MSHAMBULIAJI wa Yanga, Mrisho Ngassa ‘Anko’, ameandika historia kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufunga ‘hat trick’ katika mechi mbili mfululizo na bado bao moja tu aifikie rekodi ya Mfungaji Bora wa mashindano hayo msimu uliopita, Mcameroon Alexis Yougouda Kada wa Coton Sport ya Cameroon.
Lakini cha kushangaza, Ngassa amenyimwa mpira na
Shirikisho la Soka la Comoro. Mwamuzi wa mchezo huo alimpa Ngassa mpira
baada ya mechi kwa mujibu wa kanuni, lakini shirikisho hilo likamfuata
likimuomba awaachie tu mpira huo kwa vile hawana mingi.
Ngassa aliiambia Mwanaspoti kwamba walimuomba
asichukue mpira huo baada ya kuzungumza na viongozi wa Yanga ambao
wameahidi kwa watampa mpira wakishafika jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Ngassa, rekodi yake ya kupiga mabao
matatu peke yake ugenini, ilishatabiriwa na swahiba wake wa karibu
ambaye ni mwamuziki, Diamond Platnumz.
Ngassa mwenye kasi na akili ya mpira, alifunga
‘hat trick’ hizo kwenye mechi zao na Komorozine ya Comoro. Alianza na
ile ya Dar es Salaam waliposhinda 7-0 na kisha marudiano ya juzi
Jumamosi ya Comoro waliposhinda 5-2.
Kwa mabao yake sita, amebakiza moja tu ili aifikie
ya Yougouda ambaye aliibuka kinara mbele ya Mmisri Ahmed Gaafar wa
Zamalek ya Misri na Muivory Coast, Mamadou Soro, wa AFAD Djekanou ya
Ivory Coast. Hao msimu uliopita walifungana kwa kuwa na mabao sita kila
mmoja.
Lakini Yougouda alishindwa kuvunja rekodi ya
Mghana Emmanuel Clottey wa klabu ya Berekum Chelsea ya Ghana aliyemaliza
na mabao 12 msimu wa mwaka 2012 na waliomfuatia walikuwa wamefungana;
Mohamed Aboutrika wa Al-Ahly ya Misri, Mtanzania Mbwana Samata na Mcongo
Tresor Mputu wote wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,
wao walikuwa na mabao sita kila mmoja.
Ngassa ambaye anatua nchini asubuhi ya leo
Jumatatu na kikosi chake cha Yanga, alisema hiyo ni furaha kubwa kwake
kufunga mabao hayo na malengo yake ni kuweka rekodi zaidi na kuibuka
mfungaji bora wa mashindano hayo msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu, Ngassa
alisema: “Diamond bwana ni mtu wa ajabu, naweza kusema maono yake ni
sawa na mtabiri, aliniambia kwenye mechi ya Comoro ni lazima nitafunga
‘hat trick’ na ndiyo imekuwa kweli.
“Katika kumshukuru rafiki yangu kipenzi huyo, mabao yote haya, nimemzawadia yeye. Hata mpira nitakaopewa na klabu nitampa yeye.”
Akizungumzia mechi yao na Al Ahly, Ngassa alisema:
“Kila kitu kinawezekana, nina imani hao Al Ahly tutawatoa tu kikubwa
dua kutoka kwa wadau wa soka, wapenzi wa Yanga na watu wote.”
chanzo:mwanaspoti
chanzo:mwanaspoti
0 comments :
Post a Comment