.

.

SHOP HERE

News
Loading...

.

.

.

shop now

Rais Kikwete afichua siri kuhusu Mandela.........


JK_5ea4e.jpg
Na Neville Meena, Mwananchi
Qunu: Rais Jakaya Kikwete jana aliyateka mazishi ya Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, alipotoa salamu mbele ya maelfu ya waombolezaji na wageni wa kimataifa walioshiriki katika mazishi hayo.
Rais Kikwete aliweka bayana jinsi Tanzania ilivyoshiriki katika vita ya ukombozi si kwa Afrika Kusini pekee bali kwa nchi nyingi za Kusini mwa Afrika zikiwamo Angola, Msumbiji, Zimbabwe na Namibia (EL)

Kadhalika alizungumzia jinsi wapigania uhuru wa ANC walivyoweka kambi zao na kufungua ofisi za chama hicho nchini Tanzania ambako walipewa makazi na vifaa, maelezo ambayo yalishangiliwa na umati wa watu uliohudhuria.
"Kwa hakika ANC walipata makazi mapya Tanzania ambayo waliyatumia kuendesha mambo yao, kujipanga na kuendeleza vita ya ukombozi. Kutoka Tanzania ANC waliweza kuwafikia makada wake na wanachama waliobaki Afrika Kusini kwa kutumia mawasiliano ya siri," alisema Kikwete na kuongeza:
"Kimsingi Serikali ya Tanzania ililazimika kuanzisha redio maalumu kwa ajili ya vita ya ukombozi ambayo ANC waliitumia kupaza sauti ambazo walikuwa wamenyimwa na utawala wa ubaguzi wa rangi."
Rais Kikwete aliyekuwa na kazi ya kumwelezea Mandela kama mpigania uhuru, alieleza jinsi Mandela alivyofika Tanzania Januari 1962 bila kuwa na hati ya kusafiria na kwamba katika mazungumzo yake na Hayati Mwalimu Nyerere alieleza mpango wa kudai uhuru kwa njia ya mapambano.
"Mwalimu Nyerere alikuwa na maoni tofauti kuhusu mpango wa kuendesha mapambano kwa kutumia silaha, lakini baadaye walikubaliana na Tanzania ilikubali kuanzishwa kwa kundi hilo na mwalimu (Nyerere) aliwapa sehemu ya kuendeshea shughuli zao na vifaa," alisema Kikwete na kuongeza:
"Kwa hiyo, kwa wale walioshiriki katika vita vya ukombozi na askari wa MK (Jeshi la ANC), majina kama Kongwa, Mgagao, Mazimbu na Dakawa hayawezi kuwa mageni na pengine mtakumbuka enzi zile maisha yalivyokuwa."
Kikwete alisema wakati akiwa Tanzania, Mandela alikuwa akiishi kwa aliyekuwa Kada wa TANU, Marehemu Nsilo Swai na kwamba baada ya kusaidiwa kupata nyaraka za kusafiria kwenda Nigeria, Morocco na Ethiopia, aliacha buti zake nyumbani kwa mzee huyo.
"Familia hii iliendelea kutunza buti hizo wakitaraji kwamba Mandela atarudi, lakini wakati anatoka katika safari yake hakupita tena Tanzania na kwa bahati mbaya alipofika Afrika Kusini alikamatwa na kufungwa," alisema Kikwete katika hotuba iliyorushwa na vituo vyote vya televisheni vya kimataifa.
Aliongeza: "1995 ikiwa mwaka mmoja tangu Mzee Mandela aingie madarakani, viatu vile vililetwa na mjane wa marehemu Swai, Vicky Nsilo Swai ambaye nimekuja naye leo ili ashirikiane nanyi katika msiba huu ninyi mlio ndugu zake."
Alisema vita ya ukombozi haikuwa rahisi kwani wakati mwingine Tanzania mbali na kuwasaidia wapigania uhuru hati za kusafiria, ililazimika pia kuwapa majina ya bandia ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri.
Alimtania Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki akimuuliza iwapo alirejesha hati yake ya kusafiria na kusababisha waombolezaji kuangua kicheko. "Sifahamu kama Thabo amerejesha ya kwake," alisema.
