Saa chache kabla ya kuanza kwa tukio maalumu la kihistoria la Ibada ya
Kitaifa ya kumuaga Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson
Mandela, makomandoo wa Marekani wameshika jukumu la ulinzi katika maeneo
nyeti nchini hapa. Ulinzi huo unatokana na ujio wa Rais wa Marekani,
Barrack Obama, mkewe Michelle pamoja na viongozi wa nchi mbalimbali,
ambao watahudhuria tukio linalotarajiwa kushuhudiwa na mamilioni ya
watu; ndani na nje ya Afrika Kusini.
Rais Jacob Zuma atahutubia katika ibada hiyo, ambayo itafanyika katika
Uwanja wa FNB (Soccer City), wenye uwezo wa kuchukua watu 95,000 kwa
wakati mmoja.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na Mawasiliano ya Afrika
Kusini inasema milango ya uwanja huo ambao ulitumika wakati wa sherehe
za ufunguzi na fainali za Kombe la Dunia 2010, itakuwa wazi kuanzia saa
12:00 na Ibada ya kwaheri inatarajiwa kuanza saa 5:00 asubuhi.
Karibu barabara zote za kuingia uwanjani hapo zimetangazwa kufungwa kwa
ajili ya magari yote, badala yake Serikali imeandaa usafiri wa bure kwa
wananchi watakaokwenda katika tukio hilo.
Jana, kutwa nzima, helikopta zilikuwa zikiruka katika anga la Jiji la
Johannesburg lakini zilitumia muda mwingi zaidi kuzunguka juu ya Uwanja
wa FNB ulioko Soweto, huku kukiwa na taarifa kwamba makomandoo wa
Marekani walikuwa kazini, kuhakikisha usalama wa kiongozi wao.
Pamoja nao, mamia ya polisi wa Afrika Kusini walionekana katika maeneo
yanayozunguka uwanja huo, huku baadhi ya vyombo vya habari vikiwanukuu
maofisa wa Serikali kwamba askari 11,000 watashiriki katika ulinzi
wakati wa maombolezo na mazishi.
Ulinzi pia umeimarishwa katika sehemu mbalimbali za Jiji la Johannesburg
pamoja na kule atakakozikwa katika Kijiji cha Qunu, Mthatha ambako
wanajeshi wenye silaha wamelizunguka eneo la makazi ya kiongozi huyo.
Maeneo mengine yaliyowekewa ulinzi mkali ni katika viwanja vya ndege na
katika Majengo ya Umoja (Union Buildings) jijini Pretoria ambako mwili
wa Mandela utawekwa kwa ajili ya wananchi kutoa heshima za mwisho kati
ya keshokutwa na Ijumaa.
Vituo vya televisheni vya Afrika Kusini vilionyesha magari ya kijeshi
zaidi ya 10 yakiwa yameegeshwa katika eneo linalozunguka makazi ya
Mandela, Qunu.
Waandishi waliokuwa wamepiga kambi karibu na makazi ya Mandela, Qunu
walihamishwa na kuwekwa mbali zaidi kutokana na sababu walizoelezwa kuwa
ni za kiusalama.
About feisal pinto
Computer Application Student, Author, Short Stories Writer, Business Proposal Writer, Presenter and Application Builder. Email feisalpinto4@gmail.com for complains and business only.
0 comments :
Post a Comment