BEKI kitasa wa Simba, Donald Musoti (32) ametua jijini Dar es Salaam jana Jumatatu mchana na kutamka kuwa ana kila aina ya mbinu za kupambana na mshambuliaji mpya wa Yanga, Emmanuel Okwi, raia wa Uganda.
Musoti amesajiliwa na Simba akitokea Gor Mahia ya
Kenya kwa mkataba wa miaka miwili sambamba na kipa, Ivo Mapunda, ambaye
pia anatoka Gor Mahia.
Beki huyo mrefu mwenye nguvu anasifika kwa akili
ya mpira na kujiamini na alikuwa nguzo ya ukuta wa Gor Mahia mbele ya
Mapunda ambaye kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsem ametamka kwamba ndiye
kipa bora nchini kwa sasa.
Alitua Dar es Salaam na ndege ya Shirika la Kenya
na kupata mkosi wa mabegi yake kusahaulika jijini Nairobi. Kutokana na
tatizo hilo, Musoti ambaye alitakiwa kuunganisha ndege kwenda kuwafuata
wenzake Zanzibar kuanza mazoezi, amelazimika kubaki Dar es Salaam hadi
leo Jumanne atakapopata mabegi yake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Musoti alisema:
“Nimekuja Simba kwa lengo la kuisaidia na kubwa ni kwamba wasubiri mambo
yangu uwanjani.”
Kuhusu Okwi, alisema: “Namfahamu Okwi vizuri sana,
si ni yule jamaa wa Uganda au kuna mwingine? Okwi ni mchezaji mzuri
lakini kwa upande wangu niko vizuri na nimejiandaa, nitapambana naye na
ndiyo maana nimesajili Simba.”
Musoti ana kazi ya kuhakikisha anaondoa machungu
ya mashabiki wa Simba ambao walikuwa hawana imani na safu yao ya beki ya
kati na hasa sasa baada ya Okwi kusaini Yanga.
Musoti alienda mbali na kuwaambia mashabiki wa
Simba akisema: “Ninachowaomba wanipe muda tu na ushirikiano ili
ninayoyategemea yakamilike. Kama unavyojua, mimi ni mgeni na nimefika
kwenye timu kuna wenyeji nitakutana nao ambao nahitaji kuwafahamu namna
tutakavyojipanga ili mambo yaende vizuri.”
Hata hivyo, Musoti ni mara ya kwanza kucheza nje
ya Kenya lakini anaamini hilo si tatizo na yuko tayari kukabiliana na
changamoto za aina yote.
Akizungumzia jezi atakayoivaa kwa kipindi
atakapokuwa Simba, Musoti ambaye alipokuwa na Gor Mahia alikuwa akivaa
jezi namba nne, alisema: “Niko tayari kuvaa jezi yoyote nitakayopewa,
ingawa binafsi napenda namba isiyozidi 16.”
0 comments :
Post a Comment