*Vyama vya michezo mingine vipewe msaada na umuhimu kama wa soka
Inasikitisha sana kwamba Watanzania
tumeipa kisogo michezo mingine isiyo soka kwa sababu za kibiashara.
Hakuna ubishi soka inalipa kutokana na kupendwa na watu wengi lakini
kihabari, unapoandika au kutangaza soka na kupata manufaa kiuchumi,nini
kinakuzuia kutumia nafasi iliyobaki au muda uliobaki kuandika au
kutangaza kuhusu michezo mingine?
Lawama hii haipaswi kuwa dhidi ya
vyombo vya habari vya Tanzania bali dhidi ya wadau wenyewe wa michezo
mingine isiyo soka. Hapa leo nitakupa mfano wa michezo miwili tu;
netiboli (mpira wa pete) na basketiboli (mpira wa kikapu).
Wakati wa karinyekarinye za
mchakato wa uchaguzi wa TFF, watu wa soka wa nchi ya Tanzania
walitengeneza habari kubwa kubwa kila siku kuhusu uchukuaji na
urudishaji fomu, kuwekwa mapingamizi, uamuzi wa mapingamizi, rufani za
mapingamizi na habari nyingine kemkem. Sasa hivi mtu akikuuliza suala la
uchaguzi wa Chama cha Netiboli nchini (CHANETA) limefikia wapi, huna
jibu kwa sababu CHANETA wenyewe hawana juhudi zozote za kulikupandisha
juu suala hilo kihabari.
Mashabiki wa mpira wa wavu wakiwa katika uwanja wa YMCA Dar
Kama mapingamizi kwenye mchakato
wa uchaguzi wa TFF yalivyokuwa habari kubwa, ndivyo kusuasua kwa wadau
wa mchezo wa netiboli kuchukua fomu za kugombea uenyekiti, umakamu
Mwenyekiti na Uweka Hazina kulivyopaswa kuwa habari kubwa ya mchakato wa
uchaguzi wa CHANETA. Hii ya CHANETA haikuwa hivyo kabisa.
Ni habari kubwa mno timu yetu ya
soka ya Taifa (Taifa Stars) kuifunga Morocco 3-1 hapa nyumbani lakini
kwa mshangao si habari kabisa kwa timu yetu ya taifa ya netiboli
iliyoshiriki mwezi Desemba 2012 mashindano ya mataifa sita
yanayojulikana kama “Netball Nations Cup” huko Singapore ikipambana na
wenyeji Singapore, Malaysia, Sri Lanka, Jamhuri ya Ireland na Namibia
kubeba kombe hilo huko ugenini mbele ya miamba hiyo ya mchezo huo!
Kama tulivyowahi kuandika
hapa, Tanzania imepanda kwenye msimamo wa mwezi Desemba 2013 wa viwango
vya mchezo wanetiboli duniani toka nafasi ya 19 mpaka ya 17 ikiwa ya nne
barani Afrika, ikiziruka nchi maarufu kadhaa kwa mchezo huo kama
ifuatavyo na nafasi zao kwenye mabano:- Ireland
(29), Singapore (19), Malaysia (24), Switzerland (33), Namibia (26),
Zambia (23), Sri Lanka (22) and USA (18). Hii wala haikuwahi kuwa habari
popote zaidi ya kwenye mtandao huu wa www.tanzaniasports.com
Na
wala kwenye msimamo wa Januari 27, 2013 tulipokamata nafasi hiyo
hiyo na tukiwa nafasi ile ile ya nne barani Afrika tukizidiwa tu na
Malawi (5), Afrika Kusini (6) na Botswana (17) wala hiyo haikuwa habari
nchini Tanzania! Kinyume chake, tunachimba sana habari za soka kwa
sababu huko kuna biashara ya uhakika kupitia wasomaji, wasikilizaji na
watazamaji wetu walio wengi sana.
Serikali inabidi ivisaidie vyama kuwa na mashindano kama iivyokuwa Bonite Cup
Tukiutazama
mchezo wa basketiboli. Mchezo huu ndiyo unaoongoza kwa kutengeneza
mwanamichezo tajiri kuliko wote wa kitanzania. Huyu ni Hasheem Thabeet
wa timu ya Oklahoma City Thunder
ya moja ya ligi kubwa za basketiboli duniani ya NBA ya Marekani. Kupitia
changamoto ya mafanikio ya mchezaji huyo, wadau wa mchezo huo wa
Tanzania wangeuinua vya kutosha mchezo huo miongoni mwa vijana wa kizazi
hiki. Kinyume chake, kuna mashindano ya taifa ya mchezo huo yamefanyika
Tanga hivi karibuni bila msisimko wowote, kiushabiki na kihabari!
Kufuatia
kudorora kwa sasa kwa michezo mingine nchini ukiondoa soka, ipo haja
kwa wadau wa michezo hiyo mingine kuweka suala la kuiinua miongoni mwa
watoto wetu na vijana wetu kuwa moja ya mikakati yao ya kuendeleza
michezo hiyo. Wenyewe wawe wanahangaika kulazimisha habari zao kuingia
kwenye vyombo vya habari. Wasiige soka inayojitangaza yenyewe kwa ukubwa
wa upenzi inaopata toka kwa watu.
Nashauri
kila mdau wa mchezo wowote ule, uliopo na usiokuwepo nchini lakini wa
kimataifa kama Raga (Rugby) iliyo maarufu jirani kabisa hapa Kenya,
kuweka mikakati ya nguvu ya kuinua umaarufu wa michezo hiyo nchini kiasi
cha kuwajua na kuwashabikia wachezaji wake kama enzi za kina Flaviana
Makorongo na Jane Butinini wa mchezo wa netiboli au Dulla na Mwinuka wa
basketiboli.
Bila
kufanya hivyo, kuna siku watoto wetu watapita jirani na uwanja wa
netiboli au basketiboli na kuuliza ” eti yale yaliyosimamishwa ni manini
na yana kazi gani?” wakiuliza kuhusu milingoti ya magoli ya michezo
hiyo kama sasa hivi watoto wengi wa kitanzania waliozaliwa miaka ya 2000
kuja miaka hii wasivyojua chochote kuhusu ala za muziki wa dansi.
0 comments :
Post a Comment