STRAIKA wa zamani wa Yanga, Idd Moshi ‘Mnyamwezi’, ametamka neno ambalo halitafurahiwa na Mrisho Ngassa pamoja na mashabiki wake juu ya kwenda kucheza soka la kulipwa Afrika Kusini. Moshi, aliyewahi kutamba pia na Milambo ya Tabora, alisema kuwa winga huyo wa zamani wa Yanga, amechelewa mno kwenda kucheza Afrika Kusini kwani hatadumu muda mrefu tofauti na kama angekwenda mapema.
Moshi alisema: “Ngassa angeweza kwenda Afrika Kusini au Ulaya siku nyingi tu zilizopita, ingawa amepata nafasi lakini hawezi kudumu kipindi kirefu kwani umri wake umeenda sana hivyo kwa kifupi ni kama amechemsha kwa kiasi fulani.
“Tatizo letu sisi Watanzania huwa hatutaki kujaribu vitu kipindi ambacho tunahitajika. Tunajaribu pale tu tunapoona kuwa mambo yanaonekana kufika mwisho, hili lilitakiwa kuangaliwa mapema na wachezaji kama Ngassa.
“Nafasi aliyoipata ni sehemu tu ya bahati yake kisoka, hivyo anatakiwa acheze kwa nidhamu ya hali ya juu ili aweze kufungulia milango wachezaji wengine wa Kitanzania kwenda kucheza Afrika Kusini na nchi zingine.”
Ngassa ambaye tayari yupo Afrika Kusini, amesajiliwa kwa mkataba wa miaka minne kuichezea Free State Stars inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini baada ya kumaliza mkabata wake Yanga hivi karibuni.
Source: Mwanaspoti
0 comments :
Post a Comment