MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi, Nguza Viking maarufu kama Babu Seya na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ pamoja na ndugu zao, Jumatano iliyopita walitoka kwa vicheko katika Mahakama ya Rufaa Tanzania baada ya kuridhishwa na utetezi uliotolewa na wakili wao, Mabere Marando, anayepinga hukumu ya kifungo cha maisha jela, waliyopewa wanamuziki hao.
Mbele ya majaji watatu wa Mahakama hiyo, Marando alikabiliana na timu ya mawakili watano waandamizi wa serikali ambao ni Jackson Brashi, Angaza Mwaipopo, Imaculate Banzi, Joseph Pande na Apimark Mabruk.
Miongoni mwa hoja ambazo Marando alionekana kuwabana mawakili wa serikali ni jinsi Jamhuri ilivyowatia hatiani wateja wake kwa kutumia ushahidi uliotolewa na watoto katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar, akisema zipo taratibu za kuchukua katika ushahidi kwa mtoto ikiwemo kurekodiwa, jambo ambalo halikufanyika.
Hata hivyo, jopo la mawakili wa Jamhuri licha ya kukumbana na wakati mgumu kutoka kwa wakili Marando, liliendelea kusisitiza kuwa hukumu iliyotolewa dhidi ya washitakiwa hao ilikuwa sahihi.
Baada ya mawakili hao kusisitiza hivyo Marando alipewa nafasi nyingine ya kutoa utetezi wake, ambapo aliendelea kufafanua makosa mbalimbali yaliyofanyika kuwahukumu wateja wake kwa kutaja vifungu vya sheria ambavyo vilionekana kama kuwasafishia njia wateja wake hao hali iliyozua tabasamu na vicheko mahakamani hapo.
0 comments :
Post a Comment