Dar es Salaam. Kocha
mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni amewashangaa wanaomtupia lawama sasa
wakati jukumu lake lilikuwa kutegeneza kikosi bora cha msimu ujao.
Kauli hiyo ya Kibadeni imekuja baada ya
hivi karibuni baadhi ya viongozi na mashabiki kumshutumu yeye na benchi
lake la ufundi kufuatia timu hiyo kunyukwa na Azam 2-1 na kutoka sare
1-1 na Kagera Sugar na kushuka hadi nafasi ya nne katika msimamo.
Matokeo hayo yamesababisha baadhi ya
viongozi wa ngazi ya juu ya klabu hiyo, hivi karibuni kuanza mazungumzo
na kocha wa Gor Mahia ya Kenya, Bobby Wiliamson kuja kuchukua jukumu
lake.
Akizungumza na gazeti hili jana Kibadeni
alisema, “wote wanaolitupia lawama wanapaswa kukumbuka malengo na
mikakati niliyotoa wakati nachukua jukumu hili mbele ya viongozi wote
wakiwamo viongozi wa matawi.
“Mikakati yangu ilikuwa ni kutengeneza
kikosi kwa ajili ya Ligi Kuu msimu ujao, lakini pamoja na yote hayo
namshukuru Mungu, pia tumeweza kufanya vizuri katika mechi za mzunguko
huu ambapo hadi sasa tupo katika nafasi nzuri ya kuwania ubingwa.
“Wale wote wanaotushutumu kuwa
tumeshindwa kazi wanapaswa kulitambua hilo, mikakati na malengo yetu
yanalenga ubingwa msimu ujao, pia tunataka mafanikio msimu huu,” alisema
Kibadeni ambaye alitua Simba akitokea Kagera Sugar.
Simba wavunja viti 195
Thathimini iliyofanywa na Serikali
imeonyesha mashabiki wanaodhaniwa wa Simba waling’o viti 195 kwenye
Uwanja wa Taifa wakati wa vurugu zilizotokea wakati timu hiyo
ilipolazimishwa sare 1-1na Kagera Sugar uwanjani hapo wiki iliyopita.
Vurugu hizo zilisababisha askari kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki waliyohudhuria uwanjani hapo.
Habari za ndani kutoka kwa mmoja wa
viongozi wa Serikali ambaye hakupenda kuandikwa gazetini zinaeleza kuwa
ukarabati wa kiti kimoja uwanjani hapo unagharimu dola 100 (sawa Sh 160,
000) hivyo hadi kukamilika ukarabati wa viti 195 vilivyong’olewa
itagharimu dola 19,500 sawa na zaidi ya (Sh 31. 2 milioni).
Kaimu katibu mkuu wa TFF, Boniface
Wambura alisema tayari Bodi ya Ligi (TPL) imeanza kushughulikia suala
hilo sambamba na kupitia ripoti ya mechi hiyo kwani wao ndiyo wanahusika
na ligi na itakapokuwa tayari hatua zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
_Mwananchi

0 comments :
Post a Comment