillip Mulugo ili kutolea ufafanuzi suala hilo, lakini simu zao za
mkononi zilikuwa zikiita bila majibu.
Msimamo wa Tamongsco
Alipotafutwa
Katibu Mkuu wa Tamongsco, Benjamin Nkonya kueleza kama wanakubaliana na
agizo hilo la Serikali alisema, "Inaonekana Serikali haiko tayari
kutekeleza mkakati wake wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN)."
"Kama
wizara inalazimisha wanafunzi walio na ufaulu mdogo kuendelea na masomo
katika mfumo wa vidato (formal education), lazima tutegemee kuona
wanafunzi wakifanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne."
Alisema
kuwa asilimia 98 ya wanachama wa chama hicho ni Watanzania wazalendo
kwamba hawapo tayari kutekeleza agizo la Serikali kwa sababu siyo la
kizalendo na limetolewa kwa ajili ya kutimiza malengo ya kisiasa ya
kujiongezea umaarufu wa muda mfupi, huku Watanzania wakiogelea kwenye
dimbwi la umaskini unaotokana na ujinga.
"Wachache
watakaosaliti msimamo huu watakuwa wamekubali kupoteza muda wa vijana
wetu huku wakijua kwamba watafika kidato cha nne, kupata daraja sifuri
na kuishia kuwa machangudoa, wauza dawa za kulevya, bangi, wizi na
vitendo vingine vya uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu," alisema.
Alisema
ili kuwasaidia wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo yao;
"Mwanafunzi ambaye ufaulu wake utakuwa chini ya asilimia 45 aondolewe
katika mfumo wa elimu ya vidato (formal education) na kuingizwa katika
mfumo wa elimu ya ufundi mchundo (TVET - Technical education and
vocational education)."
Alisema
wanachama wa Tamongsco wanamiliki vyuo 586 kati ya vyuo 750 vya ufundi
mchundo (VETA) na wanamiliki vyuo 1975 kati ya vyuo 1988 vya ufundi
stadi (technical institutes) ambavyo vinasimamiwa na Baraza la Taifa la
Elimu ya Ufundi Stadi (NACTE).
"Vyuo
hivi vina uwezo wa kuchukua wanafunzi wote ambao wana ufaulu wa chini ya
asilimia 45 kuwaendeleza hadi chuo kikuu. Kikwazo pekee kilichopo ni
kwa Serikali kukubali kuchangia gharama za uendeshaji wake."
"Kikwazo
hiki kitaondoka endapo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itakubali
kutekeleza sera, sheria na kanuni za ushirikiano kati ya sekta ya umma
na binafsi (PPP) partnership) kama ilivyopitishwa na Bunge mwaka 2010.
Kidato cha pili 2012
Katika
mtihani huo mwaka 2012 wanafunzi 136,923 kati ya 386,271 waliofanya
mtihani huo walifeli. Idadi ya waliofeli ilikuwa sawa na asilimia 35.5,
wakiwamo wasichana 74,020 na wavulana 62,903, waliofaulu walikuwa
wanafunzi 245.9,32.
Chanzo:Mwananchi
0 comments :
Post a Comment