TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa mshtuko
taarifa za tukio la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa
CHADEMA Wilaya ya Temeke, Josephat Yona Patrick.
Chama kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano, mbali
ya kukemea kwa nguvu zote tukio hilo la kihuni na mengine ya namna hiyo
yenye lengo ya ukatili dhidi ya binadamu, katika hatua ya sasa kinapenda
kusema yafuatayo juu ya tukio hilo ovu ;
1. Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi juu ya tukio hilo la
kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Temeke ili ukweli
ujulikane na haki itendeke, kwa sheria kuchukua mkondo wake.
2. Chama kinawataka wanachama na Watanzania kwa ujumla
kutulia, hasa pale ambapo watu wenye hila na malengo yao, wanaanza
kukihusisha chama na tukio hilo. Watambue kuwa pamoja na mtu yeyote kuwa
kiongozi wa chama, bado anayo maisha yake na uhusiano na watu wengine
katika jamii.
3. Jeshi la Polisi linapaswa kuyachukulia uzito mkubwa na
unaostahili matukio ya namna hii ambayo yanaanza kuota mizizi kutokana
na watu waovu wanayoyatekeleza kutochukuliwa hatua za kisheria ambazo
zingesaidia kuzuia yasitokee tena.
4. Watanzania bado wanakumbuka kwamba hadi sasa Jeshi la Polisi
limeshindwa kutoa taarifa za kina na kuchukua hatua za kisheria ambazo
zingesaidia ukweli kujulikana na haki kutendeka katika matukio ya
kutekwa na kuteswa kwa kiongozi wa madaktari Dk. Steven Ulimboka na
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda. Hivyo ingesaidia
kuzuia matukio mengine kutokea.
5. Ni kutokana na jeshi hilo kushindwa kuwajibika ipasavyo
katika matukio mengine ya namna hiyo, watu waovu wanaweza kutumia mwanya
wa kinachoendelea ndani ya CHADEMA kwa chama kuchukua hatua za
kinidhamu dhidi ya wanachama wasio waadilifu, kufanya matukio ya namna
hiyo ili kujenga taswira ya kukihusisha chama na uhuni huo unaobeba kila
sifa ya kuitwa ukatili dhidi ya binadamu.
6. Aidha kushindwa kwa Jeshi la Polisi kuwajibika ipasavyo
katika kufanya uchunguzi wa matukio hayo (yaliyotolewa kama mfano hapo
juu) na mengine ya namna hiyo, jeshi hilo linazidi kujiweka katika
wakati mgumu wa kukwepa tuhuma za baadhi ya watendaji wake kujua na
kushiriki masuala haya, hususan kwa kurejea tukio la kutekwa kwa Dkt.
Ulimboka.
Imetolewa leo Jumanne, Januari 7, 2014 na;
Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
0 comments :
Post a Comment