Timu hiyo ya Kilimanjaro Stars itacheza saa 7:30 mchana kwenye uwanja huo ambao katika mchezo wa kwanza ilicheza hapo na kutoka sare ya bao 1-1 na Zambia, ambayo itacheza na Sudan nusu fainali ya pili mjini Mombasa.
Katika uwanja ambao Stars itachezea kuna huduma za
kifahari vyumbani kama runinga za kisasa zilizounganishwa na digitali,
vinywaji laini vya kila aina, chai na maji ya moto ya kuoga jambo ambalo
linaufanya uwe tofauti na viwanja vingine vya Afrika Mashariki na Kati
ingawa bado nyasi haziridhishi hasa mvua inaponyesha.
Kocha wa Stars, Kim Poulsen amesisitiza kwamba
katika mchezo huo watashambulia kama walivyofanya dhidi ya Uganda mjini
Mombasa mwishoni mwa wiki.
Kim alisema: “Ni mchezo mgumu sana ulioko mbele
yetu lakini naamini kwamba tupo tayari kushinda katika mazingira yoyote
yale, nina kikosi imara ambacho kimeimarika kimchezo, nina imani
tutavuka.”
“Hakutakuwa na mabadiliko makubwa sana kikosini
kwa vile tuna wachezaji wengi ambao wako tayari kwa mchezo,lengo sasa ni
kucheza fainali na ninaamini huo uwezo upo tuna mastraika wazuri,
mabeki na viungo.
“Tutacheza mchezo kwa staili tofauti zaidi,
tunajua Kenya itakuwa na faida ya uenyeji kuanzia mashabiki na kila kitu
lakini haitatusumbua, tutafanya kazi yetu uwanjani,”alisisitiza Poulsen
ambaye asilimia kubwa ya kikosi chake wachezaji wake wamefanya vizuri
kwenye ligi zao.
Habari za ndani zinadai kwamba Kenya ilifanya
mpango wa kuhamisha mchezo huo kutoka Mombasa hadi Machakos kutokana na
hali ya hewa.
Mombasa ni joto, hali ambayo Tanzania wameizoea
lakini Kenya inawapa taabu kutokana na wachezaji wake kuzoea baridi ya
jijini Nairobi. Kocha Adel Amrouche alisema; “Tanzania ni ngumu ina
mastraika wazuri, tunajua inaingia ikiwa na morali ya kumtoa bingwa
mtetezi, lakini sisi tutacheza soka yetu na ninaamini Kenya kiufundi ipo
sawa tayari kwa fainali za Alhamisi.”
Kenya itakuwa ikiwategemea mastraika wake Allan
Wanga na Jacob Kelli huku Stars ikiwa na ukuta imara wa Kelvin Yondani
na Said Morad huku langoni akizuia Ivo Mapunda.
Kiungo cha Stars huenda akasimama Athuman Iddi
‘Chuji’ na Frank Domayo ambao watakuwa wakitengeneza mipira kwa
wachezaji wa pembeni Amri Kiemba na Mrisho Ngassa.
Stars imeonyesha mabadiliko makubwa kiuchezaji
haswa baada ya kuingia kwa Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu ambao
wameonyesha kujiamini na wanacheza soka la kufundishwa jambo ambalo
limewafanya wawe gumzo zaidi.
0 comments :
Post a Comment