FAMILIA ya beki wa zamani wa Simba, David Naftal, imemchimba mkwara beki huyo kuwa kama atarudi nchini na kuzichezea timu za Simba na Yanga itampa laana.
Beki huyo amebakiza mkataba wa miezi sita na timu
ya Bandari FC ya Mombasa, Kenya, aliliambia Mwanaspoti kuwa anaangalia
soka la nje zaidi na kati ya Februari au Machi mwakani atakwenda kufanya
majaribio na moja ya timu ya Afrika Kusini.
Alisema kuwa mpango huo umefanywa na wakala wake Hussein Catesh ‘Amigo’ ambaye anaishi mjini huko ingawa ni raia wa Qatar.
“Mkataba wangu bado kidogo kumalizika, kuna baadhi
ya timu hapa Tanzania zilikuwa zinanihitaji lakini kiukweli siwezi
kurudi nyuma naangalia soka la kulipwa zaidi hata familia yangu
imenikataza na kunitamkia kabisa kuwa nikicheza timu za hapa nitapewa
laana hasa Simba na Yanga.”
“Familia yangu ndiyo kila kitu kwani huwa pamoja
kwa shida na raha, kilichowachukiza ni tabia ya timu za Tanzania kupenda
kuwatumia wachezaji na si kuwasaidia kwa maisha yao ya kisoka hasa
tunapokuwa na matatizo, nakwenda Afrika Kusini kufanya majaribio,”
alisema Naftal.
Beki huyo ambaye amewahi kuzichezea Simba na Yanga
kwa nyakati tofauti pia ameichezea Bandari FC ambayo imemaliza ligi
ikiwa nafasi ya sita, amesema hata kama hatafanikiwa kwenye majaribio
yake basi atatafuta timu nyingine nchini Kenya.
“Naamini nitapita kwenye majaribio hayo ambayo
nilitakiwa kwenda hata mwezi huu, kutokana na mwingiliano wa mambo
nilishindwa,” alisema.
0 comments :
Post a Comment