MAKOCHA wa Simba, Zradvko Logarusic na msaidizi wake Selemani Matola ambaye ni Baba mlezi wa soka wa Ramadhani Singano ‘Messi’, hawakumpa nafasi ya kwanza mwanasoka huyo katika mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga iliyochezwa Desemba 21 mwaka jana.
Huenda hawakumwandaa kucheza au hawakumwamini, ni
tofauti na ilivyokuwa kwa Said Ndemla aliyeanza. Hata hivyo, ni kwamba
Singano alikuwa katika kiwango cha juu mno cha uchezaji wake siku hiyo
kiasi cha kusababisha madhara makubwa kwa wana wa Jangwani.
Singano ameleta mtafaruku mkubwa pale Jangwani,
Sasa kocha, Ernest Brandts, ambaye hivi karibuni mkataba wake uliongezwa
muda wa mwaka mmoja, keshapewa notisi. Masikini Kelvin Yondani na Nadir
Haroub ‘Cannavaro’ wako kikaangoni, eti walicheza chini ya kiwango.
Watu wanasahau kuwa Singano alikuwa katika kiwango
chake cha mwisho kabisa cha ubora, kinachotakiwa sasa kwake ni kutafuta
malisho mengine kulingana na umri wake ulivyo.
Yondani na Cannavaro hawana makosa hata kidogo,
umri wao unawaruhusu kabisa kucheza walivyocheza mbele ya dogo Singano
mwenye umri usiozidi miaka 21.
Nitashangaa nikimkuta Singano akiwa Mtaa wa Samora
akitafuta kununua TV kubwa na redio ya kisasa, nitafadhaika nikimwona
Singano na wapambe wake wakitafuta kiwanja maeneo ya Chamazi, Mbande au
Tuangoma, inaniuma mno nikisikia watu wanamsifia Singano eti ana akili
kisa kanunua gari la biashara kalipaki pale Buguruni.
Natamani niwe mshauri wake sasa, natamani
ningekuwa wakala wa wachezaji kama alivyo rafiki yangu, Damas Ndumbalo.
Ningekuwa hivyo nisingemwacha Singano hivi hivi, ningehakikisha namuuza
Ulaya.
Singano ana kila kitu katika soka cha kumfanya
asajiliwe Ulaya, kama kuna kitu anachopungukiwa nacho ni nguvu tu. Ili
Singano aingie kwenye soka la ushindani, ni lazima aachane na biashara
ya kununua TV, redio au kiwanja. Ni lazima apigane na kula, ni lazima
afikie hatua ya kuweza kula kuku wa kinyeji wawili na kunywa lita mbili
za maji kwa wakati mmoja.
Singano atakapofikia malengo ya kupambana na
Wazungu katika baridi kali, mahali ambapo soka linalipa, nafasi ya
kununua kiwanja itakuwa haipo tena atakuja kununua mtaa mzima pale
Masaki. Hivyo ndiyo soka lilivyo.
Katika moja ya makala zangu, niliwahi kumwambia
Mbwana Samatta aende Simba, aifanye klabu hiyo njia na sasa wanaomwona
Samatta hawana la kusema. Wenye macho ya kuona mbali tumekuona Singano,
Simba na Tanzania kwa ujumla si mahala pako, ondoka katafute malisho
mengine.
Damas Ndumbalo, Salehe Ally wa Zanzibar, Saidi
Tully sifa yenu nyie ni mawakala. Hivi kweli hamjamwona Singano? Au
macho yangu siku hizi ni ya makengeza?
Naamini ni wakati wenu sasa wa kumtamfutia mtu
maalumu au watu maalumu wa kumwandaa Singano kimazoezi, kiafya na
kisaikolojia ili awe Singano anayestahili. Kwa sasa anatakiwa aishi
maisha ya kuvuna kulingana na kazi yake, maisha ya kutoka jasho la damu
ili muda mfupi ujao dunia imtambue.
Ni jukumu lenu kumwandaa, kumuachanisha na matajiri uchwara wa
nchini ambao siku zote kwao ni fahari kuwahodhi wachezaji wazuri
kujilinda na migogoro kwenye klabu zao, lakini mwishowe wanawatupa.
Ni jukumu lenu akina Ndumalo kumwelekeza kijana
huyo awaangalie akina Haruna Moshi ‘Boban’, Athuman Idd ‘Chuji’, Amri
Kiemba, Mrisho Ngassa jinsi walivyopoteza dira. Miguu yao imejaa utajiri
kwa soka walilojaaliwa, lakini wanaishia hapa hapa bila ya kuwa na
mavuno makubwa.
No comments:
Post a Comment