MOJA ya tatizo kubwa linalowasumbua wasanii wetu, hasa hawa wa muziki wa kizazi kipya, ni ukosefu wa usimamizi makini wa kazi zao za sanaa, au kama wazungu wanavyosema, Management. Wenyewe, hasa chipukizi wanaotaka kutoka, utawasikia wanasema, nina kipaji lakini sina meneja. Ingawa wanaposema meneja maana yake ni msimamizi wa kazi zao, lakini kwao huwa na maana pana zaidi, kwamba mtu huyo, ndiye awe bosi wake, amsaidie hela ya studio, kazi ikitoka aipeleke redioni kisha awe ndiye msimamizi na mpangaji wa kila kitu chake. Mikataba wanayoingia na mameneja hawa, huwaonyesha wao kama waajiriwa. Baada ya hapo ni kufuata amri zao, ndiyo maana
unaona wasanii wanakejeliwa hadi kuwekwa mitandaoni eti wanawaomba misamaha mameneja wao. Inatisha! Ukweli mmoja ambao wasanii wetu wanashindwa kuelewa ni kwamba wao ndiyo mabosi, wao ndiyo hasa wanapaswa kunyenyekewa. Meneja hawezi kuingiza hela kama msanii hapati shoo, hauzi kazi zake wala hapati matangazo. Kazi ya meneja ni kutafuta kazi, akishapata anarudi kwa bosi wake na kuweka mezani mazungumzo ya masilahi. Ni wajibu wa msanii kukubali au kukataa kutegemea na jinsi anavyojichukulia. Lakini huku ni kinyume chake, meneja anazungumza kila kitu kuhusu kazi na masilahi, msanii wetu anaambiwa tu panda jukwaani, malipo yako haya hapa!Nimegundua kwa nini wasanii wetu wengi wanaendelea kuwa kama walivyo baada ya kuongea na mmoja kati ya mameneja wa msanii Nasibu Abdul ‘Diamond’ anayeitwa Babu Tale. Kama tunavyojua, juzikati dogo alikutana na msala kule Ujerumani, baada ya kuchelewa kuingia ukumbini kwenye shoo yake na mashabiki, wengi wao wakiwa ni raia wa Afrika Mashariki, walipolianzisha na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali. Ilikuwa ni halali yao kufanya fujo, kwa sababu licha ya kukata tiketi na kuingia ukumbini saa nne usiku, Diamond alitokea ukumbini saa kumi usiku! Sasa nikampigia ili kusikia anasemaje juu ya tukio hilo, hasa baada ya kuwepo kwa habari kwamba promota aliyemualika Diamond huko Ulaya (Tunaambiwa Mnigeria flan mjanjamjanja) alipaswa kulipa hasara iliyopatikana pamoja na kijana wetu. Nikiri pia kwamba nimeanza kumsikia siku nyingi Babu Tale, kipindi kile cha ujio wa Tip Top Connection, ingawa sijawahi kufanya naye kazi.Aliniambia hivi: “Kipromosheni hii ni nzuri sana kwa sababu itamtangaza sana, kiasi cha watu kutaka kujua hivi Diamond ni nani, na kazi zake ni zipi.” Sijasomea biashara na matangazo, kwa hiyo sina uhakika na uhalali wa kauli hiyo, lakini kwa uzoefu wangu katika uandishi, maneno haya yana maana zaidi kuliko Babu Tale anavyotaka watu waelewe.
Kama ningekuwa yeye, kwa maana ya kiongozi wa Diamond, ningependa kujua nini kilitokea na sababu za kutokea kwake. Mkataba wa awali ulimpasa kupanda jukwaani saa sita, kwa nini alikubali apandishwe saa kumi? Meneja unashangiliaje vurugu zilizosababishwa na msanii wako, ukiamini kwamba zinamtangaza? Mtu asiyejua kilichotokea anayemhitaji Diamond, hawezi kuamini kuwa haheshimu mikataba, ni mwenye kuchelewa kwenye shughuli hadi kusababisha maafa? Kama meneja anaamini msanii kutangazika vizuri kwa mambo mabaya, tunashindwa vipi kuamini kuwa wao ndiyo waratibu wa skendo za mara kwa mara zinazowakumba wasanii wao? Wasanii wetu kadiri wanavyokua kimuziki na kiakili, wanapaswa pia kuangalia aina ya watu wanaofanya nao kazi kulingana na levo waliyopo. Kama skendo zinamtangaza msanii, hiyo bado inaweza kuwa siri ya ndani, lakini mbele ya hadhara, ni lazima meneja asimame na kulaani kuwa kitendo kama vurugu kwenye shoo, kimemharibia sana msanii wake na atakuwa makini zaidi katika siku zijazo ili asifanye kazi na watu kama hao, angalau kwa kuzuga!
TIA COMMENT YAKO HAPO CHINI KUHUSU HILI JAMBO...
Utakua unapata Links za habari moja kwa moja kwenye mtandao wako wakiJamii
FACEBOOK- CLICK HERE
TWITTER- CLICK HERE
0 comments :
Post a Comment