Dar es Salaam. Sakata la Yanga kugomea udhamini wa Azam Tv
limechukua sura mpya baada ya klabu hiyo kutaka kupewa kitita cha Sh600
milioni ili kukubali kudhaminiwa na Azam.
Habari za uhakika ambazo Mwananchi limezipata zinadai kuwa, Yanga
wamepata kiburi cha kugomea udhamini wa Azam baada ya kuwa na ofa mbili
mkononi ya Pepsi na ile ya Zuku.
“Pepsi wanatoa kinywaji chao kipya Pepsi Cola na wametupa ofa ya Sh600
milioni, Azam walifuatwa na kuelezwa juu ya ofa hiyo wakakataa Pepsi
wasiingie kwa vile ni wapinzani wao kwa Azam Cola,” kilisema chanzo cha
habari.
Chanzo hicho kilisema kuwa, Yanga waliwapa sharti Azam la kuongeza dau
kutoka Sh100 milioni na kama isingewezekana basi waingie mkataba na
Kampuni ya Pepsi.
“Hiki ni kinywaji cha Pepsi ni kipya na wanataka kukitangaza kupitia
Yanga, Zuku nao wametupa ofa ya Sh400 milioni, kilichopo hapa ni
mgongano wa kimasilahi,” kiliongeza chanzo hicho.
Inadaiwa kuwa, Azam wameingia kwenye ligi kwa sababu wanataka kuuza
ving’amuzi vyao, lakini dau walilotoa la Sh100 ni dogo ingawa klabu
nyingine ikiwemo Simba wamekubali.
Hata hivyo, Yanga kila kukicha imekuwa ikija na madai tofauti na tayari
wameshaweka msimamo wao ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wanachama wao
kupinga suala la udhamini wa Azam.
Klabu hiyo ya mtaa wa Jangwani imekuwa kila kukicha ikitoa madai mapya
ya kusisitiza kugomea udhamini huo wa Azam na mapema wiki hii walisema
wanagomea kwa vile kuna kipengele cha CD za mchezo ambazo Azam ndiyo
watazimiliki na kwamba wasingekuwa na shida na mkataba wa Azam kama
kampuni hiyo isingekuwa na timu kwani kitendo cha kumiliki CD kuna
uwezekano wa kuididimiza timu yao.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia akizungumzia
suala hilo alisema madai hayo ya Yanga hayana mashiko kwani klabu zote
zinapewa CD za kila mchezo, pia suala la TBL Yanga siyo peke yao ambao
wanadhaminiwa na TBL, kwani hata Simba nao ni wadhamini wao na
wamekubaliana na mkataba huo wa Azam.

0 comments :
Post a Comment