GENEVA, Uswisi
RAIS wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa), Sepp Blatter ataachia ngazi ifikapo Desemba 16, mwaka huu ambapo utafanyika mkutano mkuu wa dharura na kufanyika uchaguzi kumpata mrithi wake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Fifa juzi, Blatter ataachia ngazi Desemba 16, mwaka huu baada ya awali kutangaza kujiuzulu kutokana na kuhisi kutoungwa mkono na baadhi wanachama kutokana na tuhuma za ruishwa na ubadhirifu zilizolikumba shirikisho hilo.
Blatter alitangaza kujiuzulu wadhifa wake, Juni 2 mwaka huu ikiwa ni siku nne tangu kuchaguliwa tena kuliongoza shirikisho hilo kwa msimu wa tano.
Fifa imesema wajumbe kutoka nchi wanachama wake wote 209 wataalikwa Uswisi kwa ajili ya uchaguzi wa Rais mpya wa shirikisho hilo.
Uamuzi wa mwisho kuhusu tarehe ipi utafanyika uchaguzi itajulikana Julai, mwaka huu ambapo kamati kuu ya Fifa inatarajiwa kukutana.
Wakati huohuo, zabuni ya kuandaa Kombe la Dunia 2026 imeahirishwa kufuatia madai ya hongo katika utoaji nafasi hiyo kwa mwaka 2018 na 2022.
Katibu mkuu wa shirikisho hilo, Jerome Valcke amesema kuwa ni 'ujinga' kuanza mpango huo katika mazingira yaliopo.
Upigaji kura kumtafuta atakayeandaa kombe la dunia mwaka 2016 unatarajiwa kufanyika mjini Kuala Lumpur, Malaysia Mei 2017.
Marekani inaongoza kutaka kuandaa michuano hiyo lakini Canada,Mexico na Colombia nazo zimewasilisha maombi .
Nchi za Urusi na Qatar zilichaguliwa kuandaa michuano ya Kombe la Dunia 2018 na 2022 kwa kura ya siri iliyopigwa na wanachama wakuu wa Fifa 22 Desemba 2010.
Kwa sasa viongozi wa mashtaka nchini Uswisi na Marekani wanachunguza madai ya rushwa na kuzunguka zabuni hizo.
0 comments :
Post a Comment