KUANZIA kwa wasaka ubingwa Chelsea, Arsenal, Liverpool, Everton na Tottenham Hotspur hadi kwa wanaopigania wasishuke daraja West Ham, Fulham, Stoke City na Crystal Palace, makocha wao stori zao zitafanana tu kwenye usajili wa Januari. Wanahitaji mastraika.
Wafungaji ni kitu kinachotingisha kwenye usajili
wa Januari wa Ligi Kuu England baada ya klabu zake kuhitaji watu wa
namna hiyo kuliko wengine wowote. Jambo hilo ni wazi litawagharimu pesa
nyingi ili kunusuru msimu kabla ya kufika Mei.
Mafundi wa kutikisa nyavu kama Gonzalo Higuain,
Radamel Falcao, Jordan Rhodes, Diego Costa na wengineo wanatajwa kati ya
mastraika watakaotingisha kwa siku 31 za usajili huo zitakapofunguliwa
rasmi.
Kocha wa Everton, Roberto Martinez, ambaye
alimsajili kwa mkopo Romelu Lukaku katika siku ya mwisho kwenye usajili
wa majira ya kiangazi ilikuwa safi kwenye kikosi chake, lakini tatizo
lililopo ni kuporomoka kiwango cha straika wake Nikica Jelavic, jambo
ambalo litamlazimisha kuingia sokoni ili kusaka mfungaji.
Sam Allardyce wa West Ham ameshaweka wazi kwamba
anatarajia kumnasa straika wa Ghana, Asamoah Gyan wakati wa dirisha la
usajili la Januari litakapofunguliwa.
Washambuliaji wanaosakwa
Chelsea na Arsenal zinapelekeshana kwenye kusaka
ubingwa wa Ligi Kuu England, zote zinahitaji kuwa na straika mmoja wa
nguvu na tayari zinagongana kwa Mcolombia, Radamel Falcao, anayekipiga
Monaco.
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho amekiri kuumizwa
na mastraika waliopo kwenye kikosi chake, Fernando Torres, Samuel Eto’o
na Demba Ba, ambao wote watatu wamefunga mabao matano tu kwenye ligi
msimu huu. Arsene Wenger wa Arsenal anadhani Olivier Giroud anahitaji
kupatiwa mtu wa kushindana naye kwenye safu ya ushambuliaji baada ya
sasa kuwa yeye tu, huku Nicklas Bendtner akishindwa kuaminika.
Ukimweka kando Falcao, Mourinho pia anamsaka
Gonzalo Higuain wa Napoli, huku Alladyce mipango yake ikiwa ni kumsajili
Jermain Defoe wa Tottenham.
Alvaro Morata wa Real Madrid anaziingiza vitani
klabu mahasimu wa London, Tottenham na Arsenal, wakati Filip Djordjevic
wa Nantes akiwa kwenye rada za klabu ya Hull City na Crystal Palace.
Straika wa zamani wa Sunderland, Asamoah Gyan,
anayekipiga Al-Ain kwa sasa anapigiwa hesabu kali na West Ham wakati
Mame Biram Diouf, aliyewahi kukipiga Manchester United lakini sasa yupo
Hannover anawindwa na Stoke City.
Arsenal inaonekana kusaka straika zaidi, wamemtaja
Kostas Mitroglou wa Olympiakos kuwa ni mtu mwingine wanayemhitaji, huku
usajili wa staa huyo ukiwaingiza vitani na Liverpool.
Baada ya kumkosa kwenye usajili wa Agosti, Arsenal imepanga
kurudi tena kwa Demba Ba wa Chelsea, huku Nikica Jelavic wa Everton
akiwindwa na klabu za Tottenham, Hull City na Crystal Palace.
Hawa ni baadhi tu ya mastraika wanaoweza kupatikana kirahisi katika usajili huo wa Januari.
Hali ilivyo
Kutimiza ndoto zake za kucheza Kombe la Dunia
mwakani, straika Jelavic ameelezwa na kocha wake Martinez kwamba akubali
kutolewa kwa mkopo kwenye usajili wa Januari. Lakini, tayari Everton
itakuwa na upungufu wa straika kutokana na Arouna Kone kuwa mgonjwa,
Martinez hana chaguo jingine zaidi ya kuingia sokoni na Fabio
Quagliarella wa Juventus ndiye mtu anayemhitaji.
Wenger amechoshwa na Oliver Giroud na hivyo
anawatazama zaidi Higuain na Falcao, sawa na Mourinho alivyochoshwa na
mastraika wake watatu ambao hawana maana yoyote kwenye ligi hadi sasa.
Kocha mpya wa Tottenham, Tim Sherwood hatakuwa na
uwezo wa kumgharimia Higuain, lakini tayari atakuwa na Pauni 20 Milioni
kwa ajili ya kumnasa straika mpya sawa na Brendan Rodgers wa Liverpool,
ambaye atahitaji kuongeza mtu mwingine wa maana ili kupunguza utegemezi
kwa Luis Suarez and Daniel Sturridge.
Kwenye nafasi za chini katika msimamo, kocha wa
Crystal Palace, Tony Pulis anataka mastraika wawili kukinusuru kikosi
hicho kinachougua ugonjwa wa mabao.
Stoke City nao wamekuwa wakisuasua kwenye ufungaji
na hilo litamfanya Mark Hughes kuingia sokoni. Kutokana na Andy Carroll
kuwa majeruhi, West Ham inahitaji kupata straika mpya mwezi ujao jambo
ambalo linaweza kushuhudia pesa nyingi sana zikitumika kwenye usajili wa
Januari kwa klabu hizo za Ligi Kuu England.
Mwaka 2011, kwenye usajili wa Januari klabu za
Ligi Kuu England zilishuhudia zikitumika Pauni 85 milioni kwa wachezaji
wawili tu, Andy Carroll alipotua Liverpool na Fernando Torres
alipotimkia Chelsea kwa Pauni 50 milioni. Kiwango hicho kilikuwa kikubwa
sana kwenye usajili kwa Januari pekee, lakini msimu huu mambo yanaweza
kuwa tofauti zaidi kutokana na klabu nyingi kuhitaji mastraika,
wachezaji ambao wanaaminika kuwa ghali zaidi kwenye soko la usajili wa
wachezaji.
0 comments :
Post a Comment