MARA kipyenga kinapulizwa, Arsenal dhidi ya Real Madrid kwenye mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hakuna ujanja, vinara hao wa Ligi Kuu England
ikiwakwepa wababe hao wa Santiago Bernabeu, inaweza kuangukia kwenye
midomo ya vigogo wengine hatari zaidi, PSG, Bayern Munich, Atletico
Madrid au Barcelona.
Yote hayo yatafahamika leo, Jumatatu mjini Nyon,
Uswisi wakati upangaji wa timu zitakazochuana kwenye hatua ya 16 bora ya
Ligi ya Mabingwa Ulaya itakapofanyika.
Arsenal imeshika nafasi ya pili kwenye kundi lake,
jambo linalowaweka kwenye hatari ya kukumbana na moja ya vigogo hivyo
vilivyoongoza makundi yao.
Timu ambazo Arsenal inayonolewa na Mfaransa Arsene
Wenger haitakumbana nazo kwenye hatua hiyo ya 16 bora ni ni Manchester
United, Chelsea kwa kuwa ni za kutoka England na Borussia Dortmund kwa
kuwa zilikuwa kwenye kundi moja.
Hii ni mara ya 14 kwa Arsenal kuvuka hatua ya
makundi ya michuano hiyo, lakini kichapo cha Jumatano iliyopita dhidi ya
SSC Napoli kimewaweka pabaya.
Baada ya michuano hiyo kufika hatua ya mtoano,
akili za mashabiki wengi wa soka zinasubiri kufahamu nani atamkabili
nani kwenye michuano hiyo baada ya droo yake ya makundi itakayofanyika
mjini Nyon.
Timu zilizofuzu
Timu 16 zimeingia kwenye hatua ya mtoano, ambapo timu nane zilizoongoza makundi na nane nyingine zilizomaliza nafasi ya pili.
Wababe waliongoza makundi ni Manchester United,
Real Madrid, Paris Saint-Germain, Bayern Munich, Chelsea, Borussia
Dortmund, Atletico Madrid na Barcelona, wakati walioshika nafasi ya pili
ni Bayer Leverkusen, Galatasaray, Olympiacos, Manchester City, Arsenal,
Schalke 04, Zenit St Petersburg na AC Milan.
Ujerumani imeingiza timu nne sawa na England,
hivyo kuna kila dalili timu hizo zikapangwa kumenyana hatua hiyo ya
mtoano, huku Man City ikiwa na uhakika wa kuikwepa Bayern Munich kwenye
mtoano kutokana na kupangwa kundi moja.
Timu nyingine ambazo Manuel Pellegrini na kikosi
chake cha Man City inaweza kukumbana nazo ni Barcelona, Real Madrid,
Atletico Madrid, PSG na Borussia Dortmund, sawa na Arsenal ambayo kwenye
orodha ya timu hizo ni Dortmund tu ambazo hatamenyana nayo kwenye
mtoano wa 16 bora.
Nani kupangwa na nani?
Mabingwa saba wa zamani watachuana, ikiwamo
waliotinga fainali msimu uliopita na kuchapwa, Borussia Dortmund. Italia
imeingiza timu moja, AC Milan baada ya klabu mbili, Juventus na Napoli
kushindwa kupenya hatua ya makundi.
Wakati mechi hizo za mtoano zikisubiri hadi
Februari 18/19 na Februari 25/26 mwakani licha ya droo yake kufanyika
leo Jumatatu, wengi wanasubiri kutaka kujua nani atakwaana na nani
kwenye hatua hiyo. Kwenye karatasi, Arsenal na Man City zinaonekana kuwa
zipo kwenye mtihani mgumu wakati Chelsea na Manchester United zikitajwa
kwamba zitakuwa na mchekea kwenye hatua hiyo kutokana na kuongoza
makundi yao.
Kwa klabu za England, wakati Arsenal ikiwa kwenye
hatari ya kukutana na Real Madrid, Paris Saint Germain, Bayern Munich,
Atletico Madrid na Barcelona, Chelsea wao wanaweza kumenyana na Bayer
Leverkusen, Galatasaray, Olympiakos, Zenit St Petersburg, AC Milan sawa
na Manchester United, droo ambayo kwenye karatasi inaonekana kuwa
nyepesi.
Kitu cha kuvutia
Jose Mourinho na kikosi chake cha Chelsea anaweza
kukumbana na nyota wake wa zamani straika Didier Drogba anayekipiga
Galatasaray.
