INAFAHAMIKA kuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, ametangaza kutogombea katika uchaguzi ujao wa klabu hiyo, lakini unafahamu kilichomfanya akaamua kugombea uenyekiti katika uchaguzi mdogo ule wa Julai mwaka jana? Mwenyewe anasema ni kipigo cha 5-0 walichopewa na Simba.
Yanga ilikumbana na kipigo hicho Mei 6 mwaka jana
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania
Bara ambapo wafungaji wa Simba walikuwa; Emmanuel Okwi (mawili), Felix
Sunzu, Juma Kaseja na Patrick Mafisango (marehemu sasa).
Wakati huo Yanga ilikuwa katika mgogoro wa uongozi
na aliyekuwa Mwenyekiti, Lloyd Nchunga, akalazimika kuachia ngazi ndipo
Manji alipochaguliwa miezi miwili baadaye katika uchaguzi uliofanyikia
Diamond Jubilee na kushinda kwa asilimia 97 ya kura.
“Niliamua kuwania uongozi Yanga baada ya Simba
kutufunga mabao 5-0, kwa kweli niliumia sana kuona tumefungwa idadi
kubwa ya mabao, sasa sitagombea tena maana timu inafanya vizuri na pia
ni wakati wangu wa kuachia wengine waje kuongoza,” alisema Manji.
Viongozi wengine walioingia madarakani na Manji
katika uchaguzi huo mdogo ni Clement Sanga (Makamu Mwenyekiti)
aliyejipatia asilimia 62 ya kura.
Wajumbe wa kamati ya utendaji ni Abdallah Bin Kleb, Moses Katabaro, Aaron Nyanda na George Manyama.
Nchunga alilazimika kujiuzulu baada ya wajumbe
wake wa kamati ya utendaji kuachia ngazi katika mgogoro huo, hivyo kwa
mujibu wa Katiba ya Yanga asingeweza kuendelea kuongoza peke yake.
0 comments :
Post a Comment