Mkuu wa wilaya ya Mkalama mkoa wa Singida, Edward Ole Lenga, akizungumza kwenye hafla ya utundikaji mizinga ya nyuki kimkoa zilizofanyika katika kijiji cha Nkungi wilayani Mkalama.Wa pili kulia walioketi ni Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone na (wa kwanza kulia) ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama, James. Kushoto (aliyekaa) ni Katibu tawala mkoa wa Singida Liana Hassan.
Na Nathaniel Limu, Singida
KAIMU mkuu wa wilaya ya Singida, Edward Ole Lenga, amewataka wakazi wa wilaya hiyo wahakikishe wanahifadhi na kutunza vizuri chakula cha kutosha mwaka mzima,ili kujikinga na balaa la njaa linatishia msimu huu kutokana na mvua chache mno kunyesha.
Lenga ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Mkalama,ametoa wito huo muda mfupi kabla hajamkaribisha mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone, kuhutubia mamia ya wakazi wa tarafa ya Mgori jimbo la Singida kaskazini kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya kitaifa ya utundikaji wa mizinga ya nyuki ambapo kimkoa yalifayika katika kijiji cha Pohama.
Alisema mvua za msimu huu zimenyesha kwa kipindi kifupi mno na kukatika mapema,kitendo kinachosababisha karibu mimea yote ikiwemo ya mazao ya chakula kukauka kabla haijakomaa.
“Siku zote mkuu wetu wa mkoa Dk.Kone amekuwa akiwahimiza wakulima kulima mazao yaliyopewa kipau mbele na mkoa ambayo baadhi ni uwele,mtama na jamii ya Kunde. Mazao haya na mengine yaliyopewa kipaumbele kwa vile yanastahimili hali ya hewa katika mkoa wetu ambao ni ya ukame unaosababishwa na mvua haba. Endapo msimu huu kutakuwa na mkulima aliyelima Mahindi na zao lo lole ambalo halipo kwenye vipaumbele vya mkoa, itakuwa imekula kwake”,alifafanua.
Alisema kwa kifupi,msimu huu sio mzuri kwa upande wa kilimo kutokana na mvua kukatika mapema na hivyo ametumia nafasi hiyo kuwatahadharisha i wananchi wafanye juhudi mapema ya kuhakikisha wanakuwa na chakula cha kukidhi mahitaji.
Aidha,Lenga ametumia fursa hiyo pia kuwahimiza wafugaji wa mifugo kuuza baadhi mapema,ili waweze kununua chakula/nafaka kitakachokidhi mahitaji ya mwaka mzima.
Akifafanua zaidi,alisema “ukame wa mwaka huu, umesababisha pia kuwepo kwa uhaba mkubwa wa malisho ya mifugo na maji pia. Hali hii inaweza kusababisha mifugo kukonda na hivyo baadae itakosakabisa soko zuri au isiuzike kabisa, kwa hiyo njia pekee ya kukabiliana na balaa la nja msimu huuo,ni kununua chakula mapema”.
Kaimu Mkuu huyo wa wilaya,alisema kwa hali hiyo,upo umuhimu mkubwa baadhi ya mifugo ikauzwa mapema,ili michache itakayobaki ipate angalau malisho ya kutosheleza.
Kwa upande wake mkulima wa kijiji cha Pohama alikozaliwa waziri wa maliasili na utalii Lazaro Nyalandu, John Kipandwa,alisema kuwa ukame wa msimu huu ni mkali mno na kwa vyo vyote wananchi na mifugo yao wataathirika vibaya, hasa kuanzia miezi ya mwisho mwaka huu na mwanzoni mwakani.
“Wafugaji wengi huku kwetu na majirani zetu wameisha baini kuwepo kwa upungufu wa malisho na maji kwa matumizi ya binadamu na mifugo yao, na tayari wameisha anza hatua ya kuuza baadhi”,alisema Kipandwa.
Source: DewjiBlog
0 comments :
Post a Comment