Saturday, 28 December 2013

Beki wa Simba aachiwa laana

 
FAMILIA ya beki wa zamani wa Simba, David Naftal, imemchimba mkwara beki huyo kuwa kama atarudi nchini na kuzichezea timu za Simba na Yanga itampa laana.
Beki huyo amebakiza mkataba wa miezi sita na timu ya Bandari FC ya Mombasa, Kenya, aliliambia Mwanaspoti kuwa anaangalia soka la nje zaidi na kati ya Februari au Machi mwakani atakwenda kufanya majaribio na moja ya timu ya Afrika Kusini.
Alisema kuwa mpango huo umefanywa na wakala wake Hussein Catesh ‘Amigo’ ambaye anaishi mjini huko ingawa ni raia wa Qatar.
“Mkataba wangu bado kidogo kumalizika, kuna baadhi ya timu hapa Tanzania zilikuwa zinanihitaji lakini kiukweli siwezi kurudi nyuma naangalia soka la kulipwa zaidi hata familia yangu imenikataza na kunitamkia kabisa kuwa nikicheza timu za hapa nitapewa laana hasa Simba na Yanga.”
“Familia yangu ndiyo kila kitu kwani huwa pamoja kwa shida na raha, kilichowachukiza ni tabia ya timu za Tanzania kupenda kuwatumia wachezaji na si kuwasaidia kwa maisha yao ya kisoka hasa tunapokuwa na matatizo, nakwenda Afrika Kusini kufanya majaribio,” alisema Naftal.
Beki huyo ambaye amewahi kuzichezea Simba na Yanga kwa nyakati tofauti pia ameichezea Bandari FC ambayo imemaliza ligi ikiwa nafasi ya sita, amesema hata kama hatafanikiwa kwenye majaribio yake basi atatafuta timu nyingine nchini Kenya.
“Naamini nitapita kwenye majaribio hayo ambayo nilitakiwa kwenda hata mwezi huu, kutokana na mwingiliano wa mambo nilishindwa,” alisema.

No comments:

Post a Comment