Wachezaji wa Yanga wakifanya mazoezi kujiandaa na Ligi Kuu Bara kwenye
Uwanja wa Bora Kijitonyama jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.Picha
na Mpiga picha wetu
NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesema kwa mazoezi ya wiki mbili waliyofanya chini ya kocha Ernest Brandts ana uhakika kikosi chao kipo tayari kupambana na Simba Desemba 21 mwaka huu.
Simba na Yanga zinatarajiwa kupambana siku nne
kabla ya sikukuu ya Krismasi katika mchezo wa Nani Mtani Jembe
ulioandaliwa na wadhamini wao Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na
kusimamiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Cannavaro aliliambia Mwanaspoti kuwa hadi sasa
kikosi chao kipo tayari kwa pambano hilo licha ya baadhi ya wachezaji
kuwa katika kikosi cha Kilimanjaro Stars.
“Tunafanya mazoezi mazuri na kocha wetu, tunafanya
mazoezi uwanjani, ufukweni na gym, lengo ni kuwa na stamina ya kutosha
kuweza kuwahimili wapinzani wetu. Najua tunacheza na Simba siku chache
zijazo, sisi tupo fiti sasa kwani tuliwatangulia wiki moja ya mazoezi,”
alisema Cannavaro ambaye ni nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya
Zanzibar.
Nahodha huyo anayecheza nafasi ya beki wa kati,
alisema ana imani kila mchezaji wa Yanga aliyeshiriki kikamilifu mazoezi
ya timu hiyo yupo tayari kupambana na timu yoyote watakayokutana nayo
kuanzia sasa.
Yanga inaendelea na mazoezi yake ya kila siku
asubuhi kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama jijini Dar es Salaam na
wakati mwingine huwa wanaenda gym au ufukweni kwa lengo la kuboresha
stamina na pumzi kwa wachezaji wake.
0 comments :
Post a Comment