Godbless Lema akiongozwa na wafuasi wake. |
Wakati
uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata ya Sombetini katika Jiji la Arusha,
ukitarajiwa kufanyika kesho, hali imeanza kuwa tete baada ya Katibu wa
Chama Cha Mapinduzi(CCM) wa Wilaya ya Arusha, Elisante Kimaro na Mbunge
wa jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema kukunjana mashati katika Kituo
Kikuu cha Polisi cha Arusha jana.
Wakati hayo yakifanyika, usiku wa kuamkia jana mashina matatu ya
jumuiya ya vijana wa CCM (UVCCM) yaliyozinduliwa na Mjumbe wa NEC
katika wilaya ya Arusha, God Mwalusamba katika kata ya Sombetini Jijini
Arusha yameng’olewa na bendera zake kuchomwa moto na watu wanaodaiwa
kuwa ni wafuasi wa Chadema.
Akizungumzia tukio la kukunjana mashati, Katibu wa CCM wa wilaya ya
Arusha, Elisante Kimaro alisema Mbunge Lema alitaka kulazimisha kufungua
shina la vijana wa chama chake sehemu ya Sombetini shuleni, mahali
ambapo CCM imezindua siku mbili zilizopita, kitu ambacho vijana wa UVCCM
hawakukikubali.
Kimaro alisema kutokana na kutokuelewana ndipo Mkuu wa Polisi wa
Wilaya ya Arusha, Giles Mroto alipoitwa katika eneo la tukio na
alilazimika kuwataka viongozi wote kwenda katika kituo kikuu cha polisi
kwa mahojiano zaidi.
Alisema walipofika polisi alishangaa kuona Mbunge Lema akiwa mbogo na
kutaka kumpiga kwa kufikia hatua ya kumshika shati lakini na yeye
hakukubali na kuamua kumshika shati na tukio hilo lilitokea mbele ya
mkuu wa polisi wa wilaya ya Arusha.
"Tulikunjana mashati mbele ya OCD Mroto tukiwa kaunta ya polisi kituo
kikuu, na polisi waliamua kutuamulia na kutakiwa kwenda ofisini kwa OCD
kwa majadiliano zaidi,’’alisema.
Katibu huyo alisema, “OCD alitusihi kuacha vurugu kama viongozi na
kuwa mfano bora kwa wafuasi wa vyama vyetu na tuliruhusiwa kuondoka
polisi na kuendelea na kampeni na Lema alizuiliwa kufungua shina mahali
ambapo CCM imefungua na kulizindua”.
Alisema cha kushangaza usiku wa kuamkia jana mashina yote matatu
yaliyozinduliwa na Mwalusamba yameng’olewa na bendera zake kuchomwa
moto, kitu ambacho alidai kimefanywa na Lema na wafuasi wake.
Kimaro aliyataja mashina yaliyong’olewa na bendera zake kuchomwa moto ni pamoja na Godauni, Nguselo na Sombetini shuleni Kona.
Katibu huyo alisema amewaita vijana wa UVCCM na kuwasihi kuacha
kulipiza kisasi kwani Chadema wanataka vurugu na umwagaji damu ili
uchaguzi huo uahirishwe kwani kwa sasa hali yao sio nzuri.
“Tunajua njama zao na sisi kama chama na jumuiya zake tumeamua
kutolipiza kisasi na kuwasihi vijana kuendelea na kampeni zenye
ustaarabu ili kesho upigaji kura uwe na amani bila ya vurugu na tuna
uhakika wa kuwapiga katika kinyang’anyiro hizo,’’alisema Kimaro.
Mwandishi alipomtafuta Lema kupitia simu yake ya mkononi iliita bila
majibu na hadi tunakwenda mitamboni simu hiyo haikupokelewa.
Wakati hayo yakijiri, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema kata ya
Sombetini, Iddy Mdava siku moja kabla ya uchaguzi wa kata hiyo yeye na
kamati nzima ya siasa ya kata hiyo imehamia CCM juzi na kuleta hofu kwa
chama hicho katika uchaguzi wa kesho kama itashinda.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Madava alisema ni kutokana na
baadhi ya viongozi wa juu wa Chadema kulazimisha Ally Bananga kugombea
udiwani katika kata hiyo bila ya kufuata demokrasia.
Madava alisema Banga sio chaguo la Chadema wa kata ya Sombetini bali
ni shinikizo la viongozi wa juu wa Chadema kwa ushawishi wa Lema, kitu
ambacho ni hatari ndani ya chama hicho chenye upendeleo wa hali ya juu.
