.

.

SHOP HERE

News
Loading...

.

.

.

shop now

Sumaye: Rais ajaye awe mzalendo


*Atumia Biblia kukemea rushwa, ufisadi
Mwandishi Wetu, Mbeya
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema rais ajaye lazima awe mzalendo kwa nchi na wananchi wake.
Pia, alisema Watanzania wanahitaji kupata kiongozi mzalendo wa kweli ambaye atajali maslahi ya umma kwanza, kabla ya kitu chochote.
Alisisitiza kwa bahati mbaya hivi sasa watu wanaanza kuthamini maslahi binafsi na hilo limewakumba viongozi wengi wa umma hadi wanasiasa, huku akifafanua upotevu wa uzalendo wa kweli husababisha hasara nyingi kwa mali za nchi hasa mali asili.
Sumaye alitoa kauli hiyo jana mjini hapa wakati wa uzinduzi wa tamasha la uimbaji na kuliombea taifa amani, ambapo alisema Watanzania wawe makini katika kuchagua viongozi wao wa ngazi mbalimbali, ikiwemo ya urais.
“Uzalendo una tafsiri pana. Mzalendo wa kweli ni mkweli kwa nchi yake, ni mpenzi wa nchi yake na watu wake, husimamia haki na hujali maslahi ya umma, badala ya maslahi yake binafsi,” alisema.
Sumaye alisema Watanzania wanahitaji kupata kiongozi mzalendo wa kweli ambaye atajali maslahi ya umma kwanza, kabla ya kitu chochote.
Alisisitiza kiongozi mzalendo atajali hali ya nchi yake kwa leo na baadaye, na atapenda kuilea na kuitunza Tanzania ili iweze kulea vizazi vinavyokuja baadaye kwa kujali tabianchi na kuzuia au kupunguza madhara yanayotokana na mabadiliko hayo.
“Kiongozi mzalendo atajenga heshima ya nchi ili Tanzania iwe na sifa mbele ya uso wa dunia. Kiongozi mzalendo atapenda kuwainua Watanzania wote kwa kadri inavyowezekana ili wawe na maisha bora, badala ya kulenga kundi dogo ambalo labda yeye ana maslahi nalo,” alisema.
Alisema katika uchaguzi mkuu mwakani, Watanzania wanayo nafasi ya kiongozi wa aina hiyo na wanayo nafasi ya kuwaweka viongozi katika ngazi nyingine ambao nao watakuwa na sifa hizo.
Alisema kukosekana kwa uzalendo kumesababisha mauaji ya wanyama wetu, utoroshaji wa rasilimali zetu, uharibifu wa misitu yetu, mikataba isiyo na faida kwa wananchi wetu.”Vyote hivi ni matunda ya watu kukosa uzalendo wa dhati.”
Alisema watu huangalia zaidi kujitajirisha hata kama ni kwa gharama kubwa kwa nchi na taifa la baadaye.
“Hili ni jambo la hatari sana kwa amani ya nchi, likiachiwa kuota mizizi, hivyo ni vema kiongozi tutakayemtafuta mwakani awe mzalendo wa dhati adhibiti hali hiyo,” alisema.
Pia, alisema rais ajaye lazima awe mwenye upeo wa kufahamu nchi na kuielewa na kubwa zaidi aelewe vyema na kuyaelewa matatizo ya watanzania kwa dhati na matatatizo hayo yawe yanagusa moyoni mwake.
Alisema kiongozi huyo lazima aelewe Watanzania wanataka nini, yeye anataka kutupeleka wapi na anatufikishaje huko. “Asiwe kiongozi wa kutuburuza anavyotaka yeye au kiongozi asiyejali yanayotupata ambayo yana maumivu kwetu.
“Tunataka kiongozi anayeelewa mipango ya taifa na kuifuata kama ilivyopangwa, si kubuni mipango mipya kila kukicha wakati mipango ya awali haijatekelezwa,” alisema Sumaye.
Utawala washeria
Sumaye alisema nchi yetu ni ya demokrasia ya vyama vingi inayotawaliwa kwa kufuata misingi ya katiba na sheria zilizowekwa.
Alisema nchi nyingi zimejikuta katika machafuko kwa sababu kiongozi wake wakati mwingine huweka Katiba na sheria kando na kutawala kwa imla kadri yeye anavyoona inafaa.
“Tunahitaji kupata kiongozi atakayeheshimu katiba ya nchi na sheria mbalimbali zinazowekwa mara kwa mara kwa maslahi ya umma,” alisema.
Alisema kiongozi lazima awe tayari kuilinda na kuikuza demokrasia ya vyama vingi ambayo imeanzishwa kwa maslahi ya wananchi.
Umaskini
Sumaye alisema umaskini hilo ni tatizo ndiyo mama wa matatizo mengi nchini mwetu na vijana ndiyo waathirika wakubwa wa janga hilo. Kimsingi, Watanzania ni maskini, lakini nchi yao si maskini na ina rasilimali nyingi zikiwemo rasilimali watu, ardhi, maliasili na fursa nyingine.
“Rasilimali hizo kama hazitatumika ipasavyo hazitaondoa umasikini. Wataalamu wa uchumi wanatuambia nchi kuwa na rasilimali nyingi si lazima ilete utajiri nchini,” alisema.
