.

.

SHOP HERE

News
Loading...

.

.

.

shop now

YANGA JEURI BWANA


BAADA kuhakikisha imemtia ndani ya himaya yake straika ghali wa Afrika Mashariki, Emmanuel Okwi, Yanga sasa imeelekeza nguvu zake zote kwa kocha mwenye jina kubwa, Bobby Williamson, ambapo matajiri wa sasa wa Mskochi huyo, Gor Mahia, ya Kenya wanaelekea kukubali yaishe.
Yanga imefanya mazungumzo ya kina na Bobby na kimsingi kocha huyo amekubali ila ameomba kwanza akutane na mabosi wake wa Gor Mahia ambao wana mkataba naye wa miezi sita kuangalia jinsi ya kulimaliza suala hilo.
Bobby aliiambia Mwanaspoti jana Jumatatu kwa njia ya simu kutoka Nairobi akisema: “Ni kweli Yanga wananihitaji, lakini siyo Yanga pekee kwani nimekuwa nikifuatwa sana. Lakini nasema mimi ni kocha ambaye ninaheshimu mkataba wangu wa kazi, nimewaomba kwanza waanze kuzungumza na uongozi wa klabu hasa Mwenyekiti.
“Mimi ni kocha wa Gor Mahia, napenda kufuata taratibu katika kufanya kazi zangu, ninafuraha kuwa hapa lakini kama kunaweza kuwa na mabadiliko hakuna shida, itategemea nini uongozi wa Gor Mahia utaniambia.”
Hata hivyo Bobby alionekana kushituka alipojua kwamba Mholanzi,  Ernest Brandts, amefukuzwa Yanga licha ya kuwa timu hiyo inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Alisema: “Kama timu inaongoza ligi inakuwaje wanamfukuza kocha wao? Lakini hayo ni maoni yao, naomba kwanza uongozi wa Yanga ufuate taratibu kwa kuzungumza na uongozi wa Gor Mahia, kwa sasa nasubiri kuanza maandalizi ya msimu mpya, tutaanza kambi Ijumaa ya wiki hii.”
Mwenyekiti Gor Mahia
Mwenyekiti wa Gor Mahia, Ambrose Rachier, amepokea taarifa ya kuhitajika kwa kocha wao kutoka kwa Bobby mwenyewe na kiongozi huyo pia amethibitisha kupokea ujumbe mwingine kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, ambaye ameomba kukutana naye bila ya kumtajia ajenda.
“Unavyonipigia tayari nimeshapokea ujumbe kutoka kwa kocha wangu (Bobby), amenitaarifu juu ya Yanga wanavyomuhitaji, bado sijamjibu,” alisema.
“Lakini wakati najipanga cha kumjibu, nimepata ujumbe mwingine kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga, ameniomba nikutane nizungumze naye.
“Gor Mahia hatuwezi kumzuia Bobby kuondoka endapo atakuwa tayari kuondoka, nipo kijijini nikirudi mjini nitaongea na Bobby kama atakubali kuondoka ndiyo nitazungumza na huyo kiongozi wa Yanga kujadiliana nini wanatakiwa kukifanya katika kuuvunja huu mkataba wetu na kocha.”
Kocha Mbelgiji

Mwanaspoti pia iliwasiliana na kocha Mbelgiji, Luc Eymael, ambaye yupo kwenye orodha ya makocha wanaowindwa na Yanga.
Mbelgiji huyo alisema: “Niliwasiliana na mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni kiongozi wa Yanga, tulikuwa tunawasiliana kupitia barua pepe, ameniambia kuwa wananihitaji.
“Mimi sasa ni kocha huru baada ya kuondoka AFC Leopards (pia ya Kenya) miezi michache iliyopita, nimewafuatilia Yanga ni timu nzuri, ipo katika nafasi ya kwanza katika ligi ya huko Tanzania, kama watakuja na ofa nzuri nitajiunga nao, kwa sasa nimeshakataa ofa mbili kutoka Algeria nawasubiri hao Yanga.”
Yanga wenyewe
Uongozi wa Yanga umetangaza kuwa zaidi ya makocha 42 wameomba kazi na wanatoka nchi mbalimbali za mabara ya Asia, Ulaya na Amerika Kusini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu, aliliambia Mwanaspoti akisema: “Idadi ya makocha ambao hadi sasa wametuma maombi ni zaidi ya 42, bado maombi yanaendelea kutumwa na imani yangu mwisho utakuwa mwanzoni mwa mwaka mpya, lakini kwa sasa ni mapema kuweka wazi majina yao.”
Share on Google Plus

About feisal pinto

Computer Application Student, Author, Short Stories Writer, Business Proposal Writer, Presenter and Application Builder. Email feisalpinto4@gmail.com for complains and business only.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment

ad