Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic ameeleza kuwa kuna mambo mengi
yanayotakiwa kufanyiwa kazi katika kikosi cha Simba ili timu ifanikiwe
na jambo la kwanza aliloona halijakaa sawa ni mishahara ya wachezaji
Logarusic, raia wa Croatia aliiambia Mwanaspoti
kuwa wachezaji wengi wa Simba wanalipwa fedha tofauti na kazi au viwango
walivyo navyo, hivyo ni lazima uongozi uwe makini na jambo hilo.
Kocha huyo aliyepewa mkataba wa miezi sita kuinoa
klabu hiyo, alisema wachezaji wengi wa timu hiyo wanalipwa kiasi kikubwa
cha fedha huku wakionyesha uwezo mdogo uwanjani.
“Kuna wachezaji hapa wanalipwa mishahara kama
wachezaji wa kulipwa lakini matendo yao ndani na nje ya uwanja ni kama
wachezaji wa ridhaa, sasa hili ni tatizo katika timu unayotaka mafanikio
ndani ya muda mfupi,” alisema Logarusic mwenye umri wa miaka 51.
Mwanaspoti lilimshuhudia Logarusic akikasirika
mara kwa mara alipokuwa akitoa maelekezo kwa wachezaji wakikosea jambo
lililomfanya awaite wachezaji wote mara kwa mara na kuwaelekeza jambo la
kufanya.
Zoezi lililoonekana kumkwaza zaidi kocha huyo ni
lile la wachezaji wawili kushindwa kumtoka beki mmoja na kufunga ambapo
mabeki walifanya vizuri kwa kuwazuia washambuliaji na viungo waliopewa
jukumu la kufunga.
“Zoezi lile ni dogo tu la kupima uwezo wa mchezaji
awe kiungo, beki au mshambuliaji, lakini umeona wengi wameshindwa
kufunga kwa kuwa wanafanya mambo kama wachezaji wa ridhaa, wakati
wanalipwa kama wachezaji wa kulipwa,” alisema Logarusic.
Hata hivyo, Logarusic aliliambia Mwanaspoti hawezi
kuingilia mambo mengi ya wachezaji kwa kuwa wengi wana mikataba ambayo
haiwezi kuvunjwa kwa kuwa klabu itaingia gharama kubwa.
“Nitafanya kazi na wachezaji hawa hawa hadi mambo
yakapokaa vizuri na kwa uzoefu wangu najua nitafanikiwa kama
watanielewa,” alisema Logarusic aliyewahi kuinoa Gor Mahia ya Kenya.
0 comments :
Post a Comment