KIPA wa Yanga, Juma Kaseja, juziJumatatu alifanya mazoezi na
makipa wa timu ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars katika Uwanja
wa Karume, uliopo Ilala jijini Dar es Salaam.
Kaseja alijiunga na makipa hao mara baada ya
kumalizika mazoezi ya klabu yake ya asubuhi yaliyofanyika pia uwanjani
hapo kuanzia saa moja mpaka saa tatu.
Tukio la yeye kuamua kuendelea na mazoezi
akiungana na makipa hao wa Twiga Stars; Fatma Omari, Maimuna Saidi na
Najiath Abbas kwa kiasi kikubwa liliibua mjadala kwa mashabiki wa soka
waliokuwapo uwanjani hapo.
Kocha wa makipa wa Twiga Stars, Eliutheri Mholeli,
alisema Kaseja aliungana nao baada ya kuvutiwa na mazoezi aliyokuwa
akiwapa makipa wake.
“Alivutiwa na tulichokuwa tunafanya, akaomba
ajiunge nasi. Sikuona ubaya kwa vile haya ni mazoezi. Alichofanya pia
kimewaongezea hamasa makipa wangu, ni kutokana na uzoefu wake,” alisema
Mholeli ambaye pia ni kipa wa Bandari.
Makipa hao wa Twiga Stars walionekana kumtazama
kwa makini Kaseja katika kila hatua ili kujipatia uzoefu na walifanya
mazoezi kwa nguvu bila kuonyesha tofauti yoyote na yeye.
Kaseja anasifika kwa kujituma mazoezini akiwa na timu tofauti katika miaka zaidi ya kumi sasa.
0 comments :
Post a Comment