KIPA mpya wa Yanga, Juma Kaseja, ameandika rekodi nyingi na tofauti akiwa na klabu yake ya zamani ya Simba kwenye Ligi Kuu Bara na sasa Kelvin Mhagama amemuonya Ally Mustapha ‘Barthez’ wa Jangwani.
Rekodi ya kwanza ya Kaseja ni kuipa Simba taji la
ubingwa wa Ligi Kuu bila ya kupoteza mchezo hata mmoja. Hiyo ilikuwa
msimu wa 2011/12.
Pia ana rekodi ya kucheza dakika 2,340 ambazo ni
sawa na michezo 26 ya ligi nzima ya Bongo bila kufanyiwa mabadiliko na
kocha wake wala kuwa kwenye adhabu ya kadi au kuumia na kukosa mchezo.
Achilia mbali rekodi hizo, msimu huo huo wa
2011/12, Kaseja akiwa na Simba alidaka dakika zote 1,170 ambazo ni sawa
na mechi 13 za mzunguko wa kwanza wa ligi bila kufanyiwa mabadiliko.
Utafiti uliofanywa na Mwanaspoti baada ya mzunguko
wa kwanza wa Ligi Kuu kumalizika na kuzungumza na mabenchi ya ufundi ya
timu 14 zinazoshiriki Ligi Kuu hakuna kipa ambaye ameweza kufikia
rekodi hiyo mpaka sasa.
Kipa wa Coastal Union ya Tanga, Shabaan Kado,
alijaribu na kutaka kumfikia Kaseja lakini ghafla alijikuta akiteleza na
kuishia njiani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kado alisema:
“Nimecheza mechi zote 13 kwenye ligi ingawa kuna moja nilishindwa
kuimaliza kutokana na kuumia, nilidaka kwa dakika 45 za kwanza lakini
nikashindwa kuendelea hivyo Rubawa (Said) alichukua nafasi yangu.”
Katika hatua nyingine, kipa wa zamani wa Simba,
Kelvin Mhagama, amesema kama angekuwa yeye ndiye ‘Barthez’ angeondoka
Yanga na kurudi Simba wala asingeremba kwa vile uwezekano wa kipa huyo
kucheza kikosi cha kwanza Yanga kuanzia sasa ni finyu.
Kipa huyo mkongwe alisema ukitaka kuona uhondo wa
makipa hao ni lazima Barthez arudi zake Simba na ndio upinzani wao
utaonekana kwa kuwa yeye anaamini uwezo wao upo sawa.
Akizungumza na Mwanaspoti mjini Dodoma, Mhagama
alisema ujio wa Juma Kaseja ndani ya Yanga ni kama kikosi hicho kukosa
imani na Barthez hasa baada ya sare mabao 3-3 na Simba, hivyo nafasi
yake ndani ya timu hiyo ni ndogo.
Mhagama alisema hakuamini kama Kaseja anaweza
kusajiliwa Yanga kwa kuwa aliamini uwezo wa Barthez na Dida ndani ya
kikosi hicho ni mkubwa hivyo kutohitajika kipa mwingine zaidi ya hao.
“Uwezo wao hasa Kaseja na Barthez unafanana, Yanga
wamekosa imani na Barthez, kwa uzoefu wangu namsihi dogo afungashe
virago vyake kama vipi arudi zake Simba pale atapata nafasi maana hamna
kipa, huyo Dhaira (Abel) ni bure tu najua watampokea tu, lakini akibaki
Yanga atasugua benchi tu,”alisema Mhagama ambaye naye aliwahi kucheza
Simba akiwa na Kaseja, lakini akashindwa vita ya kuwania namba kikosi
cha kwanza.
CHANZO:MWANASPOTI
CHANZO:MWANASPOTI
0 comments :
Post a Comment