Alisema kwa kuzingatia mazingira hayo, uhusiano baina ya Tanzani na Afrika Kusini si wa bahati mbaya kwani umejengwa katika mizizi ambayo ilistawishwa na Hayati Mwalimu Nyerere na Mzee Mandela.
"Huzuni yenu, ni huzuni yetu na majonzi yenu ni majonzi yetu pia maana kama alivyo kwenu Mandela kwetu alikuwa kiongozi, baba na mfano wa kuigwa," alisema Rais Kikwete huku akimtambulisha Mama Maria Nyerere katika ibada hiyo.
Alisema baada ya kutoka gerezani, Mandela alifika Tanzania ambako alipokewa na umati mkubwa wa watu katika rekodi ambayo haijawahi kuvunjwa na ujio wa kiongozi mwingine yoyote.
Katika hatua nyingine, Rais mstaafu wa Zambia, Kenneth Kaunda jana aliuchekesha umati wa waombolezaji pale alipokwenda kwa kukimbia wakati alipoitwa jukwaani kwa ajili ya kutoa shukrani.
Kaunda pia alisababisha watu kuangua kicheko pale alipomwita Kikwete kuwa "bwana mdogo" wakati alipokuwa akianza mazungumzo yake. "Waheshimiwa marais, akiwamo huyo bwana mdogo kutoka Tanzania......," alisema Kaunda.
Viongozi wengine
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambaye ni Rais wa Malawi, Joyce Banda alisema Afrika Kusini wanapaswa kuhakikisha kwamba wanaendelea kuwa wamoja kama Mandela alivyowaacha.
Katika hotuba yake alipongeza kile ambacho alikiita ushirikiano wakati wa msiba baina ya Mjane wa Mandela, Graca Machel na Mtalaka wake, Winnie Medikizela.
"Wanawake barani Afrika tumeguswa sana na jinsi Winnie na Graca walivyoshirikiana. Kwa Mama Graca asante sana kwa mapenzi na matunzo uliyompa Madiba wakati wa siku zake za mwisho," alisema Banda. Alisema Mandela alikuwa kiongozi ambaye aliandika historia njema kwa kujenga demokrasia ambayo imeibadili dunia.
"Mimi nilijifunza kwake kwamba ukiwa kiongozi unapaswa kuwapenda watu ili na wao wakupende, kwa hakika nyayo zake ndizo zimeniwezesha mimi kuwa Rais wa kwanza mwanamke katika ukanda huu (SADC)," alisema na kuongeza:
"Madiba aliamini kwamba watu wote ni sawa na hakuweka tofauti zozote baina yao, alipigania uhuru si kwa Afrika Kusini pekee bali kwa Afrika nzima, mafanikio yaliyopatikana yamekuwa msaada mkubwa hasa kwetu sisi wanawake."
Naye Rais Zuma aliwashukuru Waafrika Kusini na nchi mbalimbali duniani kwa jinsi walivyowafariji wakati wote wa msiba.
Alisema siku kumi za maombolezo zilikuwa ngumu sana kwao, lakini zilionyesha wazi kwamba watu walimpenda na kumjali Mzee Mandela.
Rais Zuma kabla ya kuanza hotuba yake aliongoza wimbo uitwao Thina Sizwe, wimbo ambao uliimbwa 1962 nje ya gereza wakati Mandela na wenzake walipohukumiwa kifungo cha maisha.
Mandela alizikwa jana kwa taratibu za kimila na hakuna mtu nje ya familia aliyeruhusiwa kushuhudia mwili wake ukishushwa kaburini.
Itakumbukwa kwamba tangu kutokea kwa kifo cha Mandela siku 10 zilizopita, haikuwahi kuwekwa wazi ni sehemu gani katika makaburi ya familia, kaburi la Mandela limechimbwa wala aina ya kaburi hilo.
Serikali kupitia kwa Waziri katika Ofisi ya Rais, Collins Chabane alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba: "Familia ya Mandela inataka mazishi yawe ni siri na hakutakuwa na upigaji wa picha wakati mwili ukishushwa kaburini."
Share on Google Plus

About feisal pinto

Computer Application Student, Author, Short Stories Writer, Business Proposal Writer, Presenter and Application Builder. Email feisalpinto4@gmail.com for complains and business only.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment

ad