Alisema ili kupambana na umaskini, kuna mambo ambayo lazima yafanyike. Kwanza ni lazima kuwahimiza kila Mtanzania mwenye uwezo wa kufanya kazi afanye kazi kwa bidii zote. Lazima apige vita unyonyaji wa aina yoyote katika jamii yetu.
“Kila mtu afanye kazi na afanye kazi kwa bidii na kusiwe na hiyari katika kufanya kazi. Jambo la pili ni uaminifu katika kazi hasa wale watakaofanya kazi katika sekta ya umma na sekta binafsi kwa maana ya ajira,” alisema.
Aliongeza, kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya Watanzania kumesababisha waajiri wengi kutafuta wafanyakazi nje ya mipaka yetu.
Pia, jambo la tatu ni lazima yajengwe mazingira ya nchi na watu wake kufaidika zaidi na jasho lao, kuliko jasho la Watanzania kufaidi zaidi watu wa nje.
Ajira
Katika hilo, Sumaye alisema tatizo hilo lina uhusiano wa karibu na umaskini na waathirika wakubwa wa tatizo hilo ni vijana.
“Sote ni mashahidi wa jinsi vijana wetu wanavyohangaika mitaani kusaka ajira zisizokuwepo au kufanya vijibiashara visivyokidhi mahitaji muhimu ya maisha.
“Mahangaiko yote yanawakumba vijana wa makundi yote, wasiosoma, waliopata elimu kidogo na hata wasomi wa kubobea,” alisema Sumaye.
Alisema wapo vijana ambao wamepata elimu ambayo haitoshelezi kuwafanya waajiriwe, lakini wapo waliosoma vizuri hadi vyuo vya elimu ya juu na vyuo vikuu, lakini pia hawana kazi au wanafanya kazi ambazo si walizosomea.
“Kwa maana nyingine, haya ni matumizi mabaya ya vipaji tulivyovijenga kwa muda mrefu na kwa gharama kubwa,” alisema Sumaye.
Alisema tunahitaji kiongozi anayetambua hilo na kuwa na jawabu la tatizo hilo, angalau vijana waone kuna matumaini mbele na kuna fursa zinazojengeka kwamba, huko mbele ya safari ukubwa wa tatizo hilo utapungua na wengi wataondokana na kukata tamaa na kuwa na matumaini na nchi yao.
Rushwa:
Sumaye alisema katika vitabu vyote vitakatifu rushwa za aina zote zimetamkwa kuwa ni dhambi, tena dhambi inayopofusha macho ya wanaoona. Rushwa yoyote ni adui wa haki.
Alisema rushwa imechangia wananchi kukosa haki zao na wakati mwingine kununua huduma ndani ya jamii yao, licha ya kwamba wanatakiwa waipate bure.
“Rushwa huumiza wananchi wa kawaida na ni chanzo kikubwa cha malalamiko na manung’uniko ya wananchi dhidi ya Serikali yao,” alisema Sumaye.
Alisema mifano ni mingi katika taasisi na idara za umma zinazotoa huduma. Kwa mfano, kama ni mahakamani, mhalifu anaweza akapewa haki na yule aliyestahili haki si tu hupokonywa haki yake bali pia hubebeshwa adhabu aliyostahili yule mkosaji.
Alisema rushwa imeathiri hadi mfumo wa kupata viongozi wa nchi, ambapo baadhi yao wamekuwa wakihonga wapiga kura ili wachaguliwe. Hiyo ni hatari kubwa kwa nchi na lazima wananchi waichukie.
“Ninapozungumzia aina hizi za rushwa, natoa tu tahadhari kwa umma na simlengi wala simvai mtu yeyote. Nazungumzia tabia hizi mbaya ambazo nina uhakika zipo katika jamii yetu na kwa baadhi yetu.
“Lengo ni kurekebisha wenye tabia hii waache tabia hizi za hatari na kama hawataacha, basi ni kuuelimisha umma uwaadhibu kwa kuwanyima kura kwa tabia zao mbaya,” alisema.
Ufisadi.
Kwa upande wa ufisadi, Sumaye alisema hilo lina uhusiano wa karibu na rushwa kubwa au rushwa ulafi. Tofauti hapo ni si lazima fedha au chochote cha kushawishi kitumike, japo madhara yake yanafanana na ya rushwa ulafi.
“Mfano wa ufisadi ni kama waziri au kiongozi yeyote, kwa mfano, zabuni ikitangazwa wizarani kwake kushindanisha waombaji na yeye kwa kutumia nafasi yake, huamua zabuni hiyo ipewe kampuni ya mtoto wake hata kama kwa vigezo ameshindwa na waombaji wengine,” alifafanua.
Dawa za kulevya
Sumaye alisema hilo ni tatizo ambalo haliwezi kufumbiwa macho, biashara ya dawa ya kulevya hufanywa na watu wazito au kwa fedha zao au kwa madaraka yao.
“Hivi sasa nchi yetu inaonekana inakuwa kituo muhimu cha kupitishia dawa hizi kwenda nchi nyingine na kutoka nchi nyingine,”alisema.
Source: JamboLeo
Share on Google Plus

About feisal pinto

Computer Application Student, Author, Short Stories Writer, Business Proposal Writer, Presenter and Application Builder. Email feisalpinto4@gmail.com for complains and business only.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment

ad