SERIKALI imepata mfadhili wa kugharamia mradi wa ujenzi wa barabara ya juu (flyover) ambayo itakuwa ya kwanza nchini. Makubaliano ya ufadhili huo yamesainiwa jijini Dar es Salaam leo kati ya Japan na Tanzania.
Kaimu Balozi wa Japan nchini, Kazuyoshi Matsunaga amesema wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo kuwa serikali ya Japan itatoa msaada wa Yen 195 milioni, ambazo ni sawa na Sh. 77.35 bilioni za Tanzania.
Balozi Matsunaga amesema kiasi hicho ni nyongeza ya kilichotolewa awali kutokana na kukabili upungufu wa bajeti uliosababishwa na kushuka kwa sarafu ya Tanzania pamoja na ongezeko la bei za vifaa vya ujenzi.
Japan iliongeza Yen 1,722,000,000 ambazo ni sawa na Sh. 25,639,000,000 za Tanzania, alisema Balozi Matsunaga mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile aliyeiwakilisha serikali ya Tanzania.
Mkataba kwa ajili ya mradi huo utasainiwa Mei mwaka huu kati ya serikali na mkandarasi na matarajio ni utekelezaji kuanza mara moja.
Barabara ya juu itajengwa eneo la makutano la TAZARA, zinapounganika barabara ya Mandela na Nyerere. Ni mradi unaolenga kupunguza msongamano wa magari yatokayo Bandari ya Dar es Salaam na uwanja wa ndege wa kimataifa wa JK Nyerere.
“Mradi utasaidia kurahisisha usafirishaji mizigo katika bandari inayotegemewa kimataifa na hivyo kusukuma kasi ya ukuaji wa uchumi,” amesema Dk. Likwelile.
Amesema ni mradi mkubwa utakaopunguza gharama za usafirishaji mizigo ndani na nje ya nchi na kuwa kichocheo cha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam inayotegemewa na nchi kadhaa za jirani.
0 comments :
Post a Comment