Drogba, ndiye aliyeipa Chelsea taji lake la kwanza
la Ligi ya Mabingwa baada ya kufunga kwa mkwaju wa penalti katika
fainali dhidi ya Bayern Munich mwaka 2012. Na baada ya kuwa na Chelsea
kwa miaka minane ikiwa pia kuwa chini Mourinho, Drogba anaweza kuwa mtu
hatari kama atapangwa kukumbana na klabu yake hiyo ya zamani kitu
ambacho kocha huyo Mreno anapenda kitokee.
Arsenal inaweza kupangwa dhidi ya Bayern Munich,
iliyozima ndoto zao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita licha
ya kikosi hicho cha Wenger kushinda 2-0 kwenye Uwanja wa Allianz Arena
Machi mwaka huu.
Lakini, pia wanaweza kupangwa dhidi ya Real Madrid
ambapo kitendo hicho kitamfanya nyota mpya wa Washika Bunduki hao wa
London, Mesut Ozil kukutana na waajiri wake wa zamani baada ya kuwahama
mwaka huu.
Kitu kingine ni Wenger kumvaa Pep Guardiola, mtu
ambaye alipokuwa na kikosi cha Barcelona alimtambia mara kadhaa Mfaransa
huyo. Wengi walitaka kuona Barcelona na Bayern Munich zikimenyana
katika hatua hiyo ya 16, lakini sasa hilo haliwezekani kwa kuwa timu
zote zilimaliza vinara kwenye makundi yao, sawa na Mourinho kwamba
hatarejea Bernabeu kwenye hatua hiyo.
Vita ya mastaa watupu
Licha ya kwamba mtoano huo utakosa kushuhudia
ujuzi wa mastaa kadhaa kwenye soka akiwamo Douglas Costa, Antoine
Griezmann, Andrea Pirlo, Arturo Vidal, Oscar Cardozo, Mohamed Salah,
Gonzalo Higuain, Jackson Martinez na Viktor Fischer, bado kuna majina
makubwa ya wachezaji na vipaji vya kuvutia vitaendelea kuwamo kwenye
mtoano huo wa 16 bora.
Nyota wote watatu wanaowania tuzo ya Fifa ya Mwanasoka Bora wa
Mwaka (Fifa Ballon d’Or), Lionel Messi (Barcelona), Cristiano Ronaldo
(Real Madrid) na Franck Ribery (Bayern Munich) watakuwamo kwenye hatua
hiyo.
Wengine, Robin van Persie, Shinji Kagawa na Wayne
Rooney wataiongoza Manchester United, wakati Real Madrid itakuwa pia na
Gareth Bale na Isco kwenye kikosi chake, huku Galatasaray ikiwa na
wakongwe Drogba na Wesley Sneijder, Paris Saint-Germain itakuwa na
Zlatan Ibrahimovic na Thiago Silva, wakati Olympiakos itakuwa na fowadi
wake hatari Kostas Mitroglou.
Mastaa hao pia kutakuwa na Arjen Robben (Bayern
Munich), Sergio Aguero (Man City), Eden Hazard na Frank Lampard
(Chelsea), Julian Draxler (Schalke), Robert Lewandowski na Marco Reus
(Borussia Dortmund), Mesut Ozil (Arsenal), Diego Costa (Atletico
Madrid), Neymar na Andres Iniesta (Barcelona) na Mario Balotelli na Kaka
(AC Milan).
Mechi zitakavyochezwa
Kuanzia hatua ya 16 bora hadi nusu fainali, klabu
zitacheza mechi mbili dhidi ya mwenzake, nyumbani na ugenini kwa sheria
zilezile mechi za mtoano.
Mechi za kwanza za hatua ya mtoano ya 16 bora
zitachezwa Februari 18, 19, 25 na 26, wakati za marudiano zitafanyika
Machi 11, 12, 18 na 19.
Robo fainali itafanyika Aprili 1 na 2 na zile za
marudiano zitafanyika Aprili 8 na 9 mwakani, wakati nusu fainali mechi
za kwanza zitafanyika Aprili 22 na 23 na timu zitarudiana Aprili 29 na
30.
Fainali itakuwa mchezo mmoja tu, utakaofanyika
kwenye Uwanja wa Estadio do Sport Lisboa e Benfica nchini Ureno,
Jumamosi ya Mei 24 mwakani.
0 comments :
Post a Comment