Wachezaji wa timu ya Yanga wakishangilia ushindi wa bao moja dhidi ya timu ya Al-Ahly ya Misri |
Wakati jopo la Yanga lilitangulia kuwasili Cairo
jana Jumapili kudhibiti mbinu za Waarabu hao na kuhakikisha hakuna
fitna yoyote itakayofanyika, wenyeji wao walikuwa nchini ambapo jioni
walifanya mazoezi yao ya mwisho na baadaye kula chakula cha usiku na
maofisa wa ubalozi wao nchini na wataondoka leo Jumatatu.
Matajiri hao ambao ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Mashindano ya Yanga, Abdallah Binkleb na Mwenyekiti wa Kamati ya
Mashindano ya Kimataifa, Seif Ahmed wamewaongoza wanachama wengine
kuingia msituni kuidhibiti Ahly kwa ushirikiano na Watanzania wanaoishi
jijini Cairo, Misri.
Seif aliondoka nchini kimyakimya na akaliambia
Mwanaspoti kwamba wamepania kuiondosha Ahly na wanachokwenda kufanya ni
kuhakikisha Wachezaji wa Yanga wanakuwa chini ya uangalizi mkali katika
kila dakika tangu watakapotua kwenye Uwanja wa Ndege Alhamisi wiki hii.
Seif alisisitiza kuwa walishaanza kuweka mazingira
mapema, lakini sasa wanakwenda kujidhatiti zaidi kuanzia kwenye Uwanja
wa kufanyia mazoezi, hoteli, mabasi pamoja na vyakula kwani hawataki
kutumia kitu chochote cha wenyeji ili kuepuka hujuma kwenye mechi hiyo
itakayochezwa Jumapili usiku.
“Tumepata ushindi wa kihistoria lakini hatuwezi
kukaa chini kushangilia, kwa sasa tunatakiwa kuanza maandalizi ya mechi
ya marudiano ndio maana naondoka kuelekea Misri kufanya mambo,”
alisisitiza Seif.
“Tunatakiwa kujipanga vizuri kabla ya mchezo wa
marudiano, kabla ya timu kufika kuna mambo ambayo ni lazima tuyaweke
sawa ili kukamilisha lengo letu la kusonga mbele, kuna haja ya kuandaa
sehemu salama ya kufikia kikosi chetu, wapi tutafanyia mazoezi ni lazima
tuyafanye hayo yote sasa, hawa jamaa inabidi kuwa nao makini sana.”
Akizungumza na Mwanaspoti, Abdallah Bin Kleb
alisema: “Tunajua wenzetu watakuwa wamejiandaa kuhakikisha wanatufunga
nyumbani kwao, hivyo tumeanza maandalizi rasmi katika kuhakikisha
tunapata ushindi ugenini baada ya kuwafunga nyumbani.
“Kiongozi mmoja anatangulia Misri, timu inaondoka
Alhamisi na kufika Ijumaa, itachelewa kuondoka kutokana na mechi hiyo
kuchezwa Jumapili.”
Kocha Al Ahly aitisha
Kocha Mkuu wa Al Ahly, Mohamed Youssef, amesema kuwa hatakubali kufungwa mara mbili na Yanga, ugenini na nyumbani.
“Nimeziona mbinu za wapinzani wangu Yanga, sina
hofu ya mechi ya marudiano tutakayorudiana na wapinzani wetu, nimepanga
kwenda kukiboresha kikosi changu ili mechi ya marudiano tushinde,”
alisema.
“Yanga ni timu nzuri yenye wachezaji wazuri, lakini hilo
haliniogopeshi kabisa, bado tunayo nafasi kutokana na wapinzani wetu
kutufunga bao moja tu, nina matumaini makubwa ya kushinda mechi hiyo.”
Kocha Yanga kushambulia
Kocha Mholanzi wa Yanga, Hans Van Der Pluijm,
amesema: “Tumeshinda nyumbani lakini bado tuna mechi ya marudiano na
tutakuwa kwao ambako wana sifa moja ya kutofungika. Kwa sababu najua
mbinu zao, nimejiandaa nao, tunaenda kucheza kwa kushambulia tu bila
woga, ushindi huu wa bao 1-0 hauwezi kutudanganya kuwa kule tukazuie tu,
haitakuwa hivyo.
“Mnapozuia ni kwamba mmeridhika, lakini sisi
tutatafuta ushindi tu, wale jamaa wanapokuwa kwao ndiyo wanakuwa wajanja
sana na mbinu nyingi, lakini pamoja na mambo yao yote hayo,
hatutawahofia na tutawafunga huko huko kwao.”
Okwi aonya
Emmanuel Okwi, amefurahi kuvunja mwiko kwa
kuisadia timu yake kupata ushindi wa bao 1-0 lakini akawashushia onyo
zito wachezaji wenzake akiwamo yeye mwenyewe.
“Ukweli ni kwamba kupata ushindi katika mechi ya
nyumbani ni jambo ambalo kila mmoja wetu atalifurahia, mechi ilikuwa
ngumu lakini sasa ni wakati mimi pamoja na wachezaji wenzangu kuanza
kufikiria kuhusu mchezo ujao wa marudiano na kuacha kushangilia huu
mchezo wa kwanza,” alisema Okwi.
“Bado tuna dakika 90 nyingine ugenini, ambazo
naamini hazitakuwa rahisi kwetu, tunatakiwa kujituma zaidi kama kweli
tuna lengo la kusonga mbele, hawa jamaa wanakwenda kujipanga kutukabili
na sisi lazima tijiandae kwa kiwango kikubwa.”
Haruna Niyonzima yeye alisema; “Walitumia historia
yao kutubeza na kuonekana sisi hatuwezi kitu mbele yao, sasa kila mtu
anatuamini na ninakueleza kuna kitu tutafanya na tutatambulika Afrika
yote. Nasema lazima tushinde.”
0 comments :
Post a Comment