Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye amesema iwapo misingi ya uchaguzi ndani ya CCM italalia kwenye rushwa, hataendelea kuwa mwanachama na kuonya kuwa tatizo hilo limefikia pabaya na litakiangusha chama hicho.
Sumaye, ambaye alipewa adhabu ya kudhibitiwa kwa miezi 12 kwa kosa la kuanza kampeni za urais mapema, alisema msimamo wake wa kupinga rushwa na tabia yake ya kujishirikisha kwenye mambo ya kijamii vinaweza kuwa sababu ya kutuhumiwa kufanya kampeni na baadaye kupata adhabu hiyo.
Alionya kuwa vurugu zinazotokea sasa, hasa kwenye mikoa ya Kusini si ajali, bali hasira za wananchi dhidi ya viongozi wao ambao alisema wamejitenga baada ya kupata madaraka na hivyo wananchi wanatumia kila nafasi wanayoipata kuwaadhibu.
Katika mahojiano maalumu na waandishi wa gazeti hili, Sumaye ambaye alijitokeza kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2005 lakini hakupitishwa na CCM, alisema hawezi kuendelea kuwamo kwenye chama endapo kitachagua viongozi kwa rushwa.
“Suala si kama mimi nagombea au sigombei… Hata kama sigombei. Kama nitajiridhisha mwenyewe kuwa huyu amefika pale (amechaguliwa) kwa sababu ya rushwa, sitakuwapo sehemu hiyo (kwenye chama hicho), hata kama sigombei,” alisema Sumaye katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwake Kiluvya, takribani kilomita 30 kutoka jijini Dar es Salaam.
Sumaye, ambaye ndiye waziri mkuu pekee aliyemaliza awamu mbili za jumla ya miaka 10 bila ya kuondolewa, alikuwa akijibu maswali kuhusu mustakabali wake ndani ya CCM ambayo anadai imetawaliwa na rushwa. Maswali hayo na majibu yake yalikuwa:
Waandishi: Mwanzo ulisema rushwa inapokithiri kuna watu wanaweza wakatoka kwenye chama. Inavyoonekana katika mazungumzo yetu haya, wewe ni mtu ambaye unaichukia sana rushwa. Unafikiri, hivi (rushwa) inavyoendelea na labda kwenye uchaguzi wa mwakani itakuwa hivyo, unaweza siku moja ukatoka CCM?
Sumaye: Hilo nafikiri nilishawahi kulisema… nilisema kama misingi ya uchaguzi kwenye Chama Cha Mapinduzi italalia kwenye rushwa, mimi sitakuwa sehemu ya hiyo. Hilo nilishalisema na wala sibahatishi. Sasa suala si kama mimi nagombea au sigombei, hata kama sigombei. Lakini… kama nitajiridhisha mwenyewe kuwa huyu amefika pale (amechaguliwa) kwa sababu ya rushwa, sitakuwapo sehemu hiyo. Hata kama sigombei.
Waandishi: Utakuwa radhi kusema sipo mahali hapa?
Sumaye: Sasa kama naweza kusema sasa, unataka nisemeje? niandike kwa damu? (anacheka).
Sumaye, ambaye alishindwa kwenye uchaguzi wa wajumbe wa Nec mwaka 2012 kwenye Wilaya yake ya Hanan’g, alisema nchi imefika mahali pabaya kiasi kwamba watu wanaona wakati wa uchaguzi ndiyo halali kwao kupokea rushwa.
