- Ni Ally Awadh wa kampuni ya mafuta ya Lake Oil
- Atuhumiwa kumfanyia unyama mtumishi wake
- Polisi Oysterbay, Kanda Maalumu wamgwaya
Mlalamikaji anayedaiwa kupigwa na mabaunsa wa mfanyabiashara bilionea Ally Awadh (Lake Oil) |
Jumanne, Februari 11, 2014
Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, ameamua “kujipima uzito” dhidi ya bilionea Mtanzania,
Ally Edha Awadh ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Lake Oil ya Mikocheni
jijini Dar es Salaaminayoagiza,
kuuza na kusafirisha mafuta na biashara nyingine nyingi. Awadh
anayetajwa kama mmoja wa mabilionea vijana nchini, amefunguliwa
mashitaka Polisi ya kumteka, kumdhalilisha kinyume cha maumbile na
kumpora mali mmoja wa wafanyakazi wake.
Uamuzi wa
Waziri Mkuu Pinda umekuja baada ya Jeshi la Polisi nchini, katika kile
kinachoonekana ni kumgwaya bilionea huyo, kupuuza kumsaidia mlalamikaji
huyo mwenye umri wa miaka 32. Kwa sababu za kiutu na za kitaaluma, jina
la mlalamikaji tunalihifadhi kwa sasa.
Hatua ya Pinda
imetokana na barua ya mlalamikaji ya Novemba 29, mwaka jana
aliyomwandikia baada ya Jeshi la Polisi-kuanzia Kituo cha Oysterbay,
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na hata Makao Makuu, kupuuza kumsaidia
mlalamikaji ili aweze kutendewa haki.
Baada ya
kuipata barua ya mlalamikaji, Pinda alimwagiza msaidizi wake, Leila
Mgonya, amwandikie barua Katibu wa Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi. Kazi hiyo ilifanywa Desemba 29, mwaka jana.
Katika barua
hiyo ya Pinda iliyoandikwa kwa niaba yake na Mgonya, inasema, “Miongoni
mwa mambo aliyofanyiwa mlalamikaji na mwajiri wake (Awadh) ni pamoja na
kupigwa na kujeruhiwa mwili mzima kama picha zilizoambatanishwa na barua
ya mlalamikaji zinavyoonyesha, kudhalilisha pamoja na kudhulumiwa mali
zake kama inavyobainishwa katika barua ya mlalamikaji.
“Kwa kuwa
suala hili limejikita zaidi katika utendaji wa Jeshi la Polisi,
imeelekezwa kuwa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ishughulikie suala
hili kikamilifu kwa lengo la kumsaidia mlalamikaji kupata haki yake kwa
mujibu wa sheria na kuona kuwa haki inatendeka.
“Aidha,
Mheshimiwa Waziri Mkuu angependa kupata mrejesho kuhusu suala hili.
Tafadhali mfikishie Mheshimiwa Waziri maelekezo hayo ya Mheshimiwa
Waziri Mkuu.”
Pamoja na
maagizo hayo ya Waziri Mkuu, JAMHURI imebaini kuwa hakuna hatua zozote
za maana zilizokwishachukuliwa dhidi ya Awadh na washirika wake.
Barua ya mlalamikaji kwa Waziri Mkuu
Mlalamikaji
katika barua yake kwa Waziri Mkuu, anaanza kwa kusema, “Mheshimiwa, jina
langu lipo hapo juu ni kijana wa Kihidi (Mtanzania) umri wangu ni miaka
32 mzaliwa wa Tanga, nina mke na watoto.
“Mheshimiwa,
nimesomea uhasibu na nimefuzu mwaka 2004 masomo yangu… na nikaajiriwa na
Ally Edha Awadh katika kampuni yake iitwayo Lake Oil Ltd Septemba, 2010
na kuwa Finance Manager (Meneja Fedha) katika kampuni yake.
“Bila
matarajio yangu, ilipofika Mei 2, 2013 mwajiriwa mwenzangu aitwaye Ahmed
alifika ofisini kwangu na kuniarifu ya kwamba naitwa na Mkurugenzi Ally
Edha, ilikuwa saa 11:30 za jioni Alhamisi na bila kusita nikaongozana
naye hadi kwa Ally Edha nikifahamu naitwa kwa ajili ya kazi kiofisi.
“Nilishangaa
nilipofika tu ofisini kwake akahitaji simu yangu, nikampa mara
akamuagiza stafu mwingine aitwe Fahim akafuate laptop yangu na vifunguo
ya gari yangu ofisini kwangu na ofisini kwake tulipobaki mimi, yeye na
Ahmed. Alianza kunitukana na kuniambia mimi ni mwizi nimemwibia dola
milioni 10 za Marekani (Sh bilioni 16).
