BILIONEA mmiliki wa kampuni ya mafuta ya Lake Oil, Ally Edha Awadhi anayetafutwa na polisi kwa kosa la kumnyanyapaa, kumdhulumu, kumtesa na kumjeruhi mfanyakazi wake, ametoweka na huenda akawa amekimbilia nje ya nchi, Uwazi limenasa mkanda mzima.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, (DCI) Kamishna Isaya Mngulu (pichani) aliliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki ofisini kwake kuwa bilionea huyo na wafanyakazi wake wanaotuhumiwa kutenda vitendo hivyo kwa kutii maelekezo yake, Mei mwaka jana, hawaonekani.
“Kwa sasa timu yangu ya upelelezi inaendelea kumsaka mtuhumiwa huyo na atakapokamatwa atafikishwa katika vyombo vya sheria na tumejipanga vizuri, tutamnasa tu,” alisema Mngulu.
Polisi walianza kufuatilia suala hilo baada ya mfanyakazi aliyefanyiwa unyama huo kuandika barua kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akilalamika kutotendewa haki kwa shauri lake, hivyo kumfanya mtendaji huyo mkuu wa shughuli za serikali kuliagiza jeshi la polisi kufuatilia upya suala hilo.
Baadhi ya mambo aliyolalamikia kwa Pinda ni pamoja na kupigwa, kujeruhiwa mwili mzima, kudhalilishwa na kudhulumiwa mali zake kama nyumba, magari mawili Toyota lenye namba za usajili, T 786 BZG na Toyota Fortuner namba T503 BQC, bastola, fedha taslim dola za Kimarekani 100,000, mkataba wake wa nyumba, maduka yake na ofa zake tatu za viwanja huko Kigamboni.
Tukio hilo la kuteswa kwa mfanyakazi huyo aliyekuwa mhasibu katika kampuni hiyo lilitokea Mei 2, mwaka jana.
0 comments :
Post a Comment