WAZIRI Kivuli wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’ amebeza mafanikio ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania chini ya Rais, Jamal Malinzi na kulaumu kuhusu kusitishwa kwa tiketi za elektroniki kwa lengo kuwanufaisha baadhi ya watendaji.
Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni kuhusu mapato na matumizi ya wizara hiyo, Sugu alisema katika kipindi cha aliyekuwa Rais wa TFF, Leodigar Tenga michezo ilikuwa inakua kwa kasi lakini tangu aingie madarakani, Malinzi anasema anachojivunia ni kuonesha moja kwa moja mechi 12 za Taifa Stars kwenye televisheni.
Sugu alisema ni wakati mwafaka kwa Tanzania kutumia makocha wazawa ili kuhakikisha kuwa soka linakua na timu ya taifa kufanya vizuri, kwani mfano upo iliwahi kunolewa na Joel Bendera na Zakaria Kinanda na kupata mafanikio.
Kuhusu kusitishwa kwa matumizi ya mfumo wa tiketi za elektroniki (ETS) kwenye Uwanja wa Taifa na vingine uliofanywa na TFF wakati mashindamo ya Ligi Kuu yalipokuwa yakifanyika msimu uliopita, alisema ni mkakati wa serikali kuhalalisha ‘madudu na ulaji’ kwa watendaji wa TFF kwa matumizi ya tiketi za vishina.
Alisema uamuzi wa kusitisha matumizi ya ETS umelenga kurudisha ulaji wa mapato ya milangoni kupitia mauzo ya tiketi za ziada na bandia za mfumo wa kizamani wa vishina.
Sugu ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema) alisema, “Ikumbukwe kuwa tiketi za kielektroniki zilifuta ubebaji wa fedha za mapato kwenye viroba. Hakika tiketi hizo zimekuwa chungu kwa maofisa wa TFF na wizara hii ambao walikuwa wameshazoea kujineemesha kwa kubeba fedha kwenye viroba na rumbesa.”
Alisema taarifa kuwa baadhi ya klabu zililalamikia kutokuwepo uwazi kwa CRDB iliyopewa zabuni ya kutoa huduma ya tiketi hizo, ni za uongo na zimelenga kuweka milango ya ubadhirifu wa mapato ya viingilio kwakuwa CRDB walitoa ‘password’ kuwawezesha maofisa wa TFF kuona moja kwa moja fedha inayoingia kupitia mauzo ya tiketi.
source; Jambo Leo
0 comments :
Post a Comment