Mbeya City ni kama imenogewa na wachezaji waliowahi kuichezea Simba baada ya hivi karibuni kuongeza mchezaji mwingine wa zamani wa wekundu hao Ramadhan Chombo 'Redondo'
Timu hiyo imemuongeza Redondo kwenye usajili wa dirisha dogo lililofikia tamati Desemba 15 na hivyo kukamilisha idadi ya wachezaji watano wa Simba ilionao katika kikosi chao hadi sasa.
Mbeya city alianza kuwasajili mabeki wa zamani wa Simba, Haruna Shamte na Juma Nyosso, ambao walikuwa timu hiyo tangu msimu uliopita na msimu huu ikiwasajili kipa Juma Kaseja, Haruna Moshi 'Boban' na Redondo.
Hali hiyo inaonyesha kuwa timu hiyo imenogewa na wachezaji waliowahi kupitia Simba kwani kila mara imekuwa ikiwasajili.
Shamte alijiunga na City akitokea JKT Ruvu, ambayo alijiunga nayo baada ya kutemwa na Simba kwa madai ya kushuka kiwango, wakati Nyosso alijiunga na Mbeya City akitokea Coastal Union alikocheza kwa nusu msimu akitokea Simba.
Simba iliachana na Nyosso baada ya kocha wa wakati huo, Patrick Liewig ambaye kwa sasa anainoa Stand United kuwaacha wachezaji wengi wakongwe wa wekundu wa Msimbazi kwa madai ni watovu wa nidhamu na alitaka kutoa nafasi kwa vijana.
Sakata la kuachwa kwa Nyosso Simba ni kama ilivyo kwa Boban kwani Liewig aliwapiga chini wachezaji wote wazoefu kwa madai ni wasumbufu, na ndipo Boban akatimkia Coastal lakini baadae akaachana nayo kabla ya kuamua kuichezea timu yake ya mtaani ya Friends Rangers na sasa yuko Mbeya City.
Kipa Kaseja ametua Mbeya City akitokea Yanga baada ya kutokea mgogoro wa kimkataba na timu yake hiyo yenye maskani yake Jangwani jijini Dar es Salaam.
Kaseja alijiunga na Yanga 2013 baada ya kutemwa na Simba kwa madai ya kushuka kiwango, lakini hata hivyo hakuichezea Yanga muda mrefu baada ya kutokea kutoelewana na uongozi wa klabu hiyo kwa madai ya kutomaliziwa fedha zake za usajili na mshahara.
Mgogoro huo ulifika hadi katika Mahakama ya kazi kitengo cha Usuluhishi na kuzitaka pande zote mbili kukaa na kufikia makubaliano
Source: MWANANCHI
0 comments :
Post a Comment