.

.

SHOP HERE

News
Loading...

.

.

.

shop now

Nyalandu ajitosa urais

*Atangaza kugombea mwaka 2015
*Asema ni zamu ya vijana kuongoza
*Asisitiza safari moja huanzisha nyingine
Hillary Shoo, Singida
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ametangaza rasmi kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015.
Nyalandu ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, jana alitangaza nia hiyo ya kugombea urais mwaka 2015, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Ilongero wakati akihutubia mamia ya wananchi ikiwa ni mkutano mkuu wa jimbo wa jimbo hilo ambalo amekuwa mbunge kwa miaka 15.
“Huu ni wakati wa mabadiliko na fikra mpya katika kuivusha Tanzania kwenye maendeleo ya kasi na hilo litafanywa na vijana wenye uchungu na nia ya kuwatumikia watu. Naitazama siku mpya ambayo ndoto yangu itakamilika, Mungu atanyanyua vyombo na kushangaza wakubwa,” alisema Nyalandu
Alisema huu ni muda mwafaka wa vijana kuleta maono mapya na wakati wa kuleta maono mapya kwa ajili ya Watanzania wenzake. Hivyo basi, muda ukifika atachukua hatua za kwenda Dodoma kuchukua fomu ili agombee urais.
“Nina imani maelfu ya vijana na watu wa rika mbalimbali watanisindikiza ili kutimiza ndoto yangu ya kuwatumikia,” alisema.
Alitumia nafasi hiyo kusisitiza kila mwanachama wa CCM anapaswa kupimwa kwa utendaji wake wa kazi alizofanya na si vinginevyo.
“CCM tuna utaratibu, miiko na miongozo, hivyo nasubiri kwa hamu muda ufike ili niungane na wenzangu katika kuwania nafasi hii ya kuwaongoza Watanzania.
“Wale wote waliotangaza nia ndani ya chama chetu, kazi zao lazima zipimwe na zianikwe hadharani ili mwisho wa siku CCM yenyewe itazipima,” alisema Nyalandu.
Alisema pindi Rais Jakaya Kikwete atapohitimisha utawala wake, lazima atakabidhi kijiti kwa kizazi kipya.
“Nina uhakika Rais Kikwete, akiondoka madarakani, lazima akabidhi kijiti kwa kizazi chenye fikra. Zama za kusimama na kuchukua vijiti zimefika. Mwaka mwaka 2015, ndani ya CCM tunatarajia utakuwa mwaka wa mabadiliko na fikra mpya.
“Tuna wajibu wa kubadili fikra zetu, watu wasimamie Tanzania kuchukua hatua, licha ya ukweli kuwa, CCM tuna utaratibu na itikadi zetu, tumeondoa zuio kwa vijana wasiwe waoga. Tumejipanga kuwashangaza wengi,” alisema Nyalandu.
Wapinzani.
Waziri Nyalandu, alisema uamuzi wake utawashangaza wengi na kundi la kwanza litakuwa la wapinzani wakiwamo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Safari yangu ya miaka 15 katika ubunge wangu na siasa nimekutana na mengi. Mungu ametusaidia kusonga mbele kwa mafanikio makubwa na watu ninaowatumikia. Safari moja huanzisha nyingine na ninawaomba tuendelee kusoga mbele pamoja.
“Nilianzisha safari yangu ya kisiasa hapa na leo nipo hapa kuwaeleza dhamira yangu nyingine. Mlinipa jina la ‘Mwanyengu’ maana yake mtoto wa tai la kuishangaza dunia. Safari hii imekuwa ya milima na mabonde, kwa pamoja tumeweza, Mungu ameona, Kikwete ameona sawasawa,” alisema Nyalandu.
Aliongeza, anaitazama nchi hii kwa dhati kabisa inahitaji kubadilika kama nyingine zilizopiga hatua, Rais Kikwete amesimama kama jemedali, shujaa, mpambanaji na hapa alipofika lazima apongezwe.
Alisema anatambua atapitia kwenye ushindani mkubwa ndani ya chama chake ambao utatoa mtu mmoja wa kupeperusha bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Nawaambia wale wote wanaoogopa kushindanishwa ni waoga, siku, saa, mwezi na hata mwaka utakapofika chini ya Kikwete, wachukua fomu na kupeleka kazi zao ili zipimwe,” aliongeza.
Viongozi wenzake
Nyalandu alisema ni muhimu na haki kwa viongozi wote wastaafu waliotawala taifa hili wanapaswa kupewa heshima zote.
“Hawa wazee wetu ni muhimu na japo wapo nje, lakini wanaendelea kuongoza kwa mawazo na ushauri, ni lazima tuwaenzi na kuwaheshimu. Wana haki ya kuheshimiwa, lakini zamu ya vijana imefika.
“Vijana tunataka taifa litakaloleta siku njema, ni wajibu wetu tuwatunze ndiyo maana kupitia kwao, maisha yetu yamebadilika,” alisema.
Licha ya kutangaza nia hiyo, Nyalandu alisema bado ataendelea kuwapenda wananchi wa jimbo lake.
Achangia mamilioni
Mara baada ya kuwasili katika Kijiji cha Ilongero, Nyalandu alikwenda katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Ilongero ambako alishiriki misa na kuahidi kuchangia sh. milioni 10, kwa ajili ya ujenzi wa kanisa.
Pia, alitembelea Kanisa la FPTC-Tanzania ambako nako alitoa msaada wa sh. milioni 10 na kiasi kama hicho alitoa kwenye Msikiti waIjumaa.
Nyalandu aliambatana na mke wake, Faraja Kota, watoto wake Christopher na Serafine na wazazi wake.
Source: JamboLeo
Share on Google Plus

About feisal pinto

Computer Application Student, Author, Short Stories Writer, Business Proposal Writer, Presenter and Application Builder. Email feisalpinto4@gmail.com for complains and business only.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment

ad