Mara
ilipoletwa laptop yangu na funguo za gari akanichukua na kuniagiza
nimfungulie e-mail yangu. Nilikataa na kumwambia hii ni mail yangu
binafsi na siyo ya ofisi yake, siwezi kufungua pana kazi za wateja wangu
wengine (mimi ni mhasibu wa wengi). Akanitishia kunipeleka Polisi, nami
nikamkubalia.
“Mheshimiwa,
tukifuatana na wafanyakazi wake wengine, Ahmed, Fahim, yeye na K.V
Choudry, tulishuka chini na kuingizwa katika gari ya Ahmed. Gari
ikawashwa na mara akamuagiza dereva Ahmed lile gari tulilopanda
lipelekwe godown (ghala) ili abadilishe gari kwenda Polisi. Cha
kushangaza nikaamrishwa nishuke pale godown na kuingizwa ndani, pamoja
na wale tuliofatana nao. Nilishangaa kuwakuta wengine wawili (yeye Ally
Awadh anadai ni mabaunsa wake) wanaitwa Waitey na mwingine ni Abeid.
Mabaunsa waanza kumlawiti
“Mheshimiwa,
wakajumuika pamoja wakanivua nguo, wakanilawiti. Wakanipiga sana kwa
kutumia nondo, mikanda mizito, makonde ya nguvu na huku huyo mtumishi
mwenzangu Ahmed akiwa ameielekeza pistol (bastola) kichwani kwangu kwa
kuniambia leo ni kifo changu endapo nitakataa kuyakubali anayotaka bosi
wake, yaani Ally.
“Mheshimiwa,
mateso haya yalikuwa zaidi ya masaa mbili na nusu (zaidi ya saa mbili na
nusu) nikilazimishwa nikubali kutoa kila kitu changu (assets) nimpatie
yeye, vinginevyo wataniua na wakanionesha picha za maiti wawili
zilizokuwepo katika simu ya baunsa wake akidai (Ally) angeniua kama hao,
na kunifunga katika mfuko wa plastiki na kunipeleka shambani kwake Soga
kunizika.”
Mlalamikaji
anaendelea kumweleza Waziri Mkuu kwamba kutokana na mateso makali na
vitisho alivyopewa, alilazimika kukubaliana na maelekezo aliyopewa, yote
hiyo ikiwa ni mbinu ya kunusuru uhai wake.
Apigwa picha akiwa uchi
“Ndipo Ally
Edha akanipiga picha nikiwa uchi na kusema endapo nitaenda Polisi, yeye
atazitoa hizo picha kwenye mitandao ya intaneti kunidhalilisha. Hivyo
nikapewa shati langu nivae na kupelekwa ofisini kwake na kulazimishwa
niandike kukubali kwamba vitu vyangu vichukuliwe,” anasema.
Kwa mujibu wa mlalamikaji, mali zilizochukuliwa ni:
A: Nyumba yangu na mke wangu iliyopo Nairobi, Kenya
B: Gari zangu mbili (i) Toyota IST T786 BZG (ii) Toyota Fortuner T503 BQC
C: Bastola yangu 6mm niliyonunua Mzinga.
D: Fedha taslimu dola 100,000 (Sh zaidi ya milioni 160)
E: Mkataba wangu wa nyumba na duka (vyangu) vilivyoko Uhuru Heights
F: Ofa zangu tatu za viwanja Kigamboni
Asainishwa kwa nguvu
“Ndipo
nikasainishwa; na majira ya saa 3 za usiku wakanitia katika gari aina ya
Navara nyekundu mali ya kampuni –dereva akiwa Ahmed wakiwamo mabaunsa
wawili, Ally Edha, na mimi. Hadi nyumbani kwangu Upanga.
“Mheshimiwa,
inasikitisha kwa sababu mke wangu alipopiga simu nikiwa kwa Ally
alinilazimisha niongee na mke wangu kwa lugha ya Kiingereza, na siyo
Kihindi. Alikuwa anapiga kwa kutoamini kwa nini niongee Kiingereza
badala ya Kihidi hadi simu ikaisha pesa ndipo tulipofika tukamkuta yupo
chini anangoja aletewe vocha na mlinzi.
“Wakanibadilisha
shati na kunivisha la Abeid (langu lilijaa damu). Wakamweka chini ya
ulinzi mke wangu. Tukapanda juu nyumbani hadi sitting room
wakamnyang’anya simu na kumkalisha chini. Ally Edha akanilazimisha
nimpeleke bedroom (chumba cha kulala), ndiye akazichukua documents
(nyaraka) zote na hizo pesa na mara wakaingia Choudry, Sree Kumar na
Ramana ambao wote ni wafanyakazi wake; na ni Wahindi wakiwa na laptop na
printer.
