
Na Khatimu Naheka
KIUNGO wa Yanga, Haruna Niyonzima, amepatwa na tatizo kubwa baada ya nyumba yake kuungua moto jana asubuhi.

Niyonzima
ambaye ni raia wa Rwanda, amejikuta katika wakati mgumu baada ya nyumba
yake hiyo iliyopo eneo la Magomeni Makuti jijini Dar kuwaka moto ambao
ulianza majira ya saa moja asubuhi na kuteketeza vitu vyote vilivyokuwa
sebuleni.

Mara
baada ya kupata taarifa hizo, Championi Ijumaa lilifika katika eneo la
tukio na kumkuta Niyonzima akiwa na majirani zake na mkewe, Nailah,
wakiwa katika hali ya majonzi huku vitu ambavyo viliteketea na moto
yakiwemo masofa, televisheni aina ya ‘flat screen’ vikiwa nje,
vikionekana havitaweza kutumika tena kutokana na kuathiriwa na moto kwa
asilimia 90.

Akizungumza
na Championi Ijumaa, Niyonzima alisema wakati moto huo ukianza, hakuwa
anajua lolote, ambapo majirani zake ndiyo walioanza kuuona na kuamua
kumuamsha, lakini tayari ulikuwa umeshateketeza karibu vitu vyote
vilivyokuwa sebuleni, zikiwemo kompyuta zake mbili za ‘laptop’, ingawa
walifanikiwa kuudhibiti kwa kutoingia katika vyumba vingine.

“Sebuleni
hakuna tulichofanikiwa kuokoa, kila kitu kimeteketea na moto, kama
mngekuta wakati unawaka, palikuwa hapapitiki kutokana na moto mkubwa
ulioambatana na moshi mwingi, nashukuru hakuna aliyeumia zaidi ya hivi
vitu vilivyoteketea.

“Nawashukuru
sana majirani zangu, leo nimejua umuhimu wa kuishi vizuri na watu,
niseme ukweli wamenisaidia sana katika kuudhibiti moto, kama isingekuwa
wao, nisingeweza kufanya hivyo nikiwa mimi na mke wangu peke yetu, moto
ulikuwa mkubwa sana,” alisema Niyonzima.

Aliongeza
kuwa, bado hajajua hasara iliyopatikana na moto huo, ambapo sasa
wanatafuta chanzo cha tatizo hilo, ingawa kwa haraka hali inaonyesha ni
kutokana na hitilafu ya umeme.
0 comments :
Post a Comment