SIMBA imeondoka jana Jumatatu kwenda Tanga kuikabili Coastal Union kesho Jumatano lakini imechomoka kwa basi ikiwa na wachezaji 22 tayari kwa mchezo huo ikiwaacha Haorun Chanongo, Abdulhalim Humoud, Betram Mwombeki, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ na Henry Joseph.
Wekundu hao wataivaa Coastal Union ambayo jana
Jumatatu ilitangaza kumtema kocha wake, Hemed Moroco na kumpa timu,
Joseph Lazaro.
Habari ambazo Mwanaspoti imepata zinasema kuwa
Humoud na Chanongo wameachwa kutokana na kucheza chini ya kiwango katika
mchezo dhidi ya Yanga juzi Jumapili na timu hizo kutoka sare ya mabao
3-3.
Wachezaji hao walitolewa kipindi cha pili na
nafasi zao kuchukuliwa na William Lucian na Said Ndemla waliobadilisha
mchezo na kuifanya timu yao iliyokuwa nyuma kwa mabao matatu kusawazisha
yote na matokeo kuwa sare.
Hata hivyo baada ya mchezo huo Kocha Abdallah
Kibadeni alilalamikia hujuma na kudai kuna baadhi ya wachezaji
walitumiwa na baadhi ya watu walioivamia kambi ya timu hiyo ili wacheze
chini ya kiwango.
“Kuna watu walikuja kambini na kuwapandikiza
maneno wachezaji, na waliopandikizwa maneno hawakucheza vile
inavyopaswa kipindi cha kwanza na wakaruhusu mabao matatu ya haraka,
siwezi kuwataja kwa majina watajijua na kujichuja wenyewe, yule Humoud
nilimpanga makusudi kama mlivyoona ndio maana nikamtoa,” alisema
Kibadeni.
Wachezaji wengine kama Mwombeki hajaungana na
wenzake safarini kwa sababu ana kadi tatu za njano zinazomzuia kucheza
mchezo huo wakati Henry Joseph bado anaendelea kutumikia adhabu baada ya
kutofautiana na kocha na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ amepelekwa timu B.
0 comments :
Post a Comment