Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa mradi wa reli wa kuanzia Mombasa hadi Kigali, Rwanda, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema mradi wa ujenzi huo pia utaijumuisha Tanzania.
Umoja wa Walio Tayari unaundwa na Kenya, Rwanda na Uganda ambazo pia ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Katika siku za karibuni, nchi hizo zimekuwa zikilaumiwa kwa kuzitenga nchi nyingine wanachama wa EAC za Tanzania na Burundi.
Akizungumzia madai hayo, Rais Kenyatta alisema nchi zinazounda Umoja wa Walio Tayari hazikuwa na mpango wa kuitenga Tanzania.
Hatua hiyo inakuja huku wakuu wa nchi tano za EAC wakitarajiwa kukutana kesho huko Kampala, Uganda.
Rais Kenyatta alisema reli hiyo inayotoka Mombasa, Kampala hadi Kigali itakuwa na tawi la kupitia Voi hadi Taveta kabla ya kuingia Tanzania ikianzia Moshi hadi Arusha.
Alisema reli hiyo inajengwa ili kurahisisha usafirishwaji wa mizigo kutoka bandari ya Mombasa kwenda katika nchi za jirani.
Alisema ujenzi wa reli hiyo haukufanywa nje ya jumuiya na nchi hizo tatu, bali ulipitia katika kamati ya EAC kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
Akilihutubia Bunge mjini Dodoma Novemba 7, mwaka huu, Rais Kikwete alisema mradi huo wa reli haumo EAC na hawakuwa na tatizo nao ila alishangazwa na kutengwa kwenye mpango wa awali wa nchi hizo akiamini Tanzania ni mshirika muhimu wa kibiashara katika eneo hili.
Pamoja na hayo, Rais Kenyatta alisema Tanzania itahusishwa pia katika mradi wa ujenzi wa barabara.
“Mwezi ujao tutakuwa kule Voi kuzindua barabara itakaokwenda Taveta na kutuunganisha na majirani zetu Tanzania, pia tunataka turekebishe hii barabara ya Lungalunga ya kupitia mpaka wa Horohoro ili ituunganishe na majirani zetu wa Tanzania sasa jamani wale ambao wanasema tunavunja.... tunavunja nini wakati sisi tunaunganisha,” alisema Rais Kenyatta.
Hata hivyo, Rais Kenyatta alisema Umoja wa Walio Tayari hauwezi kuvunja EAC kwa kuwa nchi zote ziko pamoja katika kutekeleza majukumu ya jumuiya hiyo.
Alisema wanaodai kuwa umoja huo unaleta matatizo hawajui wanachokisema kwa kuwa hakuna nchi yoyote inayoachwa nyuma katika mambo hayo muhimu.
Marais Kenyatta, Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wamefanya vikao vitatu kujadili ushirikiano miongoni mwa nchi zao.
Viongozi hao wamefanya mikutano mitatu mwaka huu, Juni 24-25 Mjini Entebbe, Uganda; Agosti 28 Mjini Mombasa, Kenya na Oktoba 28, Mjini Kigali, Rwanda.
Katika vikao hivyo, iliamuliwa kuwa nchi hizo zishirikiane katika kuboresha miundombinu, uanzishwaji wa himaya moja ya ushuru wa forodha, uhamiaji na kuundwa kwa shirikisho kisiasa.
0 comments :
Post a Comment