“Ghafla wakiwa
na hizo laptop huyo Choudry na Kumar wakaelekezwa kuandika maneno ya
mkataba ambayo mimi na mke wangu tukalazimishwa kuweka sahihi zetu
kukubali kuzitoa mali zetu kwa huyo jambazi Ally. Nakumbuka hata watoto
wanalia kutaka maziwa nyumbani Ally Edha alizuia wasipewe.”
Mlalamikaji
anaendelea kusema kwamba akiwa na maumivu makali, Ally Edha alitaka siku
ya pili amtolee pesa katika akaunti yake iliyopo katika Benki ya
STANBIC, Tawi la Nyerere Road; na akasema angezifuata hizo fedha siku ya
Jumamosi.
“Alizijua hizo
fedha kwa sababu ni akaunti niliyoitumia kuweka pesa za mshahara.
Mshahara wangu ulikuwa Sh. milioni 6 kwa mwezi. Kama hilo halikutosha,
alikuta chumbani kwangu vitabu vitatu vya hundi za akaunti ya pamoja na
mke wangu; Standard Chartered (Nairobi, 2), Benki ya Exim (3), Benki ya
NBC, akatulazimisha tuzitie sahihi zetu- na tukafanya hivyo.”
Mlalamikaji, mkewe waonywa watauawa
“Siku hiyo
aliniambia mimi na mke wangu kwamba kama angesikia tumemueleza mtu
yeyote haya mambo, angetuua. Kweli tukaogopa sana hadi siku ya tarehe 4,
2013 ndipo alipomtuma Sree Kumar kuja kuchukua zile milioni 22
alizoagiza nizitoe katiba akaunti yangu ile siku ya tarehe 2 Mei 2013.
Nilimkabidhi Sree Kumar akampelekea Ally Awadh.
“Mheshimiwa,
nakumbuka namna tarehe 8 Mei, 2013 Choudry (Mfanyakazi wa Ally Awadh)
alinitumia meseji mbili kwa kutumia simu yake kwamba angependa aje
nyumbani waniletee pochi waliyochukua siku ya tukio nyumbani kwangu
ambayo ni ya mke wangu yenye kadi yake ya ATM na kopi ya leseni ya
udereva. Nikawaambia sitokutana nyumbani, tukapanga anikute Mtaa wa
Morogoro/Jamhuri akaleta akanikabidhi bila ya kunisalimu.”
Danadana za Polisi Oysterbay
“Mheshimiwa
Waziri Mkuu, siku ya Jumamosi tarehe 4 Mei 2013 nilipatiwa wakili
aitwaye Mwanganga. Nikamueleza, akaamua tukamuone RPC Kova (Kamanda wa
Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam). Tulifika saa za mchana, nikamueleza
na nilipotaka kumwonyesha majeraha yangu alikataa na kusema kuangalia
majeraha sio kazi yake ila alipiga simu Oysterbay akatuagiza twende.
Tukafuatana na wakili hadi Oysterbay.
“Mheshimiwa,
hiyo tarehe 4 Mei 2013 tulifika Oysterbay tukamuona ofisa mmoja
simfahamu jina ila sura namfahamu (wakili wangu anamfahamu). Hakuonekana
kujali sana, ndipo akatupeleka ofisi nyingine (wakili anaifahamu). Hapo
huyo askari akamuita mama mmoja polisi ndipo akatupeleka ofisi
nyingine, ofisa akamuagiza andike maelezo naye akanisikiliza na
akanipeleka kwa ofisa mwingine. Huyo ndiye aliandika maelezo yangu.
“Cha
kushangaza huyo ofisa alianza kusema ‘wewe tayari umetajwa kwenye kesi
nyingie ya Lake Oil’, lakini tukamwambia aandike maelezo yangu. Yeye
alidai ‘pana Mhimdi mmoja, Mukesh ambaye ni Internal Auditor (Mkaguzi wa
Ndani) wa Lake Oil yupo ndani rumande hapo, na wewe pia unapaswa uwekwe
ndani’. Lakini huyo ofisa na mwanasheria wangu walitoka nje. Cha
kunishangaza wakili akanimbia eti inatakiwa niweke dhamana nikatibiwe
ili Jumatatu nirudi au nipelekwe kutibiwa nirudishwe rumande. Lakini
wakili baadaye alinifahamisha wameyamaliza- kampatia Sh 100,000; hivyo
ningepaswa nimrejeshee hizo pesa.
“Hivyo
statement (maelezo) iliandikwa na nikapewa medical examination report
yenye case file no. OB/RB/7853/2013 ya tarehe 4 Mei, 2013. Ndipo
nilipoenda Sinza Hospitali kwa matibabu.”
