BAADA kuhakikisha imemtia ndani ya himaya yake straika ghali wa Afrika Mashariki, Emmanuel Okwi, Yanga sasa imeelekeza nguvu zake zote kwa kocha mwenye jina kubwa, Bobby Williamson, ambapo matajiri wa sasa wa Mskochi huyo, Gor Mahia, ya Kenya wanaelekea kukubali yaishe.
Yanga imefanya mazungumzo ya kina na Bobby na
kimsingi kocha huyo amekubali ila ameomba kwanza akutane na mabosi wake
wa Gor Mahia ambao wana mkataba naye wa miezi sita kuangalia jinsi ya
kulimaliza suala hilo.
Bobby aliiambia Mwanaspoti jana Jumatatu kwa njia
ya simu kutoka Nairobi akisema: “Ni kweli Yanga wananihitaji, lakini
siyo Yanga pekee kwani nimekuwa nikifuatwa sana. Lakini nasema mimi ni
kocha ambaye ninaheshimu mkataba wangu wa kazi, nimewaomba kwanza waanze
kuzungumza na uongozi wa klabu hasa Mwenyekiti.
“Mimi ni kocha wa Gor Mahia, napenda kufuata
taratibu katika kufanya kazi zangu, ninafuraha kuwa hapa lakini kama
kunaweza kuwa na mabadiliko hakuna shida, itategemea nini uongozi wa Gor
Mahia utaniambia.”
Hata hivyo Bobby alionekana kushituka alipojua
kwamba Mholanzi, Ernest Brandts, amefukuzwa Yanga licha ya kuwa timu
hiyo inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Alisema: “Kama timu inaongoza ligi inakuwaje
wanamfukuza kocha wao? Lakini hayo ni maoni yao, naomba kwanza uongozi
wa Yanga ufuate taratibu kwa kuzungumza na uongozi wa Gor Mahia, kwa
sasa nasubiri kuanza maandalizi ya msimu mpya, tutaanza kambi Ijumaa ya
wiki hii.”
Mwenyekiti Gor Mahia
Mwenyekiti wa Gor Mahia, Ambrose Rachier, amepokea
taarifa ya kuhitajika kwa kocha wao kutoka kwa Bobby mwenyewe na
kiongozi huyo pia amethibitisha kupokea ujumbe mwingine kutoka kwa
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, ambaye ameomba kukutana naye
bila ya kumtajia ajenda.
“Unavyonipigia tayari nimeshapokea ujumbe kutoka
kwa kocha wangu (Bobby), amenitaarifu juu ya Yanga wanavyomuhitaji, bado
sijamjibu,” alisema.
“Lakini wakati najipanga cha kumjibu, nimepata
ujumbe mwingine kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni Makamu
Mwenyekiti wa Yanga, ameniomba nikutane nizungumze naye.
“Gor Mahia hatuwezi kumzuia Bobby kuondoka endapo
atakuwa tayari kuondoka, nipo kijijini nikirudi mjini nitaongea na Bobby
kama atakubali kuondoka ndiyo nitazungumza na huyo kiongozi wa Yanga
kujadiliana nini wanatakiwa kukifanya katika kuuvunja huu mkataba wetu
na kocha.”
Kocha Mbelgiji
Mwanaspoti pia iliwasiliana na kocha Mbelgiji, Luc Eymael, ambaye yupo kwenye orodha ya makocha wanaowindwa na Yanga.
Mbelgiji huyo alisema: “Niliwasiliana na mtu mmoja
aliyejitambulisha kuwa ni kiongozi wa Yanga, tulikuwa tunawasiliana
kupitia barua pepe, ameniambia kuwa wananihitaji.
“Mimi sasa ni kocha huru baada ya kuondoka AFC
Leopards (pia ya Kenya) miezi michache iliyopita, nimewafuatilia Yanga
ni timu nzuri, ipo katika nafasi ya kwanza katika ligi ya huko Tanzania,
kama watakuja na ofa nzuri nitajiunga nao, kwa sasa nimeshakataa ofa
mbili kutoka Algeria nawasubiri hao Yanga.”
Yanga wenyewe
Uongozi wa Yanga umetangaza kuwa zaidi ya makocha
42 wameomba kazi na wanatoka nchi mbalimbali za mabara ya Asia, Ulaya na
Amerika Kusini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu,
aliliambia Mwanaspoti akisema: “Idadi ya makocha ambao hadi sasa
wametuma maombi ni zaidi ya 42, bado maombi yanaendelea kutumwa na imani
yangu mwisho utakuwa mwanzoni mwa mwaka mpya, lakini kwa sasa ni mapema
kuweka wazi majina yao.”
No comments:
Post a Comment