“Unajua, imefika mahali watu hawawezi kujitokeza kwa sababu inaonekana mazingira yanayotakiwa ni ya rushwa. Kwa hiyo anasema ah, ya nini? Hata usiende kwenye ngazi ya urais, hivi unadhani hakuna watu wazuri ambao wangekuwa wabunge? Wako,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Hanang na kuongeza:
“Lakini wanasema to hell (potelea mbali). Kwa nini niende nikajiaibishe wakati wananchi watakachotaka ni hela? Kwa sababu sisi tumewafikisha hapo… nenda dada gombea uenyekiti wa mtaa, uone kama una plot kama hujaiuza! Kwa sababu wananchi wanasema ‘huyu anakuja kugombea. Tuone atatuletea nini. Hapo hujagawa khanga, fulana, pochi, bahasha hazijatembea. Unaona? It’s that filthy… na tumewafikisha wananchi wetu sasa wanafikiri wakati wa kampeni ni halali kwao kula rushwa. Actually wanadhani ni wakati wa mavuno, which is nonsense (ni upuuzi).”
Sumaye alisema vitendo vya wananchi wa Masasi au Liwale kuchoma nyumba za wabunge, polisi au madiwani, havitokani na kukasirishwa na kugongwa kwa bodaboda, bali hasira dhidi ya viongozi wao na hivyo hutumia nafasi hiyo kuwaadhibu.
“Wale wa Masasi; bodaboda anagongwa na gari la polisi, wanachoma nyumba ya mbunge, wanachoma halmashauri, wanachoma polisi. Hivi unadhani ni kwa sababu ya bodaboda kugongwa? Bodaboda? Watu kila siku wanauawa.
“Kila mtu anawajua (waendesha bodaboda). Hata kama wasingekuwa rough… sasa hiyo ni traffic case. Watu wamekutana barabarani, kwa nini wakachome magari ya wabunge na nyumba za wabunge? Lazima msome maandishi kwenye ukuta,” alisema Sumaye akimaanisha hadithi ya kwenye Biblia ya Mfalme Belishaza ambaye alitumia vyombo vya ibada kunywea pombe na baadaye kiganja cha mkono kikajitokeza ukutani kuandika “ufalme wako umekwisha”.
“Tumefika mahali pagumu. Kule Liwale wananchi wamechoma nyumba zote za madiwani na wote ni wa CCM, wamechoma nyumba ya mbunge na ya mama yake mbunge wakachoma. Eti (kwa sababu) bei ya korosho inashuka na kupanda! Diwani anapanga bei ya korosho?
“Watu hamuoni tu vitu ambavyo watu wanafanya. Mnadhani ni ajali tu zinatokea. Wapo watu wanachukizwa kabisa na rushwa na wanaumizwa kabisa na rushwa. Ninyi waandishi wengine mnaweza kufaidika na rushwa, lakini itakupeleka wapi.”
Hata hivyo, Sumaye alisema kwa sasa mambo yamebadilika kiasi kwamba hata vyombo vya habari vimekuwa tofauti.
“Ukisoma magazeti ya sasa ni tofauti. Zamani ulikuwa unasoma mpaka unatamani uhame nchi, mambo ya ajabu kabisa,” alisema.
Kuhusu mustakabali wa chama hicho kilichoshika madaraka kwa takribani miaka 50 sasa, Sumaye alisema anavyokiona, kama hakitadhibiti rushwa, kitakufa.
Alisema ndani ya CCM na serikalini wapo viongozi wasiofaa kutokana na kuwa wamechaguliwa kwa kutumia rushwa.
“Kwa mfano tuseme wewe unataka kugombea Ulanga na wananchi wanakujua, wanakutaka ugombee, lakini akaja mtu mwingine mwenye mapesa akawahonga viongozi wa pale Ulanga kisha anapita yeye… yule mtu anayependwa na wananchi walio wengi atahamia chama kingine na unafikiri nini kitatokea? CCM itapoteza kiti kile. Sasa kama zaidi ya nusu ya nchi ikifanya hivyo, unafikiri nini kitatokea?” alihoji.
Alisema hiyo inatokana na mabadiliko makubwa yaliyopo nchini kwa sasa, akifafanua kuwa wananchi wengi wamebadilika, wamekuwa na upeo mkubwa wa kutazama na kuelewa mambo na kuwa wanajua wanachotaka na kamwe hawahadaiki kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Source: Mwananchi
0 comments :
Post a Comment