Woga wamfanya akimbilie Zanzibar
Mlalamikaji
anasema kutokana na woga wa ahadi za mateso zaidi au kuuawa kama
alivyoahidi Awadh, aliamua Mei 5 aende mafichoni Zanzibar.
“Tarehe 6 Mei
nilipigiwa simu na Mutafungwa aliyejitambalisha kwangu kwamba yeye ni
OCD wa Kinondoni akisema amesikitishwa kuisoma statement yangu na
angependa kukuona. Hivyo nikarejea Dar es Salaam na tarehe 7 Mei
nikaenda na kaka yangu na wakili wangu. Tukamwona, akaagiza kwa ofisa
mwingine wa CID kumweleza hiyo kesi ni ya ukweli kwa hiyo wakamatwe
wahusika mara moja na kuniagiza nishirikiane naye.
“Baada ya siku
mbili, yaani Mei 9, nikapigiwa siku na Salum (CID Osysterbay)
akanieleza yeye ndiye mpelelezi wa kesi yangu na angependa kuniona.
Tahere 12 Mei nilimuona Salum. Kwa sababu ya kuwa Zanzibar ndiyo maana
nilichelewa kumuona. Akanisikiliza na kusema angepeleleza hiyo kesi na
angeniita.
“Mheshimiwa,
kila mara huyu Salum hakunipa msaada ipasavyo kwa madai kwamba hajamuona
Ally Edha. Nilishangaa sana sababu ofisi ya Ally Edha ipo, wanaijua na
iweje waseme hawamuoni? Baada ya muda, katikati ya Mwezi wa Ramadhani,
Salum aliniita na kuniambia mwenzake aitwae James angeweza kunisaidia
kuipata silaha yangu kutoka kwa Ally na nikamuona huyo James ambaye
aliahidi Ally Edha akirudi safari yake kwa asilimia 90 nitapata pistol
(bastola) yangu. Akasisitiza pia akimuona siku ya kwanza tu Ally
angenipatia hiyo bastola.”
Aombwa chochote akishasaidiwa
“Nakumbuka
katikati ya Oktoba, mwaka jana Salum alinipigia simu akasema James
anauliza endapo akinisaidia kuipata hiyo bastola mimi ningempa zawadi
gani. Nikamjibu, ‘Nitampatia anachotaka’ ilimradi nipate bastola na vitu
vyangu.
“Mheshimiwa, Nashangaa tangu wakati huo walipoanza kutaka chochote kwangu, hawajanipigia tena, wala kunisaidia.
Nami
nilishajiandaa kuwakamatisha kwa rushwa. Nikaendelea kupata matatizo ya
kujificha kwa kuamini Ally Edha ana mamlaka ndani ya Jeshi la Polisi na
anaweza kunifanyia chochote atakacho.
“Mheshimiwa,
Nikashauriwa niende kutoa taarifa Makao Makuu ya Polisi (wizarani).
Hivyo tarehe 27 Novemba, mwaka jana nilienda huko nikamuona Bwana Laizer
ambaye ni Kamishna. Nikamueleza na nikamuonesha vielelezo. Alisikitika
sana na hapo alimuagiza RPC wa Kinondoni ashughulikie hilo jambo na
amueleze kwa kila kinachoendelea.
“Hadi leo
tarehe 29 Novemba, nimeamua nikatumie barua hii na vielelezo vyangu ili
unisaidie, kwani polisi hawanisaidii tangu nifanyiwe unyama huu.
Najiuliza na kujiona mkiwa kwa kuamini kwamba huyu Ally Adha Awadh yupo
juu ya sheria? Iweje polisi wamlinde tangu Mei 2013 hadi leo pasipo
kukamatwa? Mheshimiwa Naomba msaada wako.”
Barua hii ya
mlalamikaji aliweza kupeleka nakala kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Utawala Bora, Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Katibu Mkuu wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), na Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa.
Kwa upande
wake, Awadh amegoma kuzungumza na JAMHURI. Mara kadhaa amepigiwa simu
yake, lakini amekataa kuzungumza hata pale simu ilipopokewa. Ametumiwa
ujumbe kwa nyakati na siku tofauti, lakini hadi tunakwenda mitamboni
alikuwa hajajibu.
Ujumbe mmoja ulisema, “Habari za kazi.
Hapa ni gazeti
JAMHURI. Tuna habari za kesi ya … dhidi yako. Tunaomba kujua kama hili
suala unalijua kabla hatujaichapisha. Tangu jana tunaomba utupatie
majibu- bila mafanikio. Tumetekeleza wajibu wetu kitaaluma kwa hiyo
hatustahili lawama. Mhariri”.
CHANZO: Gazeti la Jamhuri
credits: JestinaGeorgeBlog
SIOOO KWELIIIIIIIIIIIIII KUCHAFULIANAAAAA JINAAAAAAAAA
ReplyDelete