Akizungumza na NIPASHE jana, wakala wa wachezaji wa soka anayetambuliwa na Shirikisho la Soka duniani (Fifa), Said Al Maskary, alisema kinachomkwamisha mchezaji huyo ni gharama ambazo klabu zinazomhitaji zitatakiwa kulipa kutokana na mchezaji huyo kuwa na mkataba na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Maskary aliitaja Klabu ya Suur ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Oman kuwa iko tayari kumsajili nyota huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Azam na Simba lakini inashindwa kuendeleza mazungumzo ya kumsajili kutokana na wao kutokuwa na utaratibu wa kulipa ada ya uhamisho, jambo ambalo ni kinyume na taratibu za uhamisho wa wachezaji kote duniani.
Wakala huyo alisema suala hilo limekuwa kikwazo kikubwa na linakwamisha wachezaji kujiunga na timu zenye malipo mazuri ukilinganisha na Klabu za Tanzania wanazozitumikia.
"Kwa kweli inakatisha tamaa, wachezaji wanapata klabu tena wakiahidiwa kulipwa mishahara mikubwa, gari na nyumba ya kuishi lakini wanaishia kukwama," alisema wakala huyo.
Alimtaja mchezaji mwingine ambaye alishindwa kujiunga na timu hiyo ni Zahor Pazi, ambaye alipokuwa African Lyon, uongozi wa klabu hiyo ukiwa chini ya Rahim Zamunda, ulimnyima ruhusa na hatimaye ofa hiyo ilittoweka.
Maskary alieleza kuwa, kwa sasa anataka kumpeleka mshambuliaji wa Chuoni, Nassor Mohammed 'Ozil' na taribu za kumsajili nyota huyo ziko katika hatua ya mwisho.
Aliwataja wachezaji ambao aliwahi kuwatafutia timu nje kwa nyakati tofauti kuwa ni pamoja na Boniface Pawasa, Emmanuel Gabriel, Shekhan Rashid na Bita John.
Alisema mbali na wachezaji wa Tanzania, pia anawatafutia timu za kucheza katika Bara la Asia wachezaji kutoka Cameroon, Nigeria na Ghana na kwa kiasi kikubwa wanafurahia mikataba yao mipya.
Ngasa aliwahi kutakiwa na Klabu ya El Merreikh ya Sudan lakini alikataa kujiunga na timu hiyo mwaka juzi wakati alipokuwa amebakisha muda wa mwaka mmoja wa kuitumikia Azam.
Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema hawana taarifa za Ngasa kutakiwa Oman, na watakapojulishwa rasmi watafanya mazungumzo na klabu husika ili kufikia makubaliano.
CHANZO: NIPASHE
0 comments :
Post a Comment