“Chaguo la wana-Chadema Sombetini ni Gody na mimi Madava na sio
Bananga lakini kwa kuwa demokrasia ndani ya Chadema hakuna
tunalazimishwa kwa nguvu na viongozi wa juu wa chama hicho,” alisema
Madava.
Madava alisema kuna wanachama wengi wa Chadema na viongozi wa kata
wako njiani kukihama chama hicho kutokana na chama hicho kuendeshwa
kibabe na upiundishwaji mkubwa wa demokrasi, kitu ambacho kinawakatisha
tamaa.
Alisema kwa sasa Chadema imekosa mwelekeo na iko siku hayo yote
yatakuwa hadharani kwani baadhi ya wana-Chadema na viongozi wanayaficha
bila ya sababu za msingi wakati hali ni mbaya.
Akizungumzia hilo, Katibu wa CCM wa wilaya ya Arusha, Elisante Kimaro
alisema kuwa chama kimempokea na kinamkabidhi Madava kwa uongozi wa
tawi aliko ili chama kiweze kumchunguza mienendo yake isije ikawa
Chadema imeleta pandikizi.
Kimaro alisema kamati ya siasa ya tawi ndio wenye jukumu la kujua
kama kweli amerudi kwa dhati ama kwa kutaka kuchunguza na baada ya
kujiridhisha chama kitampokea rasmi kwa mkutano mkubwa na kumkaribisha
rasmi CCM kwa mikono miwili.
Uchaguzi wa Kata ya Sombetini unatarajia kufanyika kesho na mchuano
mkali uko kwa wagombea watatu wa vyama vya CCM, Chadema na CUF.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas amewataka
viongozi wa vyama vyote na wafuasi wao kuwa watulivu katika muda huu wa
dakika za mwisho na siku ya upigaji kura na yeyote atayedhubutu kuleta
vurugu polisi haitasita kumchukulia hatua.
“Hatutaangalia mtu katika vurugu kwani yeyote mwenye kuleta vurugu
dola iko na itamchukulia hatua bila ya woga kwani hakuna mtu yuko juu ya
sheria na polisi hailifumbii macho hilo,’’ alisema.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji
Damian Lubuva amesema kuwa hali ya kisiasa Jijini Arusha na kata 26
nchini zinazotarajia kufanya uchaguzi kesho ni safi kwani vyombo vya
dola vimejipanga kuhakikisha wananchi wa kata zote wanapiga kura na
kutimiza wajibu wao.
Aidha amesema kuwa serikali imetoa Sh bilioni 279 kwa ajili ya
uboreshwaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura na hivi sasa hatua za
awali zinaendelea kufanyika kwa kupitia vituo vya kupigia kura ili
visogezwe maeneo jirani na mahali wanapoishi wananchi.
Jaji Lubuva aliyasema hayo jana Jijini hapa wakati akizungumza na
waandishi wa habari pamoja na viongozi mbalimbali vya vyama vya siasa
juu ya hatua mbalimbali za Tume walizoziona katika chaguzi za udiwani
zinazotarajia kufanyika nchi nzima kesho.
Alisema ingawa kasoro za hapa na pale zilijitokeza wakati wa kampeni
za kila vyama lakini anaamini polisi waliweza kuzishughulikia pamoja na
wasimamizi wa Tume ya Maadili lakini malalamiko mengi ya tume ya
maadili waliyokuwa wakiyapata ni kutoka vyama viwili vya upinzani yaani
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
ambapo kulikuwa na majibizano ya hapa na pale.
"Tume haijafurahishwa na matokeo ya vurugu wakati wa kampeni za
udiwani yaliyotokea katika kata mbalimbali za uchaguzi, lakini nasema ni
vyema wahusika wa vyama vya siasa kunadi sera na si kupigana lakini na
hao waliofanya vurugu polisi wakidhibitisha watachukuliwa hatua za
kisheria pia daftari la wapigakura litaboreshwa kwani serikali imeshatoa
fedha kwa ajili ya kuboresha daftari hilo na hivi sasa kazi imeanza,
jitokezeni wananchi mkapige kura''.
Alisema vituo vipo zaidi ya 62 vya kupigia kura huku wasimamizi wa
uchaguzi wakiwa 86 ikiwemo wasimamizi wa vituo 62, wasimamizi wasaidizi
62, makarani waongozaji 62 ,wasimamizi wa akiba 4 na kutoa rai kwa
wananchi kujitokeza kupiga kura siku hiyo
0 comments :
Post a Comment