Msanii mkongwe wa muziki wa kizazi kipya, Ambwene Yesaya 'AY', amesema woga unawakwamisha wasanii wengi kupiga hatua kimuziki.
Mkali huyo wa mashairi alisema kuwa wasanii wengi wamekuwa waoga wa kuuliza mambo wasiyoyajua na wengine hudhani kuwa wanajua mengi kuliko waliowatangulia.
Msanii huyo ambaye pia hujulikana kama 'Mzee wa Commercial', alisema wasanii hususan wa muziki wa kizazi kipya wanatakiwa kuuliza na kufuatilia malengo kwa kuwa muziki ni biashara.
Katika mahojiano na kituo cha EATV wiki iliyopita, alisema njia peke itakayoweza kuwasaidia wasanii wenzake kufanya kazi kwa kushirikiana ili waweze kutoka hatua moja kwenye nyingine.
"Wasanii tusiwe waoga kuuliza na kufuatilia yanayohusu tasnia ya muziki ili tuweze kufikia malengo kwa sababu muziki ni biashara," alisema 'Mzee wa Commercial'.
Alisema muziki kwake una faida na hafikiri kutoka katika tasnia hiyo kwa kuwa ameufanya kwa muda mrefu.
"Kufanya biashara na kuwa mfanyabiashara mkubwa ni ndoto yangu na muziki na umiliki wa vipindi haunipi changamoto sana, ninafanya kazi na wasomi, wanaojielewa na kazi zao haziingiliani na kazi yangu ya muziki," alisema.
0 comments